Jeshi la Zimamoto latangaza nafasi za ajira

November 19, 2025 7:10 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ajira hizo ni kwa ajili ya waombaji wenye elimu ya kidato cha nne, kidato cha sita, wenye ujuzi maalum, na wahitimu wa shahada katika taaluma mbalimbali.
  • Mwisho wa kutuma maombi ni isemba 3, 2025.

Arusha. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limetangaza nafasi za ajira kwa vijana wa Kitanzania wenye sifa stahiki, likiwataka kutuma maombi yao kupitia mfumo wa ajira wa jeshi hilo kabla ya tarehe 3, Disemba 2025.

Tangazo lililotolewa na Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, John Masunga Novemba 19, 2025 linafafanua kuwa nafasi hizo ni kwa ngazi ya Konstebo zikihusisha waombaji wenye elimu ya kidato cha nne, kidato cha sita wenye ujuzi maalum, na wahitimu wa shahada katika taaluma mbalimbali.

Miongoni mwa vigezo vilivyotajwa kwa waombaji ni kuwa na uraia wa Tanzania kwa kuzaliwa, afya njema kimwili na kiakili, kutokuwa na kumbukumbu za uhalifu, kutokuwa na alama za kuchorwa mwilini (tatoo), na kutowahi kutumia madawa ya kulevya.

Aidha, waombaji wanapaswa kuwa tayari kuhudhuria mafunzo ya taaluma ya Zimamoto na Uokoaji, awe hajawahi kuajiriwa Serikalini pamoja na urefu stahiki.

“Awe mwenye urefu usiopungua futi 5.7 kwa mwanaume na futi 5.4 kwa mwanamke, awe tayari kujigharamia katika hatua zote za usaili endapo ataitwa, awe tayari kufanyakazi popote atakapopangiwa baada ya kumaliza mafunzo, awe na umri kuanzia miaka 18 hadi 25,” imeeleza taarifa ya Jenerali Masunga.

Kigezo cha umri kimesogezwa mbele zaidi hadi miaka 28 kwa waombaji wa nafasi za udereva wa magari makubwa, wauguzi ngazi ya stashahada, taaluma za zimamoto na uokoaji, matabibu ngazi ya Stashahada.

Waombaji wengine walioongezewa umri ni mafundi mchundo wa magari, wazamiaji, waogeleaji, wanamichezo, brass band, waandishi waendesha ofisi, Tehama ngazi ya stashahada na mafundi umeme wa ndege ngazi ya Stashahada.

Kwa waombaji wa nafasi ya uzamiaji na waogeleaji watafanyiwa uhakiki kwa vitendo huku madereva wakitakiwa kuwa na leseni daraja E na watakaoitwa kwenye Usaili watafanyiwa uhakiki kwa vitendo kuendesha magari makubwa.

Aidha, waombaji wenye elimu ya shahada wanaoomba ajira katika fani za uhandisi bahari, TEHAMA, uandisi wa ndege, ukadiriaji majenzi (QS), sheria (waliohitimu shule ya sheria kwa vitendo), mafuta na gesi, uhandisi ujenzi, mitambo na umeme nao wameongezewa umri hadi miaka 28.

Maombi yote yanapaswa kufanywa kupitia mfumo wa ajira wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa njia ya mtandao kupitia ajira.zimamoto.go.tz, huku nyaraka muhimu kama barua ya maombi, nakala za vyeti vilivyothibitishwa, cheti cha kuzaliwa, na kitambulisho cha utaifa (NIDA) zikiambatanishwa.

Nyaraka nyingine zinatakiwa kuambatanishwa ni barua ya maombi iliyoandikwa kwa mkono, fomu ya uthibitisho wa siha njema kutoka kwa mganga wa serikali, namba za mitihani ya kidato cha nne na sita, namba ya vyeti vya taaluma kutoka vyuo vinavyotambulika na Serikali ngazi ya astashahada, stashahada na Shahada na namba ya kumbukumbu ya barua ya Utambulisho kutoka kwa Afisa mtendaji wa Kijiji/Mtaa (Kupitia mfumo wa NaPA).

“Zingatia nakala za vyeti vingine kama vipo mbali na vilivyotajwa kwenye aya ya 4(d), (e) na (f) viambatishwe vikiwa vimethibitishwa na Kamishna wa viapo au hakimu, Waombaji wote waandike namba za simu kwenye barua zao za maombi,” imesema taarifa hiyo.

Jeshi hilo limeonya kuwa maombi yatakayowasilishwa kwa barua pepe, posta au kwa mkono hayatapokelewa, huku hatua za kisheria zikitarajiwa kuchukuliwa kwa wale watakaowasilisha nyaraka za kughushi au taarifa za uongo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks