Safari bado ndefu matumizi ya gesi ya majumbani Tanzania
- Ukosefu wa elimu wachangia watu wasitumie kupikia.
- Gharama na urahisi wa upatikanaji wa mkaa na kuni wachangia.
- Wadau kutoa ruzuku na uhamasishaji kwa wananchi.
Iringa. Wakati wakazi wa mjini wakigeukia matumizi ya gesi ya majumbani (LPG), mwanamke huyu bado ameng’ang’ana na mkaa kama nishati yake kuu ya kupikia nyumbani na katika biashara yake.
Ni Beatrice Lupembe, mkazi wa kata ya Ilala, Manispaa ya Iringa, Mkoa wa Iringa ambaye hatumii kabisa gesi hiyo licha ya majirani zake kuhamasika kutumia.
Gesi ya majumbani (LPG) ni miongoni mwa nishati safi na salama za kupikia ambayo ni rafiki wa mazingira na afya za binadamu hasa kwa wanawake ambao muda mwingi wanajishughulisha na upishi.
Beatrice ambaye shughuli yake kubwa ni kuuza maandazi anasema itamchukua muda mrefu kuachana na mkaa na kuanza kutumia gesi kwa sababu ya mazoea aliyonayo ya kutumia nishati hiyo.
“Mimi nimezoea kutumia mkaa, yaani kutumia gesi tena jamani ni kazi kwangu itabidi wanipe kwanza elimu ya jinsi ya kutumia. Naona itakuwa jambo jipya,” anasema Beatrice.
Matumizi ya mkaa na kuni yamekuwa kichocheo kikubwa cha ukataji wa miti na uharibifu wa misitu ambayo ni muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko, ukame, ongezeko la joto ambavyo vinatishia usalama wa watu na viumbe vingine.
Mama huyo anawakilisha idadi kubwa ya watu nchini Tanzania ambao kuni na mkaa ndiyo vyanzo vikuu vya nishati ya kupikia, jambo linalowachelewesha kufaidika na nishati safi na salama ikiwemo gesi ya majumbani.
Kwa mujibu wa Ripoti Hali ya Upatikanaji na Matumizi ya Nishati ya mwaka 2019/20 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ni asilimia 1.5 tu ya kaya za Tanzania Bara ndiyo zinatumia gesi ya majumbani kwa ajili ya kupikia.
![](/wp-content/uploads/2024/03/9e5824b83a1c4d75ee38f91ba42a7f88a6cf1d45.jpg)
Sababu kubwa inayomfanya Beatrice na wakazi wengine wa Manispaa ya Iringa kutochangamkia gesi ya majumbani ni kukosa elimu sahihi ya faida ya nishati hiyo ya kupikia ikiwemo namna ya kuunganisha jiko na mtungi wa gesi.
Kutokana na kushuhudia matukio ya baadhi ya watu kulipukiwa na gesi na kusababisha majeraha na vifo yaliyotokana na matumizi yasiyo sahihi ya nishati hiyo, imekuwa ikiwapa ugumu kuitumia.
“Baadhi ya watu walikufa na kuumia baada ya mitungi ya gesi kulipuka, sasa mimi sitaki haya yanikute ndiyo maana nimekuwa mzito kutumia hiyo nishati,” anasema Adelina Nkanga, mkazi wa kata ya Ilala katika manispaa hii.
Adelina anasema bei ya gesi iko juu na inaweza kuwa kikwazo hasa katika familia zenye watu wengi ambazo huusisha mapishi mengi na ndiyo maana mtu anaona njia rahisi ni kutumia mkaa na kuni.
Kulingana na wauzaji gesi hiyo mkoani Iringa, mtungi wa kilo 15 unauzwa kati ya Sh48,000 hadi Sh52,000 huku mtungi wa kilo sita ukiuzwa kati ya Sh20,000 na Sh22,000. Bei hizo hutegemea na eneo alipo mteja.
