Uhaba wa walimu bado wazitesa shule za msingi, sekondari Tanzania
- Zaidi ya nusu ya walimu wanaohitajika hawapo shuleni.
- Serikali yasema itaajiri walimu uchumi ukiruhusu.
Dar es Salaam. Huenda wanafunzi wa shule za msingi nchini Tanzania hawapati maarifa na ujuzi kwa ubora unaotakiwa kutokana na shule nyingi kukabiliwa na uhaba wa walimu.
Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inaeleza kuwa hadi Februari, 2023 mahitaji ya walimu katika shule za msingi yalikuwa ni 362,189 kwa kutumia uwiano wa 1:45 (Mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45).
Hata hivyo walimu waliopo ni 175,864 ambao wanafundisha wanafunzi milioni 12.36 waliopo nchi nzima katika ngazi hiyo ya elimu. Hiyo ni sawa na kusema kwa wastani, mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 70.
Uwiano huo uko juu kuliko mapendekezo ya Serikali ya mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi wasiozidi 45 katika darasa moja.
Ili kuziba pengo hilo wanahitajika walimu 186,325 au sawa na asimilia 51.44 au zaidi nusu ya walimu waliopo sasa.
Pia, mahitaji ya walimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa shule za msingi ni walimu 4,462 ambapo waliopo ni 1,517 na upungufu ni walimu 2,945 sawa na asilimia 66.
Hata wakiajiriwa walimu wote hao, tatizo la uhaba wa walimu katika shule za msingi linaweza lisiishe kabisa kwa sababu kila mwaka idadi ya wanafunzi wa darasa la kwanza wanaondikishwa inaongezeka.
Mathalan, takwimu za Tamisemi zinaonyesha kuwa katika Mwaka 2023 wanafunzi wa darasa la kwanza walioandikishwa hadi Februari walikuwa ni milioni 1.78 ambapo kati yao, wasichana walikuwa 917,211.
Uandikishaji huo ni sawa na asilimia 109.07 ya lengo la kuandikisha wanafunzi milioni 1.63 na pia ni ongezeko la wanafunzi 60,320 ikilinganishwa na wanafunzi walioandikishwa kwa kipindi kama hicho mwaka 2022.
“Ongezeko hili limetokana na uhamasishaji wa jamii, ujenzi wa vituo shikizi na kuendelea kutoa elimumsingi bila ada,” amesema Waziri wa Tamisemi, Angellah Kairuki wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2023/24.
Shule za sekondari nako bado
Tatizo la uhaba wa walimu siyo tu la shule za msingi bali linazikumba hata shule za sekondari hasa zinazomilikiwa na Serikali.
Tamisemi inaeleza kuwa mahitaji ya walimu kwa shule za sekondari hadi kufikia Februari mwaka huu ni 174,632.
“Waliopo ni 84,700 na upungufu ni walimu 89,932 sawa na asilimia 51.5. Mahitaji ya walimu kwa shule za Sekondari yanatokana na masomo yanayofundishwa,” amesema Waziri Kairuki.
Wachambuzi wa masuala ya elimu akiwemo Richard Mabala wanasema uhaba wa walimu unawakosesha fursa wanafunzi kupata maarifa kwa ukamilifu kuwawezesha kufaulu mitihani yao na kupata stadi muhimu kuboresha maisha yao.
Waziri Kairuki amesema Serikali inaendelea kuajiri walimu kulingana na hali ya uchumi inavyoruhusu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.
Aprili 12 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan aliridhia kibali cha kuajiri watumishi 21,200 wa kada za ualimu na afya, jambo likalosaidia kupunguza uhaba wa watumishi katika sekta hizo nyeti nchini.
Kati ya watumishi hao, 13,130 ni walimu wa sekondari na msingi na waliobaki ni watumishi wa afya.