Uzalishaji wa kahawa kushuka msimu ujao
Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Kahawa (2011‐2021) unakusudia kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 100,000 ifikapo mwaka 2021.
- Uzalishaji huo utashuka kwa asilimia 23.6 kutoka tani 65,527.7 za mwaka 2018/2019 hadi tani 50,000 mwaka 2019/2020.
- Sababu kubwa ya kushuka ni mzunguko mdogo na kuchelewa kwa mvua kanda ya kaskazini
- Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) yasisitiza wakulima kuzingatia kanuni za kilimo na kuongeza uwekezaji katika zao.
Dar es Salaam. Huenda mapato yatokanayo na uuzaji wa kahawa yakapungua katika msimu wa mwaka 2019/2020, baada ya Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kusema uzalishaji wa zao hilo utashuka kutokana na mzunguko mdogo na kuchelewa kwa mvua katika mikoa ya kanda ya kaskazini.
Katika taarifa ya Hali ya Sekta ya Kahawa Tanzania iliyotolewa na TCB April 2019 inaeleza kuwa katika msimu uliopita wa 2018/2019, matarajio ya uzalishaji wa kahawa yalikuwa tani 60,000 lakini mpaka msimu wa mavuno unaisha wamefanikiwa kuvuka matarajio na kuzalisha tani 65,527.7 zenye thamani ya takribani Sh180 bilioni.
Lakini mafanikio hayo yaliyopatikana huenda yakafifia kutokana na TCB kueleza kuwa msimu ujao wa 2019/2020 matarajio ya uzalishaji yatakuwa tani 50,000 ambapo ni sawa upungufu wa asilimia 23.6 ukilinganishaji na uzalishaji wa mwaka 2018/2019.
Katika uzalishaji huo wa kahawa aina ya robusta inaratajiwa kuzalisha tani 20,000 huku arabika tani 30,000.
Sababu kubwa ya kupungua kwa uzalishaji huo ni mzunguko mdogo na kuchelewa kwa mvua kanda ya kaskazini inayojumuisha mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga ambayo katika msimu uliopita zilizalisha asilimia 7.9 ya kahawa yote.
Soma zaidi:
Hata hivyo, hali hiyo ya kushuka kwa uzalishaji inasababishwa na matumizi kidogo ya pembejeo hususan mbolea, kasi ndogo ya kupokea matokeo ya utafiti yanayotolewa na wataalam wa kilimo na uwekezaji mdogo ikilinganishwa na malengo na mkakati wa kahawa 2011-2021.
Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Kahawa (2011‐2021) unakusudia kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 100,000 ifikapo mwaka 2021 lakini huenda ukatatizwa na tatizo la kuwepo kwa mibuni iliyozeeka pamoja na kutozingatia kanuni bora za kilimo cha kahawa miongoni mwa wakulima.
Kushuka kwa uzalishaji wa kahawa kunaweza kuathiri wakulima wa mikoa 15 wanaotegemea zao hilo la biashara kujipatia kipato kwa ajili ya kuendesha familia zao na kushuka kwa mapato ya fedha za kigeni zinazotokana na usafirishaji wa mazao ya biashara ikiwemo kahawa.
Mathalani, mwaka 2017 kahawa ilikuwa zao la biashara la tatu baada ya korosho na tambaku kwa kuliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni ambapo mauzo ya nje ya zao hilo yalikuwa Sh282.4 bilioni.
Bodi hiyo imeeleza kuwa katika kuhakikisha uzalishaji wenye tija unaongezeka, Halmashauri ziwekeze kwenye kahawa ili kujiongezea mapato na kuwahimiza wakulima kutumia teknolojia ya kisasa itakayoongeza thamani na ubora wa zao hilo.