Yafahamu haya unapotembelea Kigoma ‘mwisho wa reli’

August 4, 2021 12:57 pm · Jane
Share
Tweet
Copy Link
  • Kuna mambo mengi ya kuvutia utakapopata fursa ya kutembelea mkoa huu wa magharibi mwa Tanzania.
  • Usiondoke bila kula migebuka, utanishukuru ukiondoka. 

Ilikuwa ni saa 10:00 alfajiri pale alamu yangu ilipolia. Kwa hofu, nilikurupuka kitandani nikijua nimechelewa safari yangu niliyokuwa nimeipanga kwa muda kidogo.  

Safari za ndege za asubuhi kwangu huwa ni mtihani. Mara nyingi huwa zinanipa maruweruwe kwa kuwa nimeshawahi kuachwa siku za nyuma. Si mara moja ama mara mbili.

Unapoachwa na ndege kwanza inaonesha bayana ni kiasi gani hauwezi kupangilia muda wako na ni dalili za kukosa nidhamu. Hivyo, baada ya kuachwa mara mbili niliapa kuwa sitaruhusu jambo hili litokee tena.

Nimefika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 11:00 alfajiri jambo lililonipa angalau wasaa wa kunywa kahawa yangu. Napenda kahawa haswa.  

Baada ya muda kufika tulipanda kwenye ndege tayari kwa safari ya saa mbili kuelekea magharibi mwa Tanzania, Kigoma. Wenyewe wanakuita “Mwisho wa reli”.

Baada ya saa 2 na dakika 10 hivi tuliingia Kigoma na kukaribishwa na muonekano mzuri wa mashamba ya michikichi tukiwa angani. Kigoma imetukaribisha na kijua kitamu chenye kibaridi kwa mbali.

Si unajua tena ni mwishoni mwa Juni, maeneo mengi ya Tanzania huwa na baridi kiasi ukiachana na ile yenye baridi kali kama Njombe, Mbeya na Arusha.

Kwa wanaofika mara ya kwanza, Kigoma ina mengi ya kuvutia lakini kuna mambo muhimu unayopaswa kuyafahamu ili kufurahia safari yako katika mkoa huu wa mwisho wa reli ama mkoa wa migebuka.  Haya ni baadhi unayoweza kuyafurahia ukiwa mkoani hapa.

Malazi

Kigoma ya sasa si Kigoma ya miaka mitano iliyopita. Kila navyokuja hapa nakuta mambo yamebadilika. Kigoma imekua na inaendelea kukua.

Watu tunapokuwa safarini kuna vitu vingi sana tunazingatia. Kwa mimi bajeti ni kitu muhimu sana. Mahali ninapochagua kulala inategemea na bajeti yangu katika safari husika. Kuna sehemu nyingi unazoweza kulala kulingana na bajeti yako.

Kwa mfano, kwa Sh25,000 mpaka Sh30,000 unaweza kupata sehemu nzuri ya kulala inayozingatia usafi na ulinzi wa kutosha.  Kuna sehemu kama Royal Prince au Malagalasi Lodge. Hizi ni sehemu ambazo nimepata huduma zao japo wanahitaji kujiongeza kidogo upande wa kifungua kinywa.

Kama bajeti yako inakuruhusu, basi kuna sehemu Kama Sunset Vista Hotel na, Mahale Classic Lodge. Katika hizi sehemu mbili nilipenda sana huduma zao. Wanawajali sana wateja. Kifungua kinywa chao kina machaguo mbalimbali kulingana na mahitaji yao. Bei zao katika hizi sehemu mbili zinaanzia Sh60,000 na kuendelea. Kuna sehemu nyingine kama Lake Tanganyika Hotel, Hill Top Hotel zinaweza kukufaa pia kama mfuko wako umetuna kidogo.

Chakula

Chakula ambacho ni lazima utakikuta popote unapoenda unapokuwa Kigoma ni migebuka. Hiki ndicho chakula kinachoitambulisha Kigoma ama kwa Kimombo wanaita ‘Signature food’.  Ukifika mkoa huu, usiondoke bila kula hii kitu. Utasimulia nini sasa kama usipokula? Migebuka ni samaki ambao wanapatikana zaidi Kigoma katika Ziwa Tanganyika na ni watamu iwapo watakaangwa ama hata kupikwa na mchuzi.

Kuna maeneo mengi unaweza kupata chakula kizuri kuanzia kwa Mama Ntilie hadi kwenye hoteli kubwa. Wewe tu.  Mama ntilie wapo wengi unapoweza kwenda kula japo wengi hawana nembo mashuhuri kama migahawa yenye hadhi ya kati na ya juu ambayo ningeweza kuwataja.

Kwa wanaopenda maeneo yenye hadhi kubwa kwa bei ya wastani, Mamboleo Restaurant inaweza kuwa suluhu kwa kuwa wana vyakula vingi vya asili na visivyo vya asili. Unapata vyakula vya aina nyingi pale. Kuanzia migebuka, biryani, ugali, kisamvu…ushindwe wewe tu. Ila bajeti yako angalau wastani wa Sh5,000.

One Lounge ni sehemu nyingine ya kwenda wakati wa usiku. Wana chakula kitamu sana. Unaweza kujaribu figirigisi na ndizi za kukaanga. Unapata msosi na mziki mzuri.

            Kama unapenda ugali kama mimi, kuna aina nyingi ukiwemo wa mhogo na mboga mbalimbali kama nyama, migebuka au dagaa.

Maisha ya usiku

Kuna maeneo mengi ya kujidai ukiwa Kigoma. Ukitaka muziki mzuri hususan ‘live band kuna kaka anapiga kinanda matata sana ufukweni kabisa mwa Ziwa Tanganyika sehemu inayoitwa Masanga Beach. Msosi pia si haba. Hapa ‘vibe’ kama lote.

Kuna maeneo mengine kama Kigoma Park. Hapa unapata msosi mzuri, live band na muziki mzuri.

Utalii

Dr Livingstone Museum and Memorial

Kigoma ni mji wa kihistoria. Kama ni mpenzi wa historia basi Dk. Livingstone Museum and Memorial ni sehemu unahitaji kutembelea. Utajifunza historia ya utumwa na kuelewa mchango wa Dk Livingstone katika kukomesha biashara hiyo. Dk Livingstone alikuwa Mmisionari mwenye asili ya Uingereza ambaye aliishawishi nchi yake kuja Afrika kufanya biashara na kueneza dini ya Kikristo. Waliobahtika kusoma historia hapana shaka waliwahi kumsikia Dk Livingstone.

Mgumile

Hiki ni kijiji ambacho sehemu ya kijiji imemezwa na Ziwa Tanganyika. Kama ni Tomaso kuhusu mabadiliko ya tabianchi, basi nenda sehemu ukashuhudie kwa macho yako. Huduma za msingi kama shule, zahanati, msikiti, chanzo cha maji vyote vimemezwa na ziwa.

Mtaa wa Mgumile umefurikwa na sehemu ya maji ya Ziwa Tanganyika. Kuutembelea mtaa huo nje ya mji ni moja ya vivutio vya kitalii kujifunza namna mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri wananchi wa kawaida. 

Kigoma Mwisho wa Reli

Ukisikia Kigoma mwisho wa reli basi ndo hapo unahitaji kwenda kupaona. Hakuna kwenda sehemu nyingine ukishafika hapo yaani ndo mwisho yaani.

Kuna maeneo mengi ya kwenda kama Hifadhi ya Taifa ya Gombe, Hifadhi ya Taifa ya Mahale, soko la dagaa kule Kibirizi, kwenye maduka ya vitenge, lakini kwa leo tuishie hapo.

Kabla sijaondoka, kama wewe ni mpenzi wa kutazama kuzama kwa Jua (sunset) basi Jua la Kigoma linazama kwa kwa aina yake. Saa kumi na mbili jua kali kabisa. Saa moja na robo ndio muda jua linazama.

Ni jambo la furaha kushuhudia jua likizama ukiwa kwenye kingo za Ziwa Tanganyika. Ni mandhari adimu kwa wanaotembelea mkoa huu. Picha zote|Jane Shussa

Kutazama machweo ya jua na kupiga picha ni moja vitu ninavyopenda kuvifanya aidha nikiwa safarini au nyumbani. Katika picha nyingi nilizopiga, picha za Kigoma ndio ninazozipenda zaidi. Rangi zake ni zenye kukolea na kuvutia. Mfano nilipiga picha ilikuwa na rangi ya nyekundu, rangi ya chungwa pamoja na rangi ya bluu kwa mbali. Picha hii nimeitundika nyumbani kwangu kama sehemu ya kumbukumbu.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW