Twitter yaja na mbinu mpya kulinda meseji za watumiaji wake

May 12, 2023 5:56 am · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Yazindua kipengele kipya cha meseji kutokuonekana na mtu wa tatu.
  • Kitasaidia kulinda faragha za watumiaji na uhuru wa kutoa maoni. 

Dar es Salaam. Twitter umekuwa mtandao wa kwanza wa kijamii kuanzisha huduma ya meseji zilizosimbwa (encrypted messaging service). 

Meseji zinazotumwa Twitter zitasimbwa, hii ikiwa na maana kuwa meseji binafsi (DM) zitakuwa zinaonwa na mtumaji na mpokeaji bila mtu wa tatu.

DM zilizosimbwa zitatoa safu ya ziada ya usalama kwenye jukwa la ujumbe binafsi, kulinda mazungumzo ya faragha ya watumiaji dhidi ya watu wasiohusika. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Twitter, Elon Musk amesema hiyo inamaanisha kuwa hata yeye hawezi kuona mazungumzo ya watu kwenye meseji hizo.

Hata hivyo, ametahadharisha kuwa mabadiliko hayo ni ya mwanzo tu na “watu wanaweza kufanya majaribio lakini wasiamini kwanza.”

Kipengele hicho muhimu kwa sasa hakitumiki na watumiaji wote bali wenye tiki ya blue au wenye uhusiano na akaunti za Twitter ambazo zimethibitishwa. Pia kwa sasa huwezi kutuma picha kwenye meseji, ni maandishi tu.

Changamoto nyingine ya kipengele hicho ni kuwa inahusu mazungumzo ya watu wawili na siyo ya kikundi cha watu. 

Pia watumiaji hawataweza kutuma ujumbe uliosimbwa kwa watu ambao hawatumii toleo jipya zaidi la programu ya Twitter.

Zaidi ya hayo, kipengele hicho kitapatikana kwenye vifaa vya mkononi pekee na si kwenye jukwaa la wavuti la Twitter. 

Licha ya changamoto hizo, Twitter kuchukua hatua hiyo ni kielelezo kuwa inawajali watumiaji wake, inahimiza haki faragha pamoja na uhuru wa kutoa maoni.

Twitter katika siku za hivi karibuni imekuwa ikikabiliwa na ukosoaji kwa jinsi inavyoshughulikia data ya watumiaji na masuala ya faragha, na kipengele kipya kinalenga kushughulikia baadhi ya masuala haya. 

Katika taarifa yake, Makamu wa Rais wa Bidhaa wa Twitter, Kayvon Beykpour, amesema, “Tumekuwa tukifanya kazi hii kwa muda mrefu, na tunafurahi hatimaye kuisambaza kwa watumiaji wetu wote. Tunaamini kwamba kila mtu anapaswa kuwa na haki ya kuwasiliana kwa faragha, na tumejitolea kuwapa watumiaji wetu zana wanazohitaji kufanya hivyo.”

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...