Uhaba, mgao wa maji ulivyoziweka rehani afya za watu Dar

December 14, 2022 6:08 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi ya watu wadai kupata magonjwa kama kuhara na homa ya tumbo.
  • Wengine wapata mzio na upele mwilini.
  • Hali hiyo ilisababishwa na kutumia maji yasiyo safi na salama.

Dar es Salaam. “Mimi huwa situmii maji ya kisima au yanayotembezwa kwenye magari kwa kunywa au kuoga, naogopa kupata magonjwa ya matumbo na kuhara,”

Huyo ni Georina Peter, mkazi wa Kunduchi, jijini Dar es Salaam ambaye miezi miwili iliyopita alilazimika kutumia maji ya visima na yanayouzwa mitaani kwa sababu alikuwa hana njia ya kuyakwepa.

Hali hiyo ilitokana na jiji hilo la biashara kukumbwa na uhaba mkubwa wa maji kwa zaidi ya mwezi mmoja na kusababisha huduma hiyo kupatikana kwa mgao na baadhi ya maeneo kutopatikana kabisa. 

Mgao huo ambao sasa umepungua ulisababishwa na kuchelewa kwa mvua za vuli na hivyo kuukosesha maji Mto Ruvu ambao ndiyo chanjo kikuu cha bidhaa hiyo ambayo huzalishwa katika mitambo ya Ruvu Chini na Ruvu Chini mkoani Pwani.

Hata hivyo, matokeo ya kutumia maji hayo hayakuwa mazuri kwa Georina kwa sababu aliuugua ugonjwa wa kuhara na tumbo. 

“Mwanzo nilikuwa sijui nini sababu niliona tu nikinywa hayo maji naendesha sana (kuharisha) na afya yangu haikuwa vizuri,” anasema Georina (44).

Mama huyo mwenye watoto wawili ni miongoni mwa baadhi ya wakazi wa jiji hilo la mashariki mwa Tanzania ambao waliweka rehani afya zao kutokana na kutumia maji ambayo walikuwa hawana uhakika nayo yalikuwa yanatoka wapi wakati wa mgao. 

Katika kipindi hicho ambacho kiliibua mjadala mpana juu ya bidhaa hiyo, baadhi ya watu walitumia fursa hiyo kuuza maji ya visima na madimbwi na wakati mwingine yakiwa machafu ili tu kujipatia fedha.

Sehemu ya mwili wa Neem John, mkazi wa Dar es Salaam ambaye alipata tatizo la ngozi baada ya kutumia maji ambayo anadai yalikuwa na vimelea vya wadudu wakati wa mgao wa maji mkoani hapa. Picha | Lucy Samson.

Neema John (26), mkazi wa Kijitonyama jijini hapa ambaye alikuwa anatumia maji yanayouzwa kwenye madumu mtaani kwake wakati wa mgao, anasema hayajamuacha salama katika mwili wake. 

Maji hayo kwa mujibu wa Neema yalikuwa yanatochotwa kwenye visima vya watu binafsi, licha ya kutokuwa na uhakika yalikuwa yanatoka wapi.

“Ona vipele mwilini mwangu, kabla ya shida ya maji sikuwa hivi najua tu ni haya maji  tunayouziwa ndiyo yamesababisha hali hii,” anasema Neema huku akionyesha mikono yake yenye upele na michubuko.

Wakati wa kuoga, mwili wake ulikuwa ukimuwasha na kulazimika kujikuna mara kwa mara na baadaye kumuachia upele.

“Huu mgao wa maji umesababisha nimevimba mwili nimetokwa na vipele kila sehemu, nilienda hospitali wakasema huenda maji ninayooga ndiyo sababu,” anasema Neema.


Zinazohusiana:


Ni zaidi ya ugonjwa

Baadhi ya watu wamepata mzio wa vitu mbalimbali baada ya kutumia maji wakati wa mgao. Evarista  Mguta (24) mkazi wa Kibamba Chama, Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo aliyekuwa akitumia maji ya chumvi ambayo awali alikuwa hatumii amepata mzio wa kuwashwa katika mwili wake. 

“Nimebadili sana mafuta ya kupaka mwilini zaidi ya mara tatu nikijua chanzo ni mafuta mpaka niliposikia kwa jirani yangu aliyenishauri nikapime huenda tatizo siyo mafuta,” anasema Mguta.

Tangu kuanza kwa mgao huo, Evarista alianza kupata vipele na kuwashwa mwili mzima, kulikotokana na kukosekana kwa maji ya bomba kwenye mtaa wao. Kuna wakati walikaa wiki tatu bila kuyaona maji hayo.

“Kwenye hicho kipindi mwili wangu ulikuwa kama wa kenge kila sehemu upele…nilivyoenda hospitali wakaniambia nina allergy (mzio) na maji ya chumvi,” ameongeza binti huyo.

Ili kukabiliana  na hali hiyo, ilimlazimu Evarista kuoga maji ya dukani, jambo lililomuongezea gharama za maisha kwa sababu alilazimika kutoboa  zaidi mfuko wake kuipata bidhaa hiyo.

“Daktari aliniambia niache kutumia maji ya chumvi sasa nitaoga maji gani mengine na sikuwa na uwezo wa kununua dumu la lita sita la Sh4,000 kila siku,” anasema Evarista ambaye alilazimika kupitisha siku bila kuoga kipindi cha mgao wa maji.

Matumizi ya maji machafu na hali duni ya usafi wa mazingira huhusishwa na maambukizi ya magonjwa kama vile kipindupindu, kuhara, kuhara damu, homa ya tumbo na polio. 

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa kutokuwepo, kutotosheleza au kusimamiwa isivyofaa huduma za maji na usafi wa mazingira huwaweka watu katika hatari za kiafya zinazoweza kuzuilika.

WHO inaeleza kuwa takriban watu 842,000 wanakadiriwa kufa kila mwaka kutokana na kuhara kutokana na maji yasiyo salama ya kunywa, usafi wa mazingira na usafi wa mikono. 

Wakati ambao maji hayapatikani kwa urahisi, watu wanaweza kuamua kupunguza unawaji mikono na hivyo kuongeza uwezekano wa kuhara na kupata magonjwa mengine.

Athari anazoweza kupata mtu akinywa maji machafu

Dk Joshua Sultan kutoka hospitali ya Ahmadiyya ya mkoani Morogoro anasema maji ya visima au yanauzwa kwenye madumu yanaweza kuleta shida ya afya endapo hayatahifadhiwa vizuri.

“Maji yanayouzwa kutoka kwenye visima ambavyo havijasafishwa muda mrefu yanakuwa yamebeba vijidudu na bakteria yanaweza kusababisha magonjwa kama typhoid (homa ya tumbo),” anasema Dk Sultan ambaye amebobea katika tiba ya viungo na mazoezi.

Daktari huyo anasema magonjwa hayo yanayochangiwa na kunywa au kuoga maji yasiyo salama yanaweza kusababisha  kifo ikiwa mgonjwa atachelewa kupata mtibabu.

“Magonjwa hayo yanaweza kuua lakini mara nyingi ni manageable issue (yanazuilika) ikiwa mtu atawahi matibabu,” anasema Dk Sultan huku akitaja magonjwa hayo ikiwemo homa ya matumbo (typhoid), kuhara, kutapika mapunye na kipindupindu.


Tangazo


Wauza maji watoa ya moyoni

Baadhi ya wauzaji na wasambazaji wa maji hasa ya visima waliozungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) wanaeleza kuwa hawawezi kubeba lawana za watu kupata matatizo ya kiafya kwa sababu wao hawazalishi hayo maji yaliyokuwa yanauzwa wakati wa mgao.

John Lumbwago muuza maji maarufu Mtaa wa Bamaga na Sinza jijini Dar es Salaam anasema wakati wa mgao wa maji,  visima vya maji ya chumvi ndiyo vilikuwa njia pekee ya wao kupata huduma hiyo na kusambaza majumbani.

“Nilikuwa nahakikisha nachota maji kwenye visima ambavyo vimechimbwa na kuanza kutumika muda mrefu na siyo vilivyochimbwa wakati huo wa mgao wa maji kwa sababu yana uhakika,” anasema Lumbwago. 

Hata hivyo,  Lumbwago anasema kwa sasa biashara ya kuuza maji imepungua na muda mwingi mkokoteni wake haufanyi kazi kwa sababu huduma ya maji imeanza kurejea kama kawaida.

Idrissa Chingwesa, muuza maji Makumbusho anasema yeye huosha madumu yake angalau mara mbili kwa wiki  ili kuhakikisha usalama wa maji anayoyauza kwa wateja wake.

“Kwenye kusafisha madumu inategemea kama ni kipindi cha jua kali nayasafisha mara mbili kwa wiki kwa sababu jua linasababisha madumu kupata ule ukungu wa kijani jambo ambalo siyo salama kwa afya,” anasema Chingwesa.

Katikati ya mahojiano na wauza maji, akaibuka muuzaji mwingine wa maji ambaye hakupenda kutambulishwa jina lake akikiri kutoyasafisha madumu kutokana na kuzidiwa na oda za wateja kipindi hicho.

“Mimi naomba nikiri kuwa siyaoshagi, nikizidiwa na oda ndiyo sikumbuki kabisa labda wakati huu ambao wateja wamekuwa wachache ndiyo naweza kufiiria kuosha,” anasema muuzaji huyo wa maji.

Unataka kufahamu tahadhari zipi unapaswa kuchukua hata baada ya mgao wa maji kuisha? Usikose sehemu ya tatu ya makala haya itakayoeleza kwa undani mambo ya kuzingatia unapotumia maji ili usipate magonjwa.

Enable Notifications OK No thanks