Rais Samia: Majiko banifu, vituo vya kuongeza gesi viongezeke vijijini 

February 27, 2025 6:48 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Hatua hiyo itachochea matumizi ya nishati safi katika maeneo vijijini.
  • Mitungi 452,445 kusambazwa kwa bei ya ruzuku.

Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan amezindua zoezi la ugawaji wa mitungi ya gesi ya kupikia (LPG) 452,445 yenye thamani ya Sh 8.64 bilioni akisisitiza kuongezeka kwa vituo vya kujazia gesi hiyo katika maeneo ya vijijini.

Uzinduzi wa zoezi la ugawaji wa mitungi hiyo kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50 kwa maeneo ya vijijini na asilimia 20 katika maeneo ya  mijini ni miongoni mwa jitihada za Serikali kuongeza matumizi ya nishati hiyo nchini

Rais Samia aliyekuwa akizungumza na wazalishaji wa gesi katika mabanda ya maonesho katika Wilaya ya Muheza jijini Tanga leo Februari 27, 2025 amesema kuwa wazalishaji wa gesi hizo wanapaswa kuongeza vituo katika maeneo ya vijijini ili kuongeza watumiaji.

“ Haya majiko tunayagawa vijijini lakini baada ya wiki mtu anakuwa amebadilisha gesi humu ndani sasa pakubadilisha ndiyo mtihani, anzisheni vituo kule (vijijini) ili mwananchi akihitaji iwerahisi kupata,” amesema Rais Samia.

Mbali na kuhamasisha vituo hivyo vya kuongeza gesi kuanzishwa vijijini Rais Samia amewataka wabunifu wa majiko banifu yanayotumia nishati kidogo pamoja na mkaa mbadala kuwafikia wakazi wa vijijini ambao ndiyo wenye mahitaji zaidi,

“Tunataka watu wa vijijini ndiyo wayapate zaidi, mijini kuna ‘option’ chungu nzima, lakini vijijini mtu akipata jiko lake hili akitoka shamba uji wa mtoto anabandika hapa, chakula hapa mambo yanakwenda jitahidini yawe mengi vijijini,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ametoa hamasa hiyo wakati ambapo ripoti ya Utafii wa Athari za Upatikanaji wa Nishati Endelevu kwa mwaka 2021/2022 inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ikibainisha uwepo wa matumizi makubwa ya kuni na mkaa vijijini kuliko mijini.

Ripoti hiyo ya NBS  inaweka wazi kuwa asilimia 88 ya kaya zilizopo vijijini zinatumia kuni kama chanzo kikuu cha mapishi, kulinganisha na asilimia 6 ya kaya zinazotumia nishati hiyo mjini.

Rais Samia Suluhu Hassan akizindua usambazaji wa nishati safi ya kupikia kwa mkoa wa Tanga katika viwanja vya CCM Jitegemee kabla ya kuwahutubia wananchi wa Muheza mkoani humo tarehe 27 Februari, 2025.Picha|Ikulu.

Idadi hiyo ni sawa na kusema kaya nane kati 10 zilizopo vijijini bado zinazotumia nishati ya kuni kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia. 

Wakati huo huo, asilimia mbili tu ya wakazi wa vijijini ndio wanaotumia nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi.

Matumizi hayo ya majiko ya gesi katika maeneo ya vijijini yako chini mara 17 zaidi ya maeneo ya mijini kama Dar es Salaam ambapo asilimia 34 ya kaya zinayatumia nishati hiyo.

Naye Judith Kapinga Naibu Waziri wa Nishati aliyekuwa akizungumza katika ziara hiyo amesema kuongeza upatikanaji wa vituo vya kusambazia gesi vijijini Benki ya NMB wametoa mikopo kwa wasambazaji hao ili waanzishe vituo hivyo vijijini vitakavyosaidia kuhudumia wananchi kwa urahisi.

Aidha, Kapinga  amesema kuwa Sh 455.7 milioni itatumika kusambaza  majiko 26,400 jijini Tanga, majiko 3,255 yatasambazwa katika Wilaya ya Muheza ili kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks