Utambuzi wa mifugo kwa hereni za kielektroniki wasitishwa kwa miezi mitatu Tanzania
- Ni baada ya zoezi hilo kukumbwa na mapungufu ya kikanuni na utekelezaji.
- Wafugaji walalamikia gharama kubwa kupata hereni hizo.
- Katika kipindi hicho, Serikali kutafuta namna bora kutekeleza zoezi hilo.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesitiza zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki kwa kipindi cha miezi mitatu baada ya kuwepo kwa mapungufu ya kanuni, utekelezaji wa zoezi hilo na gharama kubwa za uwekaji wa heleni hizo.
Serikali ilianza kufanya utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki na kuisajili kwenye mfumo wa utambuzi ili kurahisisha ufuatiliaji wa mifugo na mazao yake Oktoba 21, 20221.
Hata hivyo, zoezi hilo limekuwa likilalamikiwa na wafugaji kwa madai kuwa limekuwa likiendeshwa kibiashara badala ya huduma.
“Serikali imesikia hoja za wafugaji kuhusu mapungufu ya kanuni, usimamizi wake na utekelezaji wake na gharama kubwa ya uwekezaji wa heleni za kielektroniki na kuona haja ya kufanya upya tathmini ya zoezi hilo,” amesema Majaliwa leo Novemba 3, 2022 bungeni jijini Dodoma wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu zoezi hilo.
Serikali imeamua kusitisha zoezi la utambuzi mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki kwa kipindi cha miezi mitatu mpaka Januari 2023 wakati ikiendelea na tathmini ambayo itawezesha kutoa mwongozo wa namna bora zaidi ya kutekeleza zoezi hilo kwa mafanikio.
Utambuzi wa mifugo kwa hereni za kielekroniki ulipaswa kukamilika Oktoba 31, 2022.
Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Udhibiti wa Magonjwa yaenezwayo na Wadudu kutoka Wizara ya mifugo na Uvuvi , Dk Benezeth Lutege akimvalisha hereni ng’ombe kwenye mnada wa Itenge uliopo kwenye Kijiji cha Itenga A, Kata ya Itenga, Wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi Desemba 20, 2021. Picha | FullShangwe Blog.
Hata hivyo, tangu kuanza kwa utekelezaji wa kanuni husika mwaka 2021 hadi kufikia tarehe hiyo, idadi ya mifugo iliyosajiliwa na kutambuliwa ni milioni 5.06 pekee. Hiyo ni sawa na asilimia 11 ya lengo la kutambua mifugo milioni 45.92.
Kutokana na hali hiyo Serikali iliongeza muda hadi Desemba 31, 2022 na baada ya hapo ingechukua hatua kisheria kwa wafugaji ambao mifugo yao haitokuwa na hereni hizo.
Kwa mujibu wa Majaliwa, malalamiko ya wafugaji yamejitokeza zaidi kwenye gharama wanazotozwa ili kupata huduma ya mifugo yao kuwekewa hereni ambapo wanadai ni kubwa kuliko uwezo wao.
Bei elekezi ya kuweka hereni ya kielektroniki kwa mnyama mmoja ni Sh1,750 kwa ng’ombe na Sh1,000 kwa punda, mbuzi na kondoo.
Soma zaidi:
Faida za heleni za kielektroniki
Mfumo wa hereni hizo husaidia kupata taarifa za utambulisho wa utaifa wa mfugo, zikifuatiwa na namba za mkoa mfugo unakotoka, namba za Mamlaka za Serikali za Mtaa ulipo pamoja na taarifa ya mifugo na mfugaji.
Zoezi la utambuzi wa mifugo ni utekelezaji wa takwa la kisheria kulingana na Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji Mifugo ya mwaka 2010 na kanuni zake za mwaka 2011.
Zoezi hilo husaidia urasimishaji wa mifugo, kudhibiti mlipuko wa magonjwa na kudhibiti kuhama hama kwa mifugo kusikozingatia sheria.
Manufaa mengine ni kuimarisha kosafu ya mifugo, kuongeza thamani ya mifugo kwenye masoko, kuwezesha matumizi ya bima na mikopo kwa wafugaji. Upatikanaji rahisi wa mifugo iliyopotea au kuibiwa na kufanikisha Sensa ya Mifugo ili kufanya maamuzi sahihi katika sekta ya mifugo nchini.
Latest