Mama huyo ambaye anafanya biashara ya kuuza bidhaa za nyumbani anasema kwa mtu wa kawaida kupata kiasi hicho cha fedha kwa wakati mmoja inakuwa ngumu ikizingatiwa kuwa kwa familia kubwa wanaweza kutumia mtungi zaidi ya mmoja kwa mwezi.
Mmoja wa wasambazaji wa mitungi ya gesi ya kampuni ya Oryx katika manispaa hii, *John (Jina sio lake) anasema mteja anayenunua gesi yao kwa mara ya kwanza ni lazima wampe elimu jinsi ya kuunganisha mtungi na jiko lakini anapewa maelezo muhimu ya jinsi ya kutumia vifaa hivyo.
“Watu wajitokeze kutumia gesi kwa sababu huko tunakoelekea hatutakwepa kuitumia,” anasema John.
![](/wp-content/uploads/2024/08/bc8f84baaeffb87c09b9a008ba4508bc98344ea0-scaled.jpg)
Mwanga wa matumaini waonekana
Licha ya baadhi ya watu kukosa kabisa mwamko wa kutumia nishati hiyo, wapo baadhi yao ambao wanatumia gesi ya majumbani pamoja na mkaa ili kuweka uwiano mzuri wa matumizi ya nishati.
“Tunatumia mkaa lakini tuna mtungi wa gesi ndani, huu tumatumia wakati wa dharura hasa usiku ili kuokoa muda wa kuwasha mkaa,” anasema Moses Nkwabi, mkazi wa Manispaa ya Iringa.
Baadhi ya wakazi wa manispaa hiyo ambao Nukta Habari (www.nukta.co.tz) wanatumia majiko banifu ya udongo na bati ambayo yanatumia mkaa mchache, jambo linalopunguza kasi ya ukataji wa miti.
Hiyo inaweza kuwa ishara nzuri katika mabadiliko kuelekea katika matumizi ya nishati safi na salama na kuachana kabisa na matumizi ya mkaa na kuni hapo baadaye.
Ikiwa elimu na hamasa itatolewa kwa wananchi, uwezekano wa matumizi ya mitungi ya gesi ya majumbani yakaongezeka nchini. Picha| Scooper.
Nini kifanyike?
Ili kuongeza kasi ya watu hasa wanawake kutumia gesi ya majumbani kwa ajili ya kupikia, wadau wa nishati ikiwemo Serikali na kampuni za usambazaji gesi wanashauriwa kuongeza uhamasishaji na elimu ili watu fahamu faida ya nishati hiyo.
“Uangaliwe uwezekano wa teknolojia ya kutumia gesi iwe inatengenezwa hapa hapa nchini. Mfano kama sasa tunaweza ku-assemble (kuunganisha) pikipiki zetu, basi tunaweza kutengeneza na majiko pia.
“Hii itapunguza sana gharama za kuagiza kutoka nje na kufanya watu wengi waweze kuimudu (hasa wa mijini),” anasema Afisa Programu wa Mtandao wa Jinsia na Nishati Endelevu Tanzania (Tangsen), Thabit Mikidadi.
Mikidadi anasema ikiwa Serikali itapunguza kodi kwenye nishati hiyo na kuweka ruzuku kwenye mitungi mitupu ya gesi, bei ya awali ya kununulia itashuka na wananchi wa kipato cha chini wataweza kumudu gharama zake.
“Kwa kuwa kuna teknolojia mpya kama KOPA-GAS ambayo inamwezesha mtu kununua na kutumia gesi kadiri ya kipato chake iangaliwe upya jinsi ambavyo inaweza kuwafikia wengi maana wengi wa watu hawana uwezo wa kutoka Sh50,000 au zaidi pale gesi inapokuwa imeisha,” anasema mtaalam huyo wa nishati.
Latest
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/download-3-1024x696-1.jpeg?fit=300%2C204&ssl=1)
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/VFLt5vHV7aCoLrLGjP9Qwm.jpg?fit=300%2C169&ssl=1)
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/71f29364436954e34871d65ac6f43839-scaled.jpg?fit=300%2C200&ssl=1)
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/images-96.jpeg?fit=300%2C157&ssl=1)