Uhaba wa maji unavyowatesa Wananchi Mpwapwa

October 1, 2026 7:06 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ripoti ya CAG yabaini upotevu wa maji wenye thamani ya zaidi ya Sh230 milioni katika Mpwapwa. 
  • Mamlaka zataja sababu ikiwemo watu kujiungia maji kyume na sheria.

Dodoma. Ni Saa nane usiku, wakati baadhi ya wanawake wakivuta shuka kitandani au kupata kumbato la wenza wao, lakini kwa wengine akiwemo Joyce Malole (37) hali ni tofauti.

Kwa mwanamke huyo anayeishi katika Kijiji cha Mazae, wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, muda huo anakuwa tayari ameshapanga foleni kwa ajili ya kupata maji yanayotumika katika matumizi  ya nyumbani.

Kwa miaka 10 aliyoishi katika eneo hilo Joyce hakumbuki ni lini alilala kwa zaidi ya saa nane kwa sababu kila siku ana jukumu la kupanga foleni kwa zaidi ya saa tano ili kupata angalau dumu nne kwa ajili ya  matumizi ya familia yake yenye watu sita.

Maumivu haya si kwa wanawake tu, yanajitokeza pia kwa Alledy Kanyasuka (60), mkazi wa Visele A, umbali wa kilomita tatu kutoka anapooishi Joyce ambaye hulazimika kukesha usiku kucha kuyasubiri maji ambayo ratiba yake bado haijulikani.

“Maji ni uhai wa mtu. Tunaumia kweli,” anasema Alledy ambaye katika kijiji chake, maji yanapatikana mara moja tu kwa wiki, mara nyingi hutoka kati ya saa tano, saa sita, au saa mbili usiku na yakitoka kila mtu anapaswa kuchota madumu manne tu.

Kwa wakazi ambao wanashindwa kukesha au kuamka usiku wa manane kupanga foleni ya maji hulazimika kununua dumu moja la lita 20 kwa Sh500 mara 25 zaidi ya bei wanayonunua maji katika mabomba ya kawaida.

Abineli James mkazi wa Mazae A mwenye familia ya watu zaidi ya 20 anasema hutumia Sh4,500 kwa siku kununua madumu tisa ya maji yanayosafirishwa kwa guta kutoka umbali wa kilomita tano hadi sita kutoka yanapootoka maji hayo hadi nyumbani kwake.

Kwa kiwango hicho, Abineli hutumia zaidi ya Sh135,000 kwa mwezi kwa ajili ya maji pekee suala linaoweza kuacha maumivu.

Hali hii inajitokeza wakati Serikali ikiendelea kupanua huduma ya maji nchini, ikilenga kufikia asilimia 90 ya upatikanaji wa maji vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2030.

Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Mei, 2026, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alisema hadi Desemba 2025, upatikanaji wa maji vijijini ulifikia wastani wa asilimia 85.2, kutoka asilimia 83.1 mwaka 2024.

Kwa mujibu wa Aweso, ongezeko hilo limetokana na kukamilika kwa miradi 54 yenye vituo 946 vya kuchotea maji, iliyowanufaisha wananchi 493,932 katika vijiji 151, na kufanya jumla ya wananchi wa vijijini wanaopata huduma ya maji kufikia zaidi ya milioni 38.6.

Maji yapo, lakini hayakidhi haja

Licha ya jitihada hizo zinazofanywa na Serikali za kuhakikisha kuwa huduma ya maji inamfikia kila mtu, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 inabainisha kuwa Mpwapwa WSSA ilirekodi upotevu wa maji wa mita za ujazo 153,878, wenye thamani ya zaidi ya Sh230 milioni.

Tatizo hili pia lilijitokeza katika ripoti ya CAG ya mwaka 2023/24 ambapo upungufu wa maji kwa wateja ulikuwa lita 503,481 kutoka mahitaji yaliyohitajika ya lita1,265,965. 

Takwimu hizi za CAG zinashabiana na ripoti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ya utendaji wa mamlaka za maji kwa mwaka wa fedha 2023/24 inayoonyesha kuwa, kwa wastani, uzalishaji wa maji ulifikia asilimia 45 tu ya mahitaji katika maeneo yanayohudumiwa na mamlaka hizo. 

Upotevu huo wa maji umewafanya wakazi hao 403,247 wa Wilaya ya Mpwapwa kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kugeukia vyanzo vingine vya maji ikiwemo visima.

Alledy Kanyasuka (60), mkazi wa Visele A, yeye na familia yake hulazimika kukesha kusubili mke wake mara tu maji yanapokuwa yametoka. Picha| Fatuma Hussein.

Kutokana na asili ya eneo la Mpwapwa kuwa na ukame wa wastani hata maji yake ni ya chumvi yenye kiwango kikubwa cha madini ya sodiamu ambayo bado hayakidhi mahitaji ya wakazi wa eneo hilo.

“Maji yanahitajika sana, hasa maji baridi. Maji ya chumvi hayafai hata kupikia mboga wala ugali. 

Ukipika ugali kwa maji ya chumvi hauivi vizuri. Hata ukiyatumia kupikia maharage au kuoshea mboga za majani, matokeo yake si mazuri kama unapotumia maji baridi,” anasema Elisia James mkazi wa Mazae A.

Mbali na kunywa, matumizi ya maji yenye chumvi nyingi katika kuandaa chakula yanaweza kuongeza kiwango cha sodiamu kinachopatikana katika lishe. 

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ulaji wa sodiamu kupita kiasi ni miongoni mwa vihatarishi vya kuongezeka kwa shinikizo la damu na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, hali iliyohusishwa na takribani vifo milioni 1.7 duniani mwaka 2023.

Nchini Tanzania, Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na. 11 ya mwaka 2009, Serikali kupitia Bodi za Maji za Mabonde ina wajibu wa kusimamia na kudhibiti matumizi ya maji ya chini ya ardhi, ikiwemo maji yanayopatikana kwenye visima. 

Pamoja na mambo mengine Sheria hiyo ina wajibu wa ikusimamia ubora wa maji hayo ili kulinda afya za watumiaji kutokana na madhara ya kiafya.

Wananchi wa mtaa wa Hazina na Kota wilayani Mpwapwa wakichota maji katika mabomba ya kijiji saa 12 asubuhi. Picha| Fatuma Hussein.

Kwa sasa hoja si tena mapambano ya wananchi ya kutafuta huduma hiyo muhimu kwa maisha, bali ni kujiuliza nini kilisababisha upotevu wa zaidi ya Sh230 milioni Mamlaka ya Maji Mpwapwa, kama ilivyobainika katika ripoti (CAG)? 

Kwanini maji yanapotea?

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri anaeleza kuwa katika sekta ya maji, upotevu unaweza kumaanisha maji yaliyotumika lakini hayakuonekana kwenye mfumo wa malipo jambo linalosababishwa  na baadhi ya watu kutumia maji kinyume na sheria, taratibu na kanuni. 

Mhandisi huyo ametolea mfano baadhi ya vitendo ikiwemo kuchepusha maji au uharibifu wa miundombinu kuwa miongoni mwa sababu za upotevu huo

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph amezitaja sababu nyingine za upotevu wa maji kuwa ni uchakavu wa miundombinu, uchakavu wa mita, dira, kutokuwa na upimaji mzuri wa maji yanayoingia kwenye mtandao ili yaweze kusambazwa, pamoja na wizi wa maji. 

“Watu wengi wanachepusha maji baada ya kuyalipia ‘wanabypass’ mita (wanatumia maji bila kuyalipia),” ameeleza Mhandisi.

Baada ya ripoti mbili mfululizo za CAG kubaini upotevu wa maji katika mamlaka hiyo, Mkurugenzi wa zamani Peter James Kabelwa aliong’olewa kwenye nafasi hiyo Aprili 28, 2026 na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso. 

Kwa sasa juhudi zimeelekezwa katika kubadili mabomba yanayovuja, mita na kutathmini matumizi ya wateja kwa kugeukia matumizi ya mita janja na huduma ya malipo ya kabla (‘prepaid meters’) ambazo zinaweza kupunguza upotevu wa maji kutoka asilimia 48 mwezi Juni hadi asilimia 38 mwezi Agosti,2026.

Mamlaka kushindwa kujiendesha

Athari za tatizo hilo hazibaki kwenye takwimu za ukaguzi, Mhandisi Joseph anasema mamlaka za maji zinategemea mapato kutoka kwa huduma ili kugharamia uendeshaji, ikiwemo umeme, mishahara, dawa za kutibu maji, mafuta na matengenezo ya miundombinu. 

Hivyo, maji yasiyolipiwa yanapunguza fedha zinazopatikana kwa ajili ya kuendesha mfumo mzima.

Kabla ya mabadiliko ya usimamizi Mhandisi Joseph,  anaeleza kuwa mamlaka ilikuwa ikikusanya hadi Sh28 milioni kwa mwezi, lakini baada ya mabadiliko mapato yaliongezeka hadi zaidi ya Sh50 milioni, huku mishahara ikianza kulipwa na deni la umeme kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupungua. 

Kwa mtazamo huo, upotevu wa maji si suala la kihasibu pekee. Ni suala linaloweza kuamua kama mamlaka inaweza kununua mita mpya, kukarabati bomba au kupeleka maji kwenye maeneo ambayo hayapati huduma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
1 Oct, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
1 Oct, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Serikali kufunga mfano wa ‘VAR’ barabarani, ikiandaa msamaha wa leseni za madereva

Serikali kufunga mfano wa ‘VAR’ barabarani, ikiandaa msamaha wa leseni za madereva

Nukta TV

DC Msando kulivalia njuga suala la posho za madereva wa mabasi

DC Msando kulivalia njuga suala la posho za madereva wa mabasi

Nukta TV

Katambi aomba dereva aliyekamatwa kwa kuchochea mgomo aachiwe

Katambi aomba dereva aliyekamatwa kwa kuchochea mgomo aachiwe

Nukta TV