Ufahamu bipolar: Ugonjwa wa hisia zinazobadilika

August 13, 2026 11:03 am · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ugonjwa huu unaweza kumpata mtu yoyote bila kubagua jinsia.
  • Waathirika wakubwa ni takribani vijana milioni 3.8 wenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 19.

Dar es Salaam. Hebu vuta picha, unazungumza na mtu kwa muda fulani mkipiga stori na kupanga mipango yenu vizuri tu lakini dakika chache baadae anabadilika na kuonesha tabia tofauti ambayo haikuwepo wakati mnaanza maongezi.

Labda anaonesha hasira kali isiyo na sababu ambayo haihusiani kabisa na mazungumzo yenu, furaha iliyopitiliza au huzuni nzito isiyoweza kujificha.

Kwa kawaida ni lazima utahamaki, lakini hiyo ni hali ya kawaida ambayo huwakumba watu wenye ugonjwa wa hisia zinazobadilika (bipolar).

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ‘bipolar’ ‘au baipola kwa Kiswahili ni hali ya afya ya akili inayoathiri hisia, nguvu, shughuli na fikra za mtu. 

‘Bipolar’ husababishwa na nini?

Ugonjwa huu husababisha uwepo wa vipindi vinavyobadilika kati ya hali ya juu sana ya furaha au msisimko (manic au hypomanic) na hali ya huzuni au mkazo (depressive episodes) ikiathiri watu zaidi ya milioni 37 duniani kote.

“Mwaka 2021 watu milioni 37 sawa na asilimia 0.5 ya idadi ya watu duniani, wakiwemo takribani watu wazima milioni 34, waliishi na ugonjwa huu,” inasema WHO.

Hii ni sawa na kusema kuwa mtu mmoja kati ya 200 duniani anaishi na ugonjwa wa bipolar . 

Jambo la kusikitisha ni kwamba waathirika hai wanaweza kufariki mapema kwa wastani wa miaka 10 ikilinganishwa na watu wengine, huku wakiwa katika hatari kubwa ya kujiua iwapo hawatapata msaada wa haraka.

Mtu mwenye changamoto hii, anaweza kuonekana mwenye mafanikio makubwa huku akiamini kila analofanya ndio sahihi na atakai ushauri lakini kiafya hali hii si ya kawaida. Picha |Canva.

Dk Theresia Royce Mwanjala, mtaalamu wa saikolojia tiba kutoka Hospitali ya Saifee jijini Dar es Salaam anasema kinachoutofautisha ugonjwa huu na changamoto nyingine za afya ya akili ni kufanya kazi kwa kipindi kirefu bila kuonyesha dalili za uchovu.

“Wagonjwa wa bipolar wanakuwa na energy (nguvu) iliyopitiliza, anapata saa chache za kupumzika lakini akiamka ana nguvu kama vile amelala usingizi wa kutosha.  ‘Energy level’ (kiwango cha nguvu) inakuwa kubwa sana,” anaeleza Dk Mwanjala.

Katika kipindi hiki, mgonjwa huonekana mwenye uwezo wa ajabu ikiwemo kufanya kazi kwa saa nyingi bila kuchoka, kulala kwa muda mfupi lakini anaendelea kuwa na nguvu kuliko kawaida, kuwa na mawazo mengi, kujiamini kupita kiasi pamoja na kufanya maamuzi hatarishi bila kufikiria matokeo.

Kuzidi kwa hali hii, humfanya mgonjwa kuangukia katika unyogofu ambapo anaanza kujilaumu, kujitenga, kujiona hana thamani, na hata kulala au kula kupitiliza.

Katika hali ya kawaida mtu mwenye changamoto hii, anaweza kuonekana mwenye mafanikio makubwa lakini kiafya hali hii si ya kawaida.

Aina za ugonjwa wa ‘bipolar’ 

Kuna aina kuu mbili za ugonjwa wa ‘bipolar’, WHO, inaeleza, kulingana na muundo wa vipindi vya mania/kichaa, hypomania na unyogovu.

Watu wenye bipolar aina ya kwanza hupata kipindi kimoja au zaidi cha mania (msisimko uliopitiliza), ambacho huambatana au kufuatiwa na vipindi vya unyogovu (depressive).

Mara nyingi mtu mwenye changamoto hii ya afya ya akili hujikuta akifanya kazi nyingi bila kuchoka ingawa hali hii haiwezi kufanana kwa watu wote wanaokutwa na ‘bipolar’. Picha| Gemin ai| Fatuma Hussein.

Kwa wenye aina ya pili ya bipolar hupata angalau kipindi kimoja au zaidi cha hypomania pamoja na angalau kipindi kimoja cha unyogovu, lakini hawajawahi kuwa na historia ya vipindi kamili vya mania.

Kwa mujibu wa tovuti ya National Institute of Mental Health (NIH), kuna aina ya tatu ya ugonjwa huu inayojulikana kama Cyclothymic disorder (cyclothymia). 

Aina hii hufafanuliwa kuwa ni hali ya mtu kuwa na dalili zinazojirudia za hypomania na unyogofu, ambazo si kali vya kutosha au hazidumu kwa muda wa kutosha kuweza kuainishwa rasmi kama vipindi kamili vya hypomania au unyogovu.

