Ushindani: Tecno yatambulisha simu mpya sokoni

May 8, 2021 8:31 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni simu ambayo inauzwa kwa chini ya Sh700,000.
  • Inaambatana na kamera nzuri, uhifadhi wa kutosha na skrini ya kufaa matumizi ya wengi.
  • Kamera yake ina uwezo wa MP64.

Dar es Salaam. Fikiria hili, zile picha za ‘selfie’ ulizofanikiwa kupiga na baadhi ya “masuper star” zingeliwezekanaje kama simu yako isingelikuwa na kamera ya mbele? 

Huenda ungelianza kusumbua watu wengine wakupige picha lakini uwazi ni kuwa bila kamera ya mbele, maisha ya kidijitali kwa sasa yangelikuwa na taswira tofauti sana.

Hivi karibuni, kampuni ya nchini China ya kutengeneza bidhaa za kielektroniki ya Tecno imetangaza simu yake mpya toleo la Camon 17.

Toleo hilo linaambatana na simu mbili ambazo ni Tecno Camon 17 na Camon 17 pro ambazo sifa zake kuu ni kamera ya mbele na betri la kutosha kukaa na chaji kwa siku nzima na mengine mengi.

Camon17 inakuja na rangi mbalimbali ikiwemo kijani, blu na silver. Picha| Tecno

Mbivu na mbichi za Camon 17 

Simu ya Tecno Camon 17 ni shindano dogo kwa mtangulizi wake Camon 16 wa mwaka jana. Mbali na kuwa Canon 17 imeshusha baadhi ya vitu kutoka kwa Camon 16, Tecno imesema kamera ya mbele ya Camon 17 haijawahi kutokea katika matoleo ya simu zake.

Ikiinganishwa na Camon 16, Tecno Camon 17 ina kamera yenye uwezo wa Megapixel (MP) 48 katika kamera ya mbele huku kamera kuu ikiwa na MP 64.

Kamera hizo zina uwezo wa kumpatia mtumiaji wake picha nzuri katika mazingira ya usiku na mchana ikilinganishwa na baadhi ya simu za hadhi yake ikiwemo Xiamo, RedMI na hata Oppo.

Pia, kwa mujibu wa jukwaa la uchambuzi wa bidhaa za teknolojia la GSM Arena, ukubwa wa Camon 17 umeshuka hadi inchi 6.55 kutoka inchi 6.8 za Camon 16.

Hata hivyo, betri la simu hiyo bado limebaki kuwa mAh 5000 ambayo kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya simu katika mtandao wa YouTube, Varler reviews, betri la Camon 17 linahitaji saa mbili kuchajiwa na kujaa kwa asilimia 100.

Mtoa huduma kwa wateja kutoka Tecno ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa endapo simu hiyo itawashwa na kukaa bila kutumika, ina uwezo wa kutunza moto kwa siku tatu huku kwa matumizi ya kawaida ya kifaa kwa siku mbili.


Soma zaidi:


Boksi la Camon 17 linakuja na nini?

Katika boksi la simu hiyo utakutana na chaja ya type C ambayo inachaji kwa kasi (fast charger) na waranti ya miezi 13 baada ya kununua simu hiyo.

Zaidi ni spika za masikioni (earphones) na jarada moja kwa ajili ya simu hiyo inayokuja na uhifadhi wa Gigabyte (GB) 128 za RAM (uhifadhi wa kumbukumbu za muda mrefu) na GB 4 za ROM (uhifadhi wa kumbukumbu za muda mrefu).

Uhifadhi huo unatosha kuhifadhi video, picha, muziki, nyaraka na programu mbalimbali katika simu hiyo bila ulazima wa kufuta mara kwa mara.

Simu hii inamfaa mtengeneza maudhui, mwanafunzi na mtu yeyote ambaye anahitaji simu yenye kamera nzuri, nafasi na ukubwa wa wastani.

Kwa mujibu wa mtoa huduma wa Tecno (@tecnotanzania) simu hiyo inauzwa kuanzia Sh420,000 kwa simu yenye ukubwa wa uhifadshi wa GB 128 za RAM na GB4 za ROM. 

Simu ambayo uwezo wake umeongezwa kufikia GB6 za RAM, inapatikana kwa Sh540,000 huku toleo lake la Camon 17 pro ikiuzwa kwa Sh680,000 ambayo uhifadhi wake ni GB256 za ROM na GB8 za RAM.

Simu gani inafuata? Endelea kufuatilia Nukta Habari.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW