Usafiri, biashara kuwa sehemu ya mwelekeo hali ya hewa Dar
- Watatoa mwelekeo wa mvua za msimu na hatua zinazopaswa kuchukuliwa na taasisi mbalimbali.
- Dar es Salaam yaangaliwa kwa jicho pevu kulinda miundombinu yake.
- Ni mwendelezo wa utekelezaji wa Mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali ya Hewa nchini.
Dar es Salaam. Jiji la Dar es Salaam siyo tu ni kitovu cha shughuli za uchumi Tanzania bali ni kiungo muhimu cha biashara inayofanyika katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Umuhimu wa Jiji hilo unatokana na jiografia yake iliyozungukwa na miundombinu ya bandari ya Dar es Salaam ambayo hupokea na kusafirisha mizigo ikiunganishwa na reli ya kisasa kuelekea mikoa ya bara na nchi jirani za Uganda, Congo DRC, Zambia, Rwanda na Burundi.
Hali hiyo imeiweka Dar es Salaam kwenye ramani ya dunia kuwa miongoni majiji yanayokuwa kwa kasi duniani. Lakini iko katika tishio kubwa la mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo ongezeko la joto, kina cha bahari kuelekea nchi kavu na mvua za msimu ambazo zimekuwa na matokeo hasi kwa miundombinu ya usafiri na shughuli za biashara.
“Mabadiliko ya hali ya hewa ni tishio kubwa kwa miundombinu ya mjini, ubora wa maisha na mfumo mzima wa wa shughuli za mjini,” inaeleza sehemu ya Ripoti ya Benki ya Dunia (WB) ya mwaka 2010 kuhusu hali ya hewa ya dunia.
Kulingana na mfumo wa hali ya hewa, Dar es Salaam inapata vipindi viwili vya mvua za msimu kwa mwaka ambapo huanza Oktoba hadi Disemba na Machi hadi Mei. Katika kipindi hicho kwa wafanyabiashara na wakazi wa jiji hilo hali ya miundombinu huwa siyo ya kuridhisha kutokana na mafuriko yanayokwamisha shughuli za uzalishaji.
Maeneo kama Jangwani na Kariakoo yamekuwa yakifurika maji na kusimamisha shughuli za kibinadamu na uzalishaji mali.
Inayohusiana:
Kwa kutambua ujio wa mvua za msimu ambazo zinategemea kuanza kunyesha Oktoba mwaka huu, wataalamu na wanayansi wa hali ya hewa nchini wamekutana kujadili rasimu ya mwelekeo wa mvua hizo.
Rasimu hiyo itatoa picha halisi ya mwenendo wa mvua na kutoa mapendekezo ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa na sekta mbalimbali ikiwemo usafiri na biashara kukabiliana na maafa yanaweza kutokea katika kipindi hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Agnes Kijazi amesema mkutano huo unafanyika Dar es Salaam kwa lengo la kupitia na kuandaa mfumo wa hali hewa katika misimu inayokuja.
Amebainisha kuwa wanasayansi watakuja na mapendekezo mbalimbali yatakayoziwezesha taasisi kufanya maamuzi ya kulinda miundombinu na kuhakikisha shughuli zao haziathiriwi na mabadiliko hasi ya hali ya hewa.
Athari za mvua kubwa ni kuharibika kwa miundombinu na hadha ya usafiri kwa wananchi. Picha| Azaniapost.
Hii ni mara ya kwanza kwa TMA kuwakutanisha wanasayansi kutoka vituo vyote nchini ambapo awali kazi ya uandaaji utabiri ilikuwa ikifanywa na wanasayansi wa Makao Makuu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere (JNIA) pekee.
TMA inatarajia kutoa mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli kwa mikoa inayopata mvua mara mbili kwa mwaka Septemba 6, 2018.
Kufanyika kwa mkutano huo kumekuja ikiwa zimepita siku saba tangu Serikali izindue Mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali ya Hewa (NFCS) Agosti 21, 2018 unaolenga kuimarisha upatikanaji na matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa zitakazochochea maendeleo nchini.
NFCS itatekelezwa kwa miaka saba (2018-2025) ambapo utahusisha shughuli mbalimbali ikiwemo kuimarisha miundombinu, tathmini ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa na njia sahihi za kukabiliana nazo.