Ujenzi wa kiwanda kipya Tanga kukabiliana na uhaba wa sukari ya viwandani

February 26, 2025 4:51 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Rais Samia asema Serikali ipo mbioni kujenga kiwanda kipya cha sukari jijini Tanga.
  • Kiwanda hicho kitaongeza uzalishaji wa sukari na kusaidia wakazi kupata ajira.

Arusha. Serikali ya Tanzania imesema inatarajia kuanzisha shamba la miwa pamoja na ujenzi wa kiwanda kipya jijini Tanga ili kukabilana uhaba wa sukari ya viwandani uliopo nchini.

Rais Samia aliyekuwa anazungumza na wananchi wa Pangani leo Februari 26, 2025 ikiwa ni siku ya nne katika ziara yake jijini Tanga  amesema kuwa uamuzi huo utaongeza uzalishaji wa sukari ya kawaida na sukari ya viwandani.

“Kuna suala la sukari la viwandani ambayo hii nayo tunaiagiza kwa wingi nchi za nje, sasa ili kuhifadhi fedha yetu ya kigeni tumeamua kiwanda hiki kijengwe ndani ya jiji la Tanga lakini shamba kubwa la miwa litakuwa pangani,” amesema Rais Samia.

Kwa mujibu wa Rais Samia kiwanda hicho kitawasaidia wananchi wa eneo hilo kupata ajira zitakazokuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa jiji hilo.

Ahadi ya ujenzi ya kiwanda hicho inakuja ikiwa ni miezi sita tangu Rais Samia aagize mawaziri wa viwanda na kilimo kuweka sera nzuri ili viwanda vilivyopo vizalishe sukari hiyo.

Rais Samia alitoa agizo hilo baada ya kiwango cha sukari ya viwandani inayoagizwa nje ya nchi kufikia tani 250,000 jambo linalochangia upotevu wa fedha za kigeni.

“Nina hakika tukivipa kazi viwanda vyetu vya sukari, sukari ya viwandani itazalishwa hapa na tutaokoa fedha za kigeni zinazotumiwa kuagiza nje,” alisema Rais Samia Agosti 24, 2024 akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa  kiwanda cha sukari Kilombero mkoani Morogoro.

Mbali na uzalishaji wa sukari ya viwandani, kiwanda hicho kitachangia uzalishaji wa sukari kwa matumizi kawaida ili kufikia lengo la Tanzania kujitegemea kwa sukari ya ndani ifikapo mwaka 2025/2026 kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo Hussein Bashe.

Kwa mwaka 2024/25 Bashe alisema uzalishaji wa sukari  umefikia tani 392,724 ikilinganishwa na tani 460,048 mwaka 2022/2023 sawa na asilimia 85.4 ya lengo la kuzalisha tani 445,000.

Rais Samia Suluhu Hassan akivuta utepe kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Bagamoyo (Makurunge)-Pangani -Tanga.Picha|Ikulu.

Bashe alitoa takwimu hizo wakati akiwasilisha hotuba ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2024/2025 akibainisha kuwa uzalishaji wa miwa kumefikia tani 4.2 milioni ambazo zimezalisha sukari

tani 392,724 sawa na asilimia 88.25 ya lengo.

Pamoja na hayo Rais Samia ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Bagamoyo (Makurunge)-Pangani -Tanga yenye urefu wa kilomita 256 pamoja na daraja la mto Pangani.

Miundombinu hiyo itachangia ukuaji wa jiji hilo ikiwezesha usafirishaji wa mazao na bidhaa kutoka kiwandani kwenda kwa walaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks