Uhaba wataalamu wa usingizi, ganzi unavyohatarisha maisha Tanzania

December 12, 2024 11:27 am · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Chama cha wataalamu wa usingizi na ganzi chasema uhaba uliopo ni kati ya asilimia 50 na 80. 
  • Watafiti waeleza maeneo yasiyo na wataalamu hao huwaweka hatarini wagonjwa wakiwemo akina mama na watoto wao wakati wa kujifungua.

Dar es Salaam. Huenda si maarufu sana miongoni mwa watu nchini kama walivyo wahudumu wengine wa afya lakini madaktari wa usingizi ni miongoni mwa wataalamu muhimu katika maisha ya mamilioni ya watu wanaohitaji huduma za upasuaji. 

Kazi kubwa ya madaktari wa usingizi ni kuhakikisha kuwa mgonjwa anayefanyiwa upasuaji mkubwa anachomwa kiwango sahihi cha dawa kitakachomwezesha kuwa nusu kaputi mpaka madaktari watakapomaliza upasuaji husika. 

Hata hivyo, licha ya umuhimu wa wataalamu hao, bado Tanzania inakabiliwa na uhaba mkubwa wa madaktari wa usingizi ambao kwa mujibu wa wadau wa afya usipodhibitiwa utaongeza mzigo kwa watumishi waliopo na kutishia uhai wa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo muhimu nchini.

Uongozi wa Chama Cha Madaktari wa Usingizi na Ganzi Tanzania unaeleza kuwa takwimu zinaonesha kuna uhaba mkubwa wa wataalamu hao ukilinganisha na idadi ya watu nchini wanaoendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.  

Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari wa Usingizi na Ganzi Tanzania (SATA) Dk. Edwin Lugazia anaeleza kuwa hadi sasa kuna wataalamu wa dawa ya usingizi na ganzi waliobobea 100 na iwapo watajumuishwa na wataalamu waliokaimishwa wanafikia 2,000 nchi nzima.

“Hivyo kuna upungufu wa asilimia 50 hadi 80,” anasema Dk Lugazia. 

Timu ya 27 ya madaktari wa China kwenda Tanzania ikikabidhi video laryngoscopes kwa idara ya usingizi ya Hospitali ya Taifa Muhimbili. Picha /Muhimbili Hospital /X.

Kwa mujibu wa viwango vya kimataifa, anasema, watalaamu 20 wa kada nyingine za afya wanatakiwa kuhudumia watu 100,000 wakati watalaamu watano wa usingizi wanapaswa kuhudumia watu 100,000. 

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kulikuwa na watu milioni 61.7, idadi inayoongezeka mwaka hadi mwaka.

Kwa takwimu hizo, mtalaamu mmoja wa usingizi na ganzi Tanzania ana mzigo mara mbili zaidi ya ule unaopendekezwa na Shirikisho la Vyama vya Madaktari wa Usingizi na Ganzi (World Federation of Societies of Anaesthesiologists -WFSA) wa daktari mmoja kuhudumia watu kati ya 20,000 na 25,000.

“Kwenye afya uwe Ulaya uwe wapi wote kama mnapasuliwa mnapewa ‘standard’ (kiwango) moja maana maumivu unayoyasikia ni yale yale anayoyasikia mtu mwingine,” ameongeza Dk Lugazia.

Mtaalamu wa dawa za usingizi, maumivu na ganzi tiba William Astone akimchoma mgonjwa sindano ya ‘Caudal’ kwa ajili ya kudhibiti maumivu sugu. Picha / William Astone.

Visiwani Zanzibar, Waziri wa Afya wa Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui alisema wanakabiliwa na uhaba wa madaktari bingwa na madaktari wasaidizi wa kada ya ganzi na usingizi pamoja na uhaba wa vifaa tiba vya kisasa.

Kwa Zanzibar nzima, alisema wakati wa maadhimisho ya siku ya wataalamu wa Ganzi na Usingizi duniani yaliyofanyika Kikwajuni Jijini Zanzibar Oktoba mwaka huu, kuwa madaktari bingwa wa Ganzi na usingizi ni wanne (4) tu ambao hawatoshelezi kulingana na uhitaji wa tiba hiyo.

Kutokana na uhaba huo, baadhi ya wataalamu wa usingizi hujikuta wakitumia muda mwingi kazini kiasi cha kukosa muda wa kupumzika na kukaa na familia zao kutokana na kuongezeka mahitaji ya huduma hizo mwaka hadi mwaka huku idadi ya wanaoingia kwenye ajira ikiwa ndogo. 

“Wiki inaweza kukata hujamuona mwanao, wakati anatoka wewe ndio unaingia nyumbani,” anasema Julia Mahemba, Mtaalamu Mwandamizi wa Uuguzi na Usingizi wa Hospitali ya Regency Medical Center jijini Dar es Salaam. 

“Nikiwa bado nakuza vitoto vyangu vidogo vidogo natoka zamu namaliza list (orodha) kama hivi naingia nyumbani, unakuta gari ya zamu inarudi inakuja kukuchukua,” anasema Julia ambaye amekuwa akifanya kazi hiyo kwa miaka 35 sasa.

Rais wa chama cha Tanzania Association of Non Physician Anaesthetist (TANPA) akiwa katika kongamano la kisayansi likilofanyika Isamilo mkoani Mwanza. Picha /Julia Mahemba.

Kwa nini watalaamu wa usingizi ni muhimu?

Watalamu hao huhitajika popote pale ambapo unafanyika upasuaji, matibabu ya maumivu, huduma za ICU, kumsafisha mgonjwa mwenye hali mbaya lakini kwa Tanzania wanahitajika zaidi wakati wa upasuaji vikiwemo vituo vyote vya afya vyenye huduma hizo. 

Dk Lugazia anasema kuwa katika ngazi za juu za huduma za afya wataalamu wa usingizi na ganzi wanahitajika zaidi kutokana na kutolewa huduma kubwa za upasuaji. 

‘Si jambo la kupuuza’

Uchache wa madaktari hao unachochea wagonjwa wanaopaswa kupewa dawa za usingizi na maumivu hususan wale wanaofanyiwa upasuaji nchini kuwa hatarini kupoteza maisha. 

Utafiti ulioangazia umuhimu wa kupanua huduma za usingizi na ganzi vijijini nchini Tanzania (Scale up of anaesthesia services in underserved rural Tanzania) wa mwaka 2023 ulieleza kuwa upatikanaji wa huduma bora za usingizi na ganzi unasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza vifo vya kina mama na watoto. 

Watalaam wa afya wakifanya ukaguzi wa watoto wachanga. Picha /Muhimbili Hospital /X.

Utafiti huo, uliofanywa na watafiti 10 wakiongozwa na Dk Elias Kweyamba wa Kituo cha Kimataifa cha Mafunzo ya Afya Tanzania (TTCIH) kilichopo Ifakara mkoani Morogoro, ulibaini kuwa ni watu wawili tu walifariki kutokana na changamoto za dawa za usingizi na ganzi kati ya kesi 2,179 za kujifungua kwa upasuaji (Cesarean deliveries) katika vituo vya afya waliovifanyia utafiti, kiwango ambacho ni cha wastani.  

“Kusingekuwepo huduma za usingizi na ganzi, wanawake wengi huenda wangepoteza maisha na watoto wao,” unaeleza utafiti huo uliofanywa mkoani Morogoro na kuchapishwa katika Jarida la utafiti la BMC Health Services Research.

Utafiti huo unaonya kuwa kwa hali ya sasa ya ukosefu wa fursa za mafunzo na uhaba wa wataalamu hao, “itachukua zaidi ya miongo” kutimiza lengo la kuwa na mtaalamu mmoja wa usingizi na ganzi kwa kila kituo cha afya na hospitali ya wilaya. 

Kwa nini kuna uhaba?

Miongoni mwa sababu kubwa zinazochochea uhaba wa madaktari hao ni pamoja uhaba wa programu za mafunzo maalum kwa madaktari wa usingizi katika vyuo vikuu na vyuo vya tiba, rasilimali za kifedha, uelewa wa jamii, muundo wa huduma za afya, uhamaji wa wataalamu na wengine kubadili fani ya kusomea.

“Kwa mfano mtu anafanya kazi siku 30 bila mapumziko ‘on call allowance’ (posho) anapewa siku 6 mtu anaona kama anafanya kazi muda mrefu lakini bado kitu anachokipata sio kizuri si bora awe muuguzi au daktari wa vitu vingine amalize kazi zake mapema arudi nyumbani kupumzika,” anabainisha Dk Lugazia. 

Upungufu wa wataalamu hao unakuja licha ya kuwepo wahitimu wengi wa kada ya afya ikiwemo ya usingizi ambao wapo mtaani kwa kukosa ajira, jambo ambalo wangetumika wangesaidia kuboresha huduma za afya na kuokoa maisha. 

Hazina isiyotumika

Baadhi ya vijana wa Tanzania waliosoma kozi za udaktari wa usingizi na ganzi nje ya nchi wanasema hadi sasa wamekosa ajira na mfumo hauwatambui licha ya kuwa bado kuna uhaba wa wataalamu hao katika vituo vya afya na hospitali. 

Sarafina Buja, mhitimu wa shahada ya kwanza ya Ganzi na Usingizi kutoka Chuo Kikuu cha CT kilichopo Punjab nchini India, kuna zaidi ya wahitimu watano aliosoma nao ambao hawajui hatma yao huku wengine wakianza mchakato wa kubadili fani zao ili kujiingizia kipato. 

Sarafina anasikitika kuona marafiki wengi aliokwenda nao chuo kikuu kutoka nchi nyingine tayari wameanza kufanya kazi au wanafanya mafunzo kwa vitendo, hatua ambayo ni mbele zaidi ya alipo. 

“Wakati mwingine najihisi kama mzigo kwa sababu wazazi wangu walifanya kazi kwa bidii kunisomesha na siwezi kuwalipa kwa wakati huu, na tayari ni wazee,” anaeleza. 

Wataalamu wa dawa za usingizi, maumivu na ganzi tiba wakiandaa mashine kwa lengo la kuanza majukumu yao.Picha / William Astone.

Tatizo mfumo

Mtaalamu wa ganzi na usingizi Abel Ntungi anasema sehemu kubwa ya vijana wanaosoma fani hii nje ya nchi wanasoma bila kujua mahitaji ya mifumo ya nchi hali inayowafanya wakose fursa ya ajira kwa kutemwa na mfumo.

Anasema vijana wanaosoma kozi hiyo wanapaswa kufahamu mifumo ya afya nchini kwa kuwa kuna mambo yanakubalika ili waweze kutambuliwa na ngazi zote za huduma ya afya nchini. 

“Ni lazima uwe na ‘degree ya medicine’ (Shahada ya udaktari ) halafu ufanye upate hiyo ‘masters’ (Shahada ya Anesthesia. Haiwezi kusimama yenyewe kama yenyewe,” anasema Ntungi.  

Madaktari wakifanya upasuaji wa kutenganisha watoto waliokuwa wameungana (Rehema na Neema). Picha /Muhimbili Hospital /X.

Nukta Habari ilifanya jitihada mbalimbali za kuwatafuta viongozi wa juu wa Wizara ya Afya kupata ufafanuzi wa jitihada zinazofanywa kupunguza uhaba huo bila mafanikio kwa zaidi ya miezi mitatu. 

Waziri wa Afya wa sasa Jenista Muhagama alipotafutwa alielekeza suala hili kwa Katibu Mkuu, Dkt John Jingu ambaye naye hadi ripoti hii inachapishwa alikuwa hajatoa majibu. 

Bosi wa SATA, Dk Lugazia anasema kuwa angalau kwa sasa Serikali inajitahidi kutoa mafunzo ya usingizi na ganzi kwa wataalamu wa ngazi za chini ili kuwakaimisha majukumu hayo ila jitihada zaidi zinahitajika kupunguza uhaba huo. 

Rais wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Dawa za ganzi na Usingizi Tanzania (Tanzania Association of Non-Physician Anaesthetists) Julia Mahemba anashauri Serikali kuongeza maslahi ya wataalamu hao ili kuwavutia wengi zaidi kufanya kazi hiyo na kupunguza uhaba uliopo. 

Visiwani Zanzibar, Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui alisema wamejipanga kuimarisha na kuiboresha taaluma ya usingizi na ganzi kwa kuwasomesha na kuwaendeleza kielimu watendaji wa kada hiyo pamoja na kununua vifaa vya kisasa vitakavyoongeza ufanisi. 

10 thoughts on “Uhaba wataalamu wa usingizi, ganzi unavyohatarisha maisha Tanzania

  1. Ahsante sana kwa taarifa hii kwani hii kazi inahitaji utulivu wa hali ya juu tunapoifanya kwani tukiwwa na uhaba ni kweli ufanisi wake utakuwa sio mzuri tunaonba tuwezeshwe kuendelezwa kielimu na kununuliwa vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa kazi eg video laryngoscope kwenye difficult intubations

