Uhaba watumishi watia doa uwekezaji sekta ya afya Tanzania

July 31, 2024 2:21 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ujenzi wa vituo vya afya waongezeka kwa kasi ndani ya miaka mitano huku uhaba wa watumishi wa afya ukiongozeka. 
  • Hadi sasa wahudumu wa afya waliopo ni chini ya nusu ya mahitaji yaliyopo nchini. 

Dar es Salaam. Licha ya Serikali kuwekeza kwa kiwango kuboresha miundombinu ya afya, huenda utoaji bora wa huduma za afya nchini ukaendelea kusuasua kutokana na uhaba mkubwa wa watumishi wa afya unaoendelea Tanzania.

Hadi sasa, kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan Tanzania ina uhaba wa watumishi wa huduma za afya kwa asilimia 60, kiwango ambacho ni zaidi ya nusu ya mahitaji ya wataalamu hao muhimu kuokoa maisha ya watu. 

Hii inamaanisha kuwa kwa sasa ni asilimia 40 tu ya watumishi wa afya wanaowahudumia zaidi ya Watanzania milioni 61 katika vituo vya afya 9,366 vilivyopo nchini kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Kwa takwimu hizo zilizotolewa na Rais Samia wakati akihutubia wakati wa kumbukumbu ya miaka mitatu ya urithi wa aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu Hayati Benjamin Mkapa iliyofanyika leo Julai 31, 2024 jijini Dar es Salaam, kati ya wahudumu wa afya 10 wanaohitajika kwa sasa, ni wanne tu wanawahudumia wagonjwa. 

Watumishi hao waliopo kazini wanahudumia wagonjwa mara mbili zaidi ya uwezo wao wa kuhudumia, jambo linalozidi kuzorotesha ubora wa huduma za afya nchini na kutishia maisha ya Watanzania. 

“Suala la nguvu kazi ya afya ni suala gumu kidogo kwani halina matokeo  haraka kwa kuwa ni rahisi zaidi kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya afya, vifaa tiba na madawa kuliko kuwekeza kutengeneza nguvu kazi ya afya,” amesema Rais Samia.


Soma zaidi:Njia rahisi za kulinda macho yako


Serikali imewekeza zaidi katika ujenzi wa miundombinu ya afya na vifaa tiba ndani ya miaka 10 ya hivi karibuni.

Ndani ya mwaka mmoja tu Tanzania iliongeza vituo vya afya 485 vikijumuisha hospitali, vituo vya afya (Health centres) na zahanati, ikiwa ni miongoni mwa ongezeko kubwa kuwahi kurekodiwa ndani ya miaka mitano. 

Vituo vya afya vya umma na binafsi vimeongezeka kutoka 8,881 mwaka 2022 hadi kufikia 9,366 mwaka 2023 kwa mujibu wa takwimu muhimu za mwaka 2023 Tanzania (Tanzania in Figures 2023) zilizotolewa hivi karibuni na NBS. 

Hata hivyo, kumekuwepo na kilio kikubwa katika maeneo mengi nchini hasa vijijini juu ya uhaba wa madaktari, wauguzi, wakunga na watalaamu wengine wa afya jambo linalotia doa uwekezaji mkubwa wa miundombinu uliofanywa na Serikali.  

Kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/25 Tanzania ilikuwa na watumishi wa afya 126,925 hadi Machi 2024 ambao kwa wakati huo walikuwa sawa na asilimia 57.9 ya watumishi 219,061 wanaohitajika nchini.

Baadhi ya viongozi na wahudhuriaji wa kumbukizi ya 3 ya urithi wa aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu Benjamin Мкара katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.Picha|Ikulu

Si tatizo la kuisha hivi karibuni’

Rais Samia amebainisha kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kuwepo kwa uhaba wa watumishi ni Watanzania kuzaliana sana, maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali katika ujenzi wa hospitali na vituo vya afya pamoja na kasi ya ukuaji wa uchumi.

“Tunazaliana wengi mno na mahitaji ni makubwa mno na ndio maana kila tunavyoajiri bado watumishi hawatoshi na kwa bahati mbaya ajira hizi zinaendana na ukuaji wa uchumi…twende tukachape kazi kweli kweli uchumi ukue tupate kuajiri watu wengi zaidi kwenye sekta hizi,” amesema Rais Samia. 

Pia ameutaja mchango mdogo unaotolewa na sekta binafsi na taasisi zisizo za kiserikali kuzalisha watumishi hao kuchangia changamoto hiyo.

Amesema taasisi hizo huwekeza zaidi katika utoaji wa huduma na utekelezaji wa miradi ya afya kwa jamii kuliko kuwekeza katika nguvu kazi ya afya jambo linaloacha mzigo mkubwa kwa Serikali kuajiri watumishi hao.

Uhaba huo wa watumishi unatokea licha ya vyuo vikuu na vyuo vya kati nchini kuendelea kuzalisha mamia ya wahudumu hao kila mwaka.

Mamia kada ya afya wahitimu kila mwaka

Mathalani ripoti ya takwimu za msingi za vyuo vikuu Tanzania kwa mwaka 2023     iliyotolewa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania  (TCU) inabainisha kuwa wanafunzi  5,317 wa kada ya afya ngazi ya cheti hadi shahada ya uzamivu kutoka vyuo vyote nchini walihitimu masomo yao mwaka jana.

Idadi hiyo ni asilimia 9.4 ya wanafunzi 56,520 wa kada zote zilizosajiliwa na taasisi hiyo waliohitimu nchini.

Ili kuongeza wahudumu wa afya na kutatua uhaba wa ajira katika sekta hiyo, Rais Samia amesema Serikali yake imejipanga kutoa ajira kwa kada hiyo kwa kadri ya ukuaji wa uchumi.

Enable Notifications OK No thanks