Twitter yabadili jina, ‘logo’ baada ya miaka 17, watumiaji wavurugwa
- Sasa kutumia nembo X badala ya njiwa wa bluu.
- Mabadiliko zaidi kutegemewa kwa siku za usoni.
Dar es Salaam. Miaka 17 baada ya kuanzishwa kwa Twitter, kampuni ya teknolojia ya Marekani ya X Corp imebadili nembo (logo) ya njiwa mwenye rangi ya bluu na sasa mtandao huo maarufu duniani utakuwa na nembo yenye herufi X.
Julai 23, 2023 mmiliki wa mtandao huo bilionea Elon Musk alieleza kwenye ukurasa wake kuwa anatarajia kuutangaza upya mtandao wa Twitter kupitia herufi X.
Ndani ya muda mfupi baada tangazo hilo aliwaambia wafuasi wake kuwa logo yeyote nzuri ambayo ingepostiwa kwa ajili ya X ingeweza kutumiwa na mtandao huo ulionunuliwa na Musk Oktoba 2022 kutoka kwa Twitter Inc kwa Dola za Marekani Bilioni 44 sawa na Sh107.8 trilioni.
Tayari nembo mpya iliyoshinda kutoka kwa mtumiaji wa Twitter ajulikanae kwa jina la Sawyer Merritt imeshaanza kuonekana kwa watumiaji wenye kompyuta za mezani au mpakato. Merritt anasema logo awali ilitengenezwa na Mhandisi wa Fikizi anayejulikana Twitter kwa jina @ajtourville.
Hatua ya kubadilisha logo ni miongoni mwa dazeni ya mabadiliko ambayo Musk anatarajia kuyafanyakwa kuwa bilionea huyo amesema nembo ya sasa ya X itatumika kwa muda mfupi tu.
Tangu Musk aununue mtandao huo kutoka kwa mwanzilishi wake Jack Dorsey, amefanya mabadiliko kadhaa ambayo yamepokelewa kwa hisia tofauti na watumiaji wa mtandao huo ikiwemo kuweka ukomo wa idadi ya Twiti wanaoweza kusoma watumiaji kwa siku.
Miongoni mwa mabadiliko yaliyogusa hisia za wengi ni kuweka utaratibu wa kulipia kila mwezi ili kupata beji ya uthibitisho (Verification) wa akaunti yako kwenye ukurasa huo.
Watumiaji wanena
Ommy Fitness ambaye ni mwalimu wa mazoezi ya mwili na mtumiaji wa mtandao wa Twitter ameiambia Nukta Habari kuwa hawajaridhishwa na mabadiliko hayo kwa kuwa hakukuwa na sababu ya kubadilisha logo mpya ambayo nayo itakwenda kubadilishwa baadae.
“Twitter ni kwa ajili ya “tweets” (twiti), sasa X ni kwa ajili ya nini? Sijaelewa kwanini amebadilisha, hakukuwa na haja ya kubadilisha na kama ilikuwa lazima angeanza kutoa ufafanuzi kwanza hii logo mpya ni kwa ajili ya nini,” amesema.
Hata hivyo, kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya habari kwa njia ya mtandao ya Msasa, Godson Mbilinyi amebainisha kuwa kubadili logo ni jambo la kawaida kwenye kampuni yoyote hasa inapopitia mabadiliko makubwa ya umiliki au kiuendeshaji na huwa na faida na hasara.
Mbilinyi amesisitiza kuwa licha ya kwamba itawachukua muda watumiaji kuzoea mabadiliko hayo, Musk amefaidika kwa kuwa sasa itakuwa rahisi kutangaza bidhaa zake nyingine kutokana na watu wengi kufuatilia kwa karibu jukwaa hilo kuona nini kitajiri.
Mabadiliko zaidi
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni X Corp, Linda Yaccarino Twitter ilibadili namna watu wanavyozungumza wao kwa wao, X itaenda mbali zaidi na kuufanya mtandao huo kuwa soko la kimataifa la mawazo, bidhaa, huduma na fursa.
Mapema mwezi Julai, Musk alitangaza kuanza kuwalipa wachapishaji wa maudhui kwenye mtandao huo ambapo baadhi yao hususan waliopo nchi za Marekani na Ulaya walithibitisha kupokea malipo yatokanayo na matangazo yaliyowekwa kwenye maudhui yao.
Siri nyuma ya herufi X
Herufi X imekuwa nyuma ya bidhaa nyingi za bilionea huyu namba mbili kwa ukwasi ulimwenguni ikiwemo kampuni yake inayoshughulika na utengenezaji wa roketi za anga za juu pamoja na teknolojia bandia inayoitwa X.ai.
Mwaka 1997 alianzisha mtandao wa kutuma na kupokea fedha kidijitali ulioitwa X.com ambao kwa sasa unatambulika kama Paypal.
Itakumbukwa mara tu baada ya kuununua mtandao huo alibadili jina la kampuni inayouendesha kutoka Twitter Inc. kwenda X Corp, mwanzoni mwa mwaka huu.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006, Twitter imebadili logo yake mara tano, ambapo iliyodumu zaidi ni ile iliyotengenezwa mwaka 2012 iliyofahamika kama Larry the Bird.
Latest