Hatua za kuikomboa Dar es Salaam dhidi ya “msitu wa zege”
- Ni pamoja na kupanda miti katika maeneo ambayo haina miti kabisa.
- Hatua hiyo itasaidia kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
- Wadau wamesema kupanda miti ni jukumu la kila mtu kwa ajili ya kesho yake.
Dar es Salaam. Kuna “meme” au unaweza kuviita vibonzo vilivyokuwa vikisambaa kwenye mitandao ya kijamii vikitania juu ya “malaika wa zamu” kuwa ni mwanafunzi anayejifunza kusimamia jua kutokana na joto kuongezeka.
Binafsi niliona ukweli wa meme hizo siku ambayo niliamua kutembea kutoka kituo cha Mwenge kuelekea Chuo Kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam (TUDARCo) huku nikiwa nimesahau kitambaa cha kufutia jasho.
Itoshe kusema siku hiyo haikuwa moja ya siku pendwa katika siku nilizoishi jijini dar es Salaam. Njiani hakuna miti ulioweza hata kunihifadhi kwa muda mfupi.
Kwa mujibu wa wadau mbalimbali wa mazingira, kupungua kwa miti jijini Dar es Salaam kunaambatana na ongezeko la watu jijini humo ambao wanavutiwa na fursa za kibiashara na uchumi.
Ripoti ya Takwimu Muhimu Tanzania (Tanzania in Figures 2020) ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inakadiriwa kuwa hadi kufikia mwaka 2020 jiji la Dar es Salaam lilikuwa na watu milioni 5.4.
Idadi hiyo iliongezeko kwa asilimia 19.2 kutoka watu milioni 4.3 wa mwaka 2012 au sawa na kusema, ndani ya miaka nane, watu milioni 1 waliongezeka jijini humo.
Kuongezeka kwa watu, kunaenda sambamba na kukata miti kwa ajili ya makazi na kutengeneza maeneo ya biashara.
Ikumbukwe kuwa asilimia 10 ya uoto asilia wa Dar es Salaam unapotea kutokana na ongezeko la watu, ikiwa ni takwimu za mwaka 2019 zilizotolewa na shirika la kimataifa la maendeleo endelevu (ICLEI) kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maendeleo na makazi.
Kasi hiyo ya ukataji miti imekuwa ikichochea mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko, kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari pamoja na ongezeko la joto katika jiji hilo linalokuwa kwa kasi Afrika.
Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2040, kiwango cha joto katika jiji la Dar es Salaam kitakuwa nyuzi joto 36.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo akizungumza Machi 22, 2022 wakati wa uzinduzi wa mradi wa miaka 10 wa utunzaji mazingira ambao utahusisha upandaji wa miti na ukuzaji wa misitu Dar es Salaam na Zanzibar. Picha| Rodgers George.
Suluhu ya athari hizo
Kukabiliana na changamoto hiyo ya mabadiliko ya tabianchi, wadau mbalimbali wameshauri hatua za kuikoa Dar es Salaam kabla haijawa “msitu wa zege” unaosababishwa na kukatwa kwa miti ili kupisha ujenzi wa majengo ya biashara na makazi ya watu.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la kuchochea uoto katika miji nchini Tanzania la Kijani Pamoja, Sarah Scott amesema kuna umuhimu wa kupanda miti katika majiji makubwa kama Dar es salaam ili kukabiriana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
“Ukipanda mti leo, huenda usiutumie wewe lakini vizazi vijavyo lazima watanufaika nao. Tunashirikiana na wadau mbalimbali kupanda miti na kuutunza uoto asili wa Dar es Salaam, ” amesema Scott.
Scott ametoa wito huo katika uzinduzi wa mradi wa miaka 10 wa utunzaji mazingira ambao utahusisha upandaji wa miti na ukuzaji wa misitu Dar es Salaam na Zanzibar.
“Tunaanza na Dar es Salaam na kisha tutaenda Zanzibar,” amesema Scott.
Soma zaidi:
Juhudi za upandaji miti katika jiji la Dar es Salaam ni muendelezo wa makabiliano ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kufanya usafi wa jiji ambayo yanafanywa na Serikali na wadau mbalimbali.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke jijini humo, Jokate Mwegelo amesema juhudi za kupanda miti ni muitikio mzuri kwa mabadiliko ya tabianchi ambazo zilianza tangu enzi za Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
“Tanzania ni kati ya nchi za Afrika ambazo zina ardhi iliyotengwa kwa ajili ya kutunza mazingira,” amesema Mwegelo na kubainisha kuwa ni jukumu la Watanzania kuendeleza juhudi hizo.
“Wito wangu ni kwa makampuni, taasisi na mtu mmoja mmoja kuchukua jukumu la kupanda miti na bustani kuipendesha Dar es Salaam,” amesema.
Juhudi za kupanda miti jijini zimeungwa mkono na wadau mbalimbali ikiwemo balozi, benki ya CRDB, NMB na kampuni ya Nabaki Afrika.
Balozi Msaidizi wa Ireland nchini Tanzania, Mags Gaynor amesisitiza kuwa kazi kubwa ya misitu ni kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kulinda dunia dhidi ya majanga.
“Vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ni suala la kidiplomasia na kipaumbele cha maendeleo kwa nchi ya Ireland. Kwahiyo Serikali ya Ireland inayo furaha kuunga mkono juhudi za Kijani Pamoja katika utekelezaji wa mradi wake ambao utachangia kwa kiasi kikubwa katika kurejesha na kuongeza uoto wa asili na misitu nchini Tanzania,” amesema Gaynor.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la WAN-IFRA-Press Freedom. WAN-IFRA haihusiki kwa namna yeyote na maudhui haya.