Ufahamu mfumo mpya wa kidijitali wa ununuzi wa pamba Tanzania

February 24, 2023 7:19 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Utarahisisha shughuli ya ununuzi wa pamba nchini.
  • Wakaulima hawataibia pamba kwa sababu manunuzi yatafanyika kwa uwazi. 

Mwanza. Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kwa kushirikisha na Bodi ya Stakabadhi za Ghala (WRRB) na Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) imetambulisha mfumo mpya wa ununuaji wa pamba kidijitali kwa wanunuzi wa pamba.

Pia utawezesha matumizi ya mizani ya kidijitali ili kuhakikisha wakulima hawadhurumiwi haki zao.

Mfumo huo utaenda sambamba na kusajili wakulima wa pamba kwa njia ya kidijitali na kwamba utamsaidia mkulima katika shughuli zote za kilimo ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa pembejeo za kilimo, mavuno na wakati wa uuzaji wa mazao yake.

Mkuu wa Usimamizi Stakabidhi za ghala wa WRRB, Sangye Bangu akizungumza kwenye kikao kilichokutanisha pamoja wanunuzi wa pamba na wadau wengine wa zao hilo jijini Mwanza Februari 23, 2023 amesema walikaa pamoja ili kuja na suluhisho litakalohakikisha linamlinda mkulima ili aweze kupata thawabu ya jasho lake.

“Mfumo utaondoa longolongo, mkulima ataweze kuuza mazao yake kwa haraka, atapata takwimu halisi lakini pia wadau wote watapata taarifa kwa usahihi,” amesema Bangu.

Amesema mfumo utatumika kwa kuanza kusajili wakulima wa pamba kwa njia ya kidijitali ambapo utamsaidia mkulima katika shughuli zote za kilimo.

Akizungumzia mfumo huo, Meneja Mifumo na Teknolojia kutoka kampuni ya Rutai, Fakii Shaibu amesema mizani ya kidigitali itamsaidia mkulima kuondokana na udanganyifu wa wanunuzi kuminya haki ya wakulima katika vipimo.

“Badala yake sasa mkulima ataweza kung’amua uzito wa mzigo wake kwa uwazi na kupatiwa risiti yenye vielelezo vyote, ikiwemo uzito wa pamba na thamani halisi,” amesema Shaibu.

Amesema mizani hiyo ya kidigitali itatolewa kwa Vyama vya Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS), ambao ndio wasimamizi wa masoko, ili mkulima aweze kupata kipimo na malipo sahihi.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amepongeza mfumo huo na kueleza kuwa utakuwa mkombozi kwa mkulima.

“Mfumo huu ungekuwepo toka zamani ungeongeza tija kwenye zao la pamba na kumsaidia mkulima kupata thamani halisi ya zao hilo,” amesema Malima

Mkuu huyo wa mkoa pia ametumia fursa hiyo kuwataka wadau hao kujadili kwa kina mstakabali wa bei ya pamba ambayo haitamuumiza mkulima na mnunuaji.

Amewataka kuweka pembeni masuala ya siasa kwenye biashara ili kusaidia zao hilo ambalo ni muhimu liweze kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

“Hatuwezi kuwa na rekodi ndogo kwenye kilimo cha pamba wakati Tanzania ina sehemu kubwa ya kilimo hicho, kwanini tuzidiwe uzalishaji na mataifa ya nje ya Brazil lazima tuweke siasa pembeni tujadili mambo ya msingi yatakayomsaidia mkulima na zao la pamba liweze kushindana kwenye soko la dunia,” amesema Malima.

Enable Notifications OK No thanks