Ufahamu mwenendo wa ufaulu matokeo kidato cha nne kwa miaka mitano Tanzania
- Ufaulu wapanda na kushuka ndani ya miaka mitano.
- Mwaka 2022 ufaulu washuka zaidi ya miaka mingine.
- Waliopata sifuri wapungua mdogo mdogo.
Dar es Salaam. Januari 25, 2024 Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) lilitangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha nne iliyofanyika Novemba 13 hadi 30, 2023, ambapo ufaulu umeongezeka kiduchu kwa asilimia 0.87.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Said Mohamed aliyekuwa akitangaza matokeo hayo, jumla ya watahiniwa 484,823 kati ya wanafunzi 572,359 waliosajiliwa kufanya mtihani huo wamefaulu na kupaisha chati ya ufaulu nchini hadi kufikia asilimia 87.65.
Kati ya watahiniwa hao, wavulana wamefaulu zaidi kwa asilimia 89.4 kulinganisha na ufaulu wa wasichana wa asilmia 84.4.
Licha ya idadi hiyo ya waliofaulu zaidi ya nusu ya watahiniwa sawa na asilimia 51.9 wamepata daraja la nne na asilimia 10.6 wamepata sifuri.
Wakati watahiniwa hao wakishika mkia wenzao 42,448 sawa na asilimia 8 wamepata daraja la kwanza, 71,255 wamepata daraja la pili na 83,723 wamepata daraja la tatu.
Miongoni mwa masomo yaliyowapasua vichwa watahiniwa hao kwa mwaka 2023 ni pamoja na hesabu, Kiarabu, Jografia na kiingereza huku masomo kama Kiswahili, Kemia, Kichina na Tehama yakiwapa matumaini baadhi ya wanafunzi kuendelea na ngazi za juu za elimu.
Uchambuzi zaidi wa matokeo hayo kwa miaka mitano iliyopita uliofanywa na Nukta Habari umebaini kupanda na kushuka kwa ufaulu wa jumla wa wanafunzi huku idadi ya wanafunzi ikiongezeka hali inayotoa taswira chanya katika sekta ya elimu nchini.
Soma zaidi:Udanganyifu, matusi vyawaponza watahiniwa 107 wa kidato cha nne 2023
Mwaka 2022 ufaulu wapungua zaidi
Mwaka 2022 jumla ya wanafunzi 456,975 walifaulu mitihani hiyo kwa daraja la kwanza hadi la nne kati ya wanafunzi 520,558 waliofanya mitihani na kufanya ufaulu kupungua kwa asilimia 0.52 kulinganisha na mwaka 2021.
Licha ya ufaulu huo kupungua, bado watahiniwa waliopata daraja la kwanza hadi la tatu walikuwa wachache wasiozidi hata nusu ya watahiniwa wote waliofanya mtihani huo Oktoba mwaka 2021.
Huu ndio mwaka pekee ambapo ufaulu wa jumla wa kidato cha nne umeshuka ndani ya kipindi cha miaka mitano ambapo uchambuzi huu ulifanyika.
Wakati huo huo watahiwa waliopata daraja la nne katika mitihani hiyo walikuwa 264,627 sawa na asilimia 50.8 ya watahiniwa wote waliofanya mitihani hiyo.
Soma zaidi:Udanganyifu, matusi vyawaponza watahiniwa 107 wa kidato cha nne 2023
Kwa upande wa mwaka 2021 ufaulu wa jumla ulifikia asilimia 87.3 ambapo watahiniwa 422,388 walifaulu ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 1.46 ikilinganishwa na mwaka wa 2020.
Licha ya kuongezeka kwa ufaulu, kiwango cha ubora wa ufaulu kiliongezeka kwa asilimia 0.74 tu kikitoka asilimia 34.27 hadi 35.1.
Hiyo inamaanisha katika kila wanafunzi 100 ni wanafunzi watatu tu waliopata daraja la kwanza hadi la tatu katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2021.
Jumla ya wanafunzi 269,479 sawa na asilimia 55.6 walipata daraja la nne huku wanafunzi 61,432 sawa na asilimia 12 wakipata daraja sifuri.
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Said Mohamed akitangaza matokeo ya kidato cha nne mwaka2023 mbele ya wanahabari Januari 25, 2024.Picha|Lucy Samson.
Mwaka 2020 ulikuwa wa neema kwa wanafunzi 373,958 waliofanya vizuri katika matokeo ya kidato cha nne wakifanya ufaulu kuongezeka hadi asilimia 85.8.
Hii ni sawa na kusema kuwa takriban wanafunzi 15 kati ya 100 waliofanya mtihani huo walipata daraja sifuri wakiwa watano sawa na asilimia 50.8
Ufaulu wa mwaka 2019 uliongezeka kwa asilimia 5.1 ikiwa ni ufaulu wa juu zaidi kuwahi kurekodiwa ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Kwa upande wa mwaka 2019 watahiniwa 340,914 walifaulu kwa asilimia 80.65 na kuwawezesha kuendelea na hatua nyingine za kimasomo.
Ufaulu huo uliongezeka kidogo kwa asilimia 1.4 kutoka ule wa mwaka 2018.
Licha ya ufaulu huo kuongezeka, bado takriban nusu ama asilimia 48.6 ya watahiniwa wote wa mwaka 2019 walipata daraja la nne.
Latest



