Sh385 milioni kuimarisha uchunguzi wa saratani kupitia AI, MUHAS
- Ruzuku hiyo imetolewa kupitia mpango wa Google Health AI Developers Foundation Program.
- Kupitia mradi huo teknolojia ya AI itatumika kuchambua picha za kitabibu ili kuboresha ugunduzi wa mapema wa saratani.
Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kinatarajia kupokea ruzuku yenye thamani ya zaidi ya Sh385 milioni kwa ajili kuimarisha matumizi ya teknolojia ya akili bandia (AI) katika uchunguzi wa saratani barani Afrika.
Ruzuku hiyo, yenye thamani ya Dola za Marekani 150,000, imetolewa baada ya Dk Sang’udi Sang’udi ambaye ni mkufunzi katika Idara ya Uhandisi Tiba (biomedical engineering) MUHAS kufanikiwa kupata ufadhili huo kupitia mpango wa Google Health AI Developers Foundation.
Kupitia mradi huo teknolojia ya AI itatumika kuchambua picha za kitabibu ili kuboresha ugunduzi wa mapema wa saratani na kuongeza usahihi katika uchunguzi.
Google Health AI Developers Foundation Program ni mpango maalum wa ufadhili na msaada wa kitaalamu ulioanzishwa na kampuni ya Google kupitia kitengo chake cha afya kwa lengo la kusaidia wabunifu, watafiti na taasisi zinazoendeleza matumizi ya AI katika sekta ya afya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na MUHAS, Februari 18, 2026 mradi huo utasimamiwa kupitia Maabara ya teknolojia zinazoibuka katika huduma za afya (ETH Lab) ya MUHAS na kusimamiwa na Dk Sang’udi.
Dk Sang’udi ambaye pia ni mwanzilishi mwenza wa SarataniAI, kampuni bunifu inayojikita katika uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi kupitia AI ataongoza tathmini ya matumizi ya modeli mpya ya MedGemma kwenye takwimu za wagonjwa barani Afrika.
MedGemma ni mfumo wa AI uliotengenezwa mahsusi kwa ajili ya sekta ya afya, unaotumika kuchambua na kutafsiri taarifa za kitabibu, hususan picha za uchunguzi wa magonjwa kama vile X-ray, CT scan, MRI na picha nyingine za kliniki.
Tathmini ya matumizi ya modeli mpya ya MedGemma inalenga kubaini kama mifumo ya AI iliyotengenezwa zaidi kwa muktadha wa nchi zilizoendelea inaweza kutoa matokeo sahihi hususan kwa magonjwa ya saratani.

Saratani kugundulika kwa haraka
Endapo mradi huo utafanikiwa, unatarajiwa kusaidia vituo vya afya vilivyo na uhaba wa wataalamu wa saratani kufanya uchunguzi wa mapema kwa haraka na gharama nafuu, hatua ambayo inaweza kupunguza vifo vinavyotokana na kuchelewa kugundua ugonjwa huo.
Aidha, teknolojia hiyo inaweza kuwezesha uchunguzi wa saratani kwa idadi kubwa ya watu bila kutegemea miundombinu mikubwa ya kitabibu.
Mbali na ufadhili wa kifedha, MUHAS imesema mradi huo utapata msaada wa kitaalamu na kiufundi kutoka Google, ikiwa ni pamoja na majaribio ya utekelezaji wa teknolojia hiyo katika mazingira halisi na kulinganisha uwezo wake na mifumo mingine ya uchunguzi wa saratani.
Latest