Utajiri uliojificha ufugaji wa kuku wa kisasa

March 25, 2020 7:08 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Licha ya kuwa kuku wana faida nyingi, bado Watanzania wengi wanafuga kuku wa asili kwa ajili ya kitoweo nakukidhi mahitaji madogo madogo ya familia.
  • Waliowekeza fedha zao katika ufugaji wa kuku wa kisasa waeleza maisha yao yalivyobadilika.
  • Wengi wanashindwa kufuga kuku wa kisasa kwa sababu hawajajipanga.

Dar es Salaam. Kama kuku wangelikuwa wanaongea, hakika wangelikuwa wanapiga umbea wa aina yake kutokana na wingi wao hasa wakiwa bandani. 

Hivyo ndivyo ilivyo katika banda la kuku nyumbani kwa Grace Mzee Tabata Segerea jijini Dar es Salaam.

Banda hilo ambalo limesheheni kuku wa rangi nyeupe, wakubwa kwa wadogo waliotengenishwa kulingana na umri. Hakika sauti zao zitakuvutia kwa vile walivyo wachangamfu. 

Ufugaji wa kuku wa Grace ni wa kibiashara zaidi ambapo amewekeza kufuga kuku wa nyama. 

“Nilianza kama mchezo tu lakini naona biashara inaenda vizuri. Sasa hivi walau naweza kujipatia fedha yangu mwenyewe na kujinunulia baadhi ya vitu,” amesema Grace ambaye tabasamu lake limeonyesha hisia za kufanikiwa.

Mpaka sasa kwenye banda la Grace kuna kuku  80 wa nyama ambao akiwauza atapata Sh480,000 itakayomuweza kuendelea kuishi mjini. 

Grace ni miongoni mwa wanawake na vijana wengi ambao wameamua kuachana na utegemezi na kuamua kutumia fursa za ufugaji wa kuku Tanzania ili kuboresha maisha yao na familia zao. 

Ripoti ya Utafiti ya Mwaka ya Sekta ya Kilimo (AAS 2016/2017) inaeleza kuwa hadi kufikia Oktoba 1, 2017 Tanzania ilikuwa na kuku milioni 44.5 huku asilimia 90.5 ya kuku hao ni wa kienyeji au asili.

Hiyo ni sawa na kusema kwa kila kuku 10 wanaofugwa Tanzania basi tisa ni wa kienyeji ambao hutumika kama kitoweo cha familia.

“Kuku wa asili wamekuwa wanafugwa kama mazoea tu na kwa matumizi madogo madogo kama ya kitoweo na kujikimu kwa tatizo liliopo kwa wakati huo,” inaeleza sehemu ya mwongozo wa ufugaji kuku kwa wakulima wa Tanzania uliotolewa na shirika la Heifer International

Licha ya kuwa kuku wengi wanaofugwa katika mazingira ya asili, bado wafugaji kama Grace wao wameamua kufuga katika mazingira rasmi ambapo wanafuga kuku wa kisasa maalum kwa nyama na mayai (Broilers and Layers) kibiashara. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya AAS 2016/2017 kuku wa nyama mwaka huo walikuwa milioni 1.19 huku mkoa wa Singida ukiongoza kwa kufuga asilimia 19.3 ya kuku hao. Kuku wa mayai walifikia milioni 1.3. 

Kutokana na uzalishaji mdogo wa kuku wa kisasa, vijana wana fursa ya kuwekeza zaidi katika ufugaji huo ili kujiajiri na kujipatia kipato kuendesha maisha. 

Kuku hawa hawana mama hivyo ni jukumu lamfugaji kuweka mazingira ya kuwatunza. Picha| @fugakuku.

Fursa iko wapi?

Tasnia hiyo ya ufugaji ina manufaa mengi. Je, ni kwa namna gani mtu anaweza kuwekeza kwenye ufugaji huu?

Mshauri wa wafugaji ambaye pia ni daktari wa mifugo kutoka kampuni ya Bytrade Tanzania Limited Dk Christowelu Zephania amesema ufugaji wa kuku ni kati ya sekta ambazo haziwezi kukutoa machozi endapo utakuwa umejipanga vizuri.

“Kuku wanalipa. Ni mradi ambao unaweza kutengeneza kuanzia Sh800,000 kwa mwezi,” amesma Dk Zephania.

Mtaalamu huyo amesema kabla ya kuanza, unatakiwa kufahamu unahitaji pesa yako irudi kwa muda gani. Kama unahitaji kurudisha pesa yako kwa haraka, ni vizuri ukafuga kuku wa nyama kwani wanakuwa tayari kwa mwezi mmoja tu.

Kwa kawaida, mtaji wa huanzia Sh4.8 milioni ambao unatosha kukuza vifaranga 1,000, utakodisha banda, utagharamia matibabu ya kuku hao na zaidi  utamlipa msimamizi wa vifaranga hivyo.


Zinazohusiana


Hata hivyo, mtu anaweza kufuga idadi anayotaka kulingana na mtaji wake.

“Hawa kuku hawana mama hivyo wanatuhitaji kuwaangalia. Kama una shughuli zingine, unaweza ukaajiri mtu kwani wanahitaji matunzo.

Ni kama kuosha vyombo vya maji asubuhi na jioni ili kuepukana na maradhi ya homa ya tumbo, kuhakikisha joto lipo sawa na mengineyo,” amesema daktari huyo.

Amesema ili kurahisisha ni vema kukodisha banda ambalo lina kila kitu vikiwemo vifaa vya joto na vyombo.

Siyo lazima ufuge kuku 1, 000 tu, endapo una pesa zaidi, unaweza kufuga kuku zaidi kwani kwa mujibu wa mshauri huyo aliye kwenye fani hiyo kwa zaidi ya miaka 10 wapo watu wanaofuga kuku zaidi ya 30,000 na maisha yao yamebadilika kutokana na kazi hiyo.

Kwa upande wa kuku wa mayai, Christowelu amesema uwekezaji kwenye mradi huu hauhitaji mtu mwenye haraka kwani unachukua walau miezi sita ili kuanza kukulipa.

“Miezi sita hiyo kuna kumlisha, chanjo umeme. Kama hukujipanga unaweza kukimbia,” amesema.

Kwa mtaji wa Sh4.8 milioni unaweza kutengeneza faida ya hadi Sh8000 ndani ya mwezi mmoja. Picha|@fugakuku.

Changamoto za kufuga kuku hao

Christowelu amesema kwa kwaida, ili mradi wowote wa ufugaji wa kuku wa kisasa (wa nyama au mayai) ulipe unahitaji kuwa na uhakika wa pesa ya mradi huo kabla hata ya kuanza ufugaji wako.

Kwa kawaida, kufuga kuku wa nyama inahitaji uwe na uhakika wa walau Sh5 milioni wakati kuku wa mayai ni Sh25 milioni ambayo kugharamia ghrama zote ikiwemo kukodisha banda, kulipa mfanyakazi/ muangalizi wa kuku, chakula, dawa pamoja na fedha ya dharula.

Hata hivyo, baadhi ya watu wanaona ufugaji wa kuku wa kisasa ni mgumu na haulipi kwa sababu wanakosa miongozo na ushauri mzuri wa ufugaji wa kuku hao ambao wanahitaji matunzo kama ya binadamu.

Kwa mujibu wa maelezo ya Mtaalamu Christowelu, ufugaji wa kuku wa nyama ni rahisi zaidi kwani unachukua muda mfupi na hata gharama yake ipo chini ikilinganishwa na ufugaji wa kuku wengine wakiwemo wa mayai na hata chotara.

Je, Unahitaji nini kufuga kuku wa nyama? Fuatilia sehemu ya pili ya makala hii kufahamu hayo na mengine mengi.

Enable Notifications OK No thanks