Unayohitaji kufahamu kuhusu simu mpya za Google
- Uwezo wa kamera, uhifadhi na betri unaridhisha.
- Kamera ya mbele huenda isiwe mshindani kwa simu nyingi za 2021.
- Earphones za kawaida zimetupwa kule.
Dar es Salaam. Wakati tukielekea mwisho wa mwaka 2021, wadau wa teknolojia nao hawapo nyuma kuhakikisha mwaka unaisha vyema kwa kuingiza bidhaa mpya sokoni.
Kampuni mama ya Alphabet inayomiliki kampuni ya Google imeingiza sokoni simu za Google Pixel toleo la sita (Google Pixel 6 na 6 Pro) ambazo zimezinduliwa mwishoni mwa mwezi Oktoba.
Baada ya kampuni zinginge yaani Apple, Samsung, Infinix na OnePlus kupoa sokoni, sasa ni zamu ya Google.
Unahitaji kujua nini kabla haujaamua kununua simu hizi?
1: Uwezo wa kukaa hewani
Kwa kila anunuaye simu, wengi wao, tamaa kubwa ni kutumia simu kwa muda mrefu ukiwa mbali na chaja.
Uwe na uhakika umeme ukikatika leo na kurudi kesho, unaweza kuendelea kubaki hewani.
Simu za Google Pixel 6 na 6 Pro zimetengenezwa na betri zilizo na uwezo wa mAh4614 na mAh 5003 mtawalia, juu ya Samsung galaxy S21 ambayo ina uwezo wa mAh4000.
Uwezo huo pia ni juu ya One plus 9 na iPhone 13.
Zikilinganishwa na simu nyingine za mwaka 2021 kama Infinix 5A, Google Pixel 6 inasubiri kwa kuwa Infinix uwezo wake ni mAh5000. Pixel 6 pro imetoboa anga kwa pointi tatu.
Google Pixel 6 na Pixel 6 Pro zinaambatana na maboresho ya programu pamoja na muonekano mpya. Picha| Narendra janapati.
2: Picha za kuumiza watu roho
Kwa wapenda picha, huenda nafsi zao zikasuuzwa na Pixel 6 au Pixel 6 Pro ambazo zinaambatana na kamera kuu zenye mega pixel 50.
Pro ina kamera tatu ikiwemo kamera kuu, kamera ya picha za mbali (telephoto) yenye MP48 na kamera ya picha pana (ultrawide) yenye MP12.
Kwa Pixel 6, ina kamera mbili ambazo ni kamera kuu na kamera ya picha pana yenye MP12.
Uwezo huo ni juu ya iPhone13, Infinix Smart 5A lakini ni chini ikilinganishwa na Samsung S21 (MP 64). Hata hivyo, ni sawa na One Plus 9 na 9 Pro ambazo pia zina MP50.
Kwa upande wa kamera ya mbele, Pixel 6 ina kamera ya MP8 huku 6 Pro ikiwa na MP 12. Uwezo huo ni wa chini ikilinganishwa na simu zingine za mwaka 2021 ikiwemo OnePlus, Infinix Note 10 ambazo zina uwezo wa MP16 na Samsung A52 yenye uwezo wa MP32.
3: Uhifadhi kumbukumbu na taarifa
Hiki ni kipengele muhimu kwani uhifadhi wa maudhui yako ikiwemo video, picha, fomu na machapisho unategemea na kiwango cha uhifadhi kinachopimwa kwa “Gigabytes” (GB).
Uzuri wa Google Pixel ni kuwa uhifadhi wake wa kumbukumbu za muda mfupi (RAM) ni GB8 kwa Pixel 6 na GB12 kwa Pixel 6 Pro.
Kwa upande wa uhifadhi wa taarifa, Pixel6 Pro ina uwezo wa GB128, GB256 na GB512. Kwa Pixel 6, uwezo wake ni GB 128 hadi GB256.
Fahamu ya kuwa, uwezo wa uhifadhi wa taarifa na kumbukumbu unachangia kwenye bei ya simu utakayochagua.
Pixel 6 ina kamera mbili na Pixel 6 pro ina kamera 3. Picha| Engeadget.
Mengineyo
Simu hizi zinatumia chaja aina ya type C huku ukubwa wake ukiwa ni inchi 6.45 x 2.99 x 0.35 ambayo ni urefu, upana na unene mtawalia kwa Pixel 6 Pro.
Pixel 6 ukubwa wake ni inchi 6.24 x 2.94 x 0.35 kwa urefu, mapana na unene.
Zote zinatumia mfumo endeshi wa kisasa wa Android 12 huku zikiambatana na uwezo wa kurekodi video zenye uwezo wa 4K ambayo ni zaidi ya “High Definition (HD)”.
Kwa simu zote, tundu la kuwekea “earphones” za kawaida yaani (3.5 mm jack) halipo yaani (3.5 mm jack). Kusikiliza muziki, mtu atatumia earphones za type C au zinazofanya kazi kwa teknolojia ya “blue tooth” ambayo inaunganisha simu na earphones kwa teknolojia ya mawimbi.
Latest