Dalili za bipolar  kwa undani

Kwa mujibu wa Dk Mwanjala dalili za ugonjwa wa ‘bipolar’  hutofautiana kati ya mtu na mtu bila kujali jinsia au rika na huihitaji zaidi tathmini ya kitaalamu ili kubaini na kuzitambua dalili za awali.

Mtu mwenye ugonjwa huu anaweza kupitia vipindi vya mania, unyogovu au vipindi mchanganyiko huku kipindi mchanganyiko hujumuisha dalili za mania na unyogovu kwa wakati mmoja.

Shirika la Embrace Mental health linabainisha kuwa dalili za vipindi vya unyogovu zinajumuisha kuhisi huzuni, kukosa tumaini au kukasirika mara nyingi, kukosa nguvu, hamu ya kula, hamu ya kufanya shughuli za kila siku, ugumu wa kuzingatia au kukumbuka mambo.

‘Bipolar inaweza kumfanya mtu ashindwe kuwa na uamuzi sahihi juu ya jambo analotaka kulifanya

Katika baadhi ya mazingira ugonjwa huo husababisha hisia za hali ya juu hali inayoweza kumfanya mgonjwa kufanya tendo la ndoa mara nyingi zaidi na kwa muda mrefu.

Uelewa ‘bipolar’ bado kiduchu

Licha ya ukubwa wa tatizo, jamii nyingi bado hazielewi ugonjwa huu. Wagonjwa mara nyingi hutafsiriwa vibaya kama watu wasio na nidhamu, wenye hasira au wasioweza kujidhibiti.

Mkazi wa jijini Dar es Salaam Juma Ally haamini na wala hajawahi kusikia kuhusu uwepo wa aina hiyo ya ugonjwa huo wa bipolar .

“Hakuna ugonjwa wa hisia, na sijawahi kuusikia. Kila binadamu ana hisia, sasa inawezekanaje hisia zikawa ugonjwa?” anaeleza Juma, anayejishughulisha na ufundi Seremala eneo la Kimara.

Wengi wanasema wanasikia juu juu tu kuhusu maradhi haya ya afya ya akili, jambo linaloongeza changamoto katika kuwasaidia wagonjwa. 

“Nafahamu kuhusu bipolar  lakini naona ni kama mtu mwenye kisukari kikali. Leo anaweza kucheka, kesho akawa na huzuni ni kama anabadilika kihisia,” anaeleza Naomi Chris, mkazi wa Kinondoni, akifananisha hali hiyo na ugonjwa wa kisukari.

Bipolar’ husababishwa na nini?

Dk Mwanjala anaeleza kuwa, hakuna sababu ya moja kwa moja ya ugonjwa wa bipolar , lakini mara kadhaa huwa unahusianishwa na historia ya vinasaba vya ugonjwa huo katika familia.

Tovuti ya masuala ya afya ya Mayo Clinic inabainisha kuwa karibu asilimia 80 ya wagonjwa wa bipolar  huirithi kutoka kwa baba au kwa mama na huweza kuonekana zaidi baada ya kupitia matukio ya mshtuko wa kihisia (trauma) au changamoto nyingine za maisha.

Kila mtu anaweza kuwa na changamoto ya ‘bipolar’ kwa njia moja au nyingine hivyo ni vyema ukiona dalili zozote kwenye mwili wako ambazo unazitilia mashaka kutafuta msaada wa kitabibu mapema. Picha| Canva.

Mbali na sababu hizo, tovuti hiyo imebainisha kuwa mtindo mbaya wa maisha unaweza kuwa chanzo kingine kikubwa cha ugonjwa huo ukihusisha matumizi ya dawa za kulevya, unywaji pombe kupitiliza, mabadiliko makubwa ya maisha, kukosa usingizi, na kuishi katika mazingira yenye vurugu kwa muda mrefu.

Je, unatibika?

Daktari bingwa wa magonjwa ya afya ya akili, Silvia Ngonyani wa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe jijini Dar es Salaam anabainisha kuwa magonjwa ya afya ya akili hayana muda maalum wa kusema mtu amepona kabisa kwani kila mgonjwa hutibiwa kulingana na ukubwa wa tatizo lake.

Hata katika ugonjwa wa bipolar Dk Mwanjala anabainisha kuwa hauwezi kuisha kabisa, lakini unaweza kudhibitiwa.

“Tunasema mgonjwa wa bipolar haponi isipokuwa kupitia sessions angalau kuanzia 20 na kuendelea…dawa husaidia kumuweka sawa na kumsaidia kujitambua,” anasema Dk Mwanjala. 

Hivyo, kupitia elimu ya kisaikolojia, kupunguza msongo wa mawazo, na kuimarisha mahusiano ya kijamii, mgonjwa anaweza kurudi katika hali ya kawaida na kuendelea na majukumu yake ya kila siku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
14 Aug, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
14 Aug, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
14 Aug, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia awataka wananchi wa Kizimkazi kutunza miundombinu ya maji

Rais Samia awataka wananchi wa Kizimkazi kutunza miundombinu ya maji

Nukta TV

Ni changamoto gani zinawakabili vijana wa kitanzania kwa sasa ?

Ni changamoto gani zinawakabili vijana wa kitanzania kwa sasa ?

Nukta TV

Akili Unde (AI) ni suluhu ya habari za uzushi ?

Akili Unde (AI) ni suluhu ya habari za uzushi ?

Nukta TV