  2. Nukta habari nashukuru kwa ufatiliaji mzuri , lakin kwa kuwa nyie ni vyombo vya habari pengine mnaweza kutusaidia kupaza sauti zaidi . Kuhusu wataalm wa dawa za usingizi na ganzi kuna shahada yaan degree imeanzishwa chuo kikuu muhimbili ambapo lengo ndy Hilo la kuwaandaa wataalm hao wa usingizi lakin vijana hao wanakumbana na changamoto kubwa ambayo uongozi nao ni kama kuna changamoto Kwan vijana hao walitakiwa kuandaliwa kama wataalm wa dawa za usingizi lakin kutokana na mambo au pengine ni maslahi ya watu wengine imekuwa ikiwataka vijana hao kusoma masomo mengine kama ya uuguzi jambo ambalo si takwa la serikali na vijana hao wamefanya jitihada nyingi kwa viongozi mbali mbali kuweza kusaidiwa wajulikane kama wataalm wa dawa za usingizi lakin hakuna mafanikio yeyote vijana wanamaliza hawajulikani wao ni kina nani hawajulikani wapo kwenye muundo gani wanalazimishwa kuwekwa kwenye muundo wa kiuuguzi kitu ambacho wao hawakusoma uuguzi wakiwa chuo waliosoma utaalam wa utoaji dawa za usingizi na ganzi kwa miaka minne na mmoja wa utarajali jumla Tano lakin matokeo yake wanamaliza hawajulikani ni kina nani naomba mpaze sauti vijana hao watambulike kama wataalm wa dawa za usingizi na ganzi vile vile miundo Yao ijulikane .. taifa linahitaji wataalm hao kupunguza vifo vya mama na mtoto lakin wenye maslahi Yao na chuki wamekuwa wakija na mawazo Yao yasiyokuwa na fact yeyote.

  3. Naungana mchapidhaji wa hili jarida lakni pia hata katika hawa wanaosoma je mitaala yao inawajenga kwenda kuwa watalamu kamili? Kwamfano hawa Nurse Anaesthesia hawa watu wanasoma miaka mnne hii course lkn kwann mtaala wao hauna misingi iliyo bora kwanini hawapewi haki yao ya kiamasomo akati ni haki yao? Kwanini hawa watu wasifundishwe Pathology,Dissection Anatomy, Anatomy in anaesthesia? Badala yake hawa watu wanafundishwa maswala ya nursing for what purpose akati hawa ni physician kabisa?

    Hawa wanafunzi kila kukicha wanahudhulia katika mahofsi kufatilia hatima yao juu ya hii course lakini watoto wawakulima wanaosomeshwa kwa shida hata tu mtaala yani ambayo ni haki yao wananyimwa? Waliomba mtaala upitiwe upya serikali ikatoa bajeti ya emergency review of carculum na kuahidiwa kuwa nawao watakuwa kama wadau lakini imekuwa tofauti ni kwamba hawahusishwi katika chochote ndo kusema kwamba mtaala unapitishwa kisirisiri au imekaaje wakati hawa nao ni wadau moja kwa moja na ndo wahanga wenyewe?
    Kwanini shahada ilizinshwa mnamo mwaka 2019 huoo mpaka sasa hawa watu hawatambuliki hata kwenye mfumo wa utumishi Tanzania?
    Kwanini clical officers anaruhusiwa kusoma level ya certificate lkn ikifika bachelor huyu mtu haruhusiwi? Kwamb hii course ni ya watu binafsi sio watanzania wote kwamfano kwanini mwanafunzi huyuhuyu wa nursing akitokeq diploma akienda kusoma bacheloranao uwezo wakusoma physiotherapia, audiology, occupation therapy na nk kwanini kuhusu hii course kuna restriction kiasi hiki kwanini huyuhuyu CO anaeruhusiwa kusoma certificate bachelor haruhusiwi hii haiko sawa hata kidgo?
    Kwanini shahda hii ikaboreshwa na ikajisimamia yenyewe ili kufanya maboresho zaidi hasa katika utendaji Yani ikawa na foundation nzuri huku chini mpka juu yani certificate, diploma, bachelor ili hata hawa wanaosoma nje waingie humo humo kwasababu wanavigezo kwanini shahada inafanywa ni kama yawatu fulani,!!
    Wadau wa elimu au wabobezi zaidi kwanini hii course msiiwekee msingi tu mizuri kama hapo juu kwanini isiitwe bachelor in anaesthesia ili kumruhusu huyu CO na nurse mwenye vigezo tu aingie? Na kuboresha zaidi katika utendaji kuepusha kuingiliana katika mjukumu kwamfano ilivo sasa nurse Anaesthesia anaesoma miaka minne huyu mtu anasomeshwa uuguzi wanini while he/she is completely physicion wa usingzi hapa unamwandaa muuguzi au mtoa dawa za usingzi au ndo mtu nusu nusu kama ni kwamba ndio anaandaliwa nurse Anaesthesia kwann wasiendelee kutumika wauguzi tu waliopo ambao ni wengi wanazaliswa kila leo wengne hata hawana ajili harafu unakuja kumuandaa hata huyu mtoa dawa ambae he/she is not competent enough kuhusu anaesthesia ifike hatua Tanzania tuondoe siasa kwenye vitu nyeti kama hivi yani binafsi najiuliza kwann huyu mtu anaeenda kumlanza mgonjwa katika operation haumfundishi Dissection Anatomy ili akaone zile nerves zote vizuri awe complent na zikamsaidie katika utendaji??
    Ukipitia mitaala ya nchi za wenzetu anaesthesia anasoma haya masomo na hata ukiangalia katika improvements kuhusu vifo vitokanavyo na dawa za usingizi na ngazi ni ndgo sana hili ni kwasababu wameboresha katika mitaala yao kwani sisi hili hatuwezi kulifanya jibu ni kwamba inawezekana ila Kuna kitu kilichofichwa ambayo hiki sio afya katika maboresho na utoaji huduma kwa watanzania zile ni afya za watu tupeni haki yetu ya kimasomo ili tuwe aproded hata leo huyu mtu anaesoma hii course awe proud na hata ikitokea kwenda kusoma nje aweze kwa mtaala huu wa sasa huyu mtu ataenda wapi kusoma nini kwasababu mtaala wetu mbovu nasio kwamba kwa bahati mbaya hili lipo chini ya uwezo wa serikali yetu tunaomba wizara iliangalie hili kama wizara ilileta hii course kuandaa wauguzi iseme na kama sivyo ituambie pia watu wanasoma lakn future zao hazionekani kabsa kwanini tunafikq huku? Katika tu hili pamoja naserikali kupambana kupunguza vifo vitokanavyo na hii idara sidhani kama vitapungua kwasababu hata wanasoma sahv hawako motivated kabsa na hawajui hata majukumu yao ni yapo huko makazi kwahiyo sioni kama hii changamoto na upungufu huu ukiisha,,,
    WANAFUNZI WALIOPO CHUO CHA AFYA MUHIMBILI WANAOSOMA SHAHADA YA USINGIZI NA GANZI SALAMA WAPEWE HAKI ZAO ZA KIMASOMO NA WATANZANIA KWA UJUMLA TUNAOMBA MABORESHO YA MTAALA WA ANAESTHESIA ILI MTANZANIA AKAHUDUMIWE KWAMAARIFA YALIYOJITOSHEREZA HATUTAKI KWENDA KUUA WATU KISA MTAALA TUPENI HAKI ZETU TUMEZUNGUKA HOFSI NYINGI TUMEKUWA TUKIAHIDIWA TUTAFANYIWA MABORESHO LAKINI IMEKUWA KAMA WIMBO MNATAKA TUKASABABISHE VIFO HUKO KISA MAARIFA HATUNA HII SIO HAKI HATA KITOGO
    HAKI YETU SISI HAIWAZUII WATU WENGINE KUPATA FURSA NA MAMBO MENGINE

  4. Kuna coarse mpya imeanzishwa Muhas inaitwa BSc Anaesthesia inatoa wataalamu wa dawa za usingizi na ganzi level ya shahada shida mpaka sasa hawana muundo wa kueleweka wa ajira na maslahi Kwani wanakua ranked kama 3yrs coarse wakati ni typically 4yrs coarse

  5. Ni huzuni kubwa sana kwa wataalumu Muhimu kama hawa kutolipwa maslahi hayo kwa wakati, pia kupewa kiasi kidogo cha mshahara. Viongoz wa juu wanahitaji kuliona na kupaza sauti kuhusu hilo @ prof. Janabi. Sema lolote.

  6. Hongereni Sana wote mnaufikisha ujumbe mzuri kwa serikali kuhusu watoa dawa za usingizi lakini pia na sisi tunaopata mafunzo ya dawa za usingizi tuwe wahamasishaji wa wengine kusoma usingizi bila kusahau tuendelee kuiweka Tanzania Kama Kijiji kwenye eneo la kutoa dawa za usingizi kwa maana ya watu wa juu tembeleeni kwenye primary health care ili kuendelea kufanya improvement kwenye upande wa utoaji wa dawa means access efficient and quality anesthesia

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks