Ni mvutano: Bilionea Musk akikataa kununua Twitter
- Twitter yampeleka mahakamani kumlazimisha anunue.
- Mawakili wa Musk wataka kesi isogezwe hadi mwakani.
Dar es salaam. Mtandao wa Twitter umemshtaki Elon Musk kumshurutisha kununua kampuni hiyo ya mtandao wa kijamii kwa dola bilioni 44 (Sh102.5 trilioni), mkataba ambao bilionea huyo alisema ataachana nao.
Kesi hiyo iliyowasilishwa katika Mahakama ya Delaware ya nchini Marekani Julai 12, 2022. Twitter inamtuhumu Musk kwa unafiki na imani mbaya katika kukiuka mkataba wake wa ununuzi.
Inadai kuwa Musk alitumia visingizio, ikiwa ni pamoja na swali kuhusu ni akaunti ngapi feki ziko kwenye jukwaa hilo, kama njia ya kujaribu kuachana na ununuzi wa mtandao huo baada ya hisa za kampuni za bilionea huyo kushuka.
Hata hivyo, kesi hiyo inaeleza, alikuwa chini ya mkataba unaomlazimisha kisheria.
“Musk alitaka kutoroka. Lakini makubaliano ya muungano yalimuachia nafasi ndogo,” aliandika wakili William Savitt na mawakili wengine wanaowakilisha kampuni hiyo ya mitandao ya kijamii.
Wiki iliyopita chombo cha habari cha Bloomberg kiliripoti kuwa mawakili wa Musk waliiwekea pingamizi ombi la Twitter la kutaka kesi hiyo isikilizwe kwa siku nne kuanzia Julai 19 mwaka 2022 badala yake ipelekwe Februari 23 mwakani au mbele zaidi.
Mawakili hao walidai kuwa “kuanza kwa kesi hiyo mwakani bado ni mapema zaidi kwa kesi kubwa kama hiyo.”
Zinazohusiana:
Chanzo cha mgogoro
Mnamo Aprili 25 2022 Bilionea Musk aliingia makubaliano ya kununua mtandao wa Twitter kwa Sh102.5 trilioni huku akiweka sharti la kupatiwa taarifa ya idadi ya watumiaji hai wa mtandao huo pamoja na akaunti zinazoendeshwa na roboti.
Bilionea huyo nambari moja duniani kwa ukwasi ambaye pia ni mmiliki wa kampuni za teknolojia za Tesla na SpaceX alisitisha mpango wa kununua mtandao wa Twitter baada ya kutopatiwa taarifa za akaunti ghushi alizokuwa anazihitaji.
Alidai kuwa chini ya asilimia 5 au zaidi ya watumiaji milioni 229 wa mtandao wa Twitter kila siku ni akaunti ghushi au feki.
Hata hivyo, Twitter walikanusha madai hayo na kueleza suala la idadi ya akaunti ghushi linaendelea kushughulikiwa.
Mtandao huo umedai kuporomoka kwa hisa za kampuni za Tesla na Space X ndiyo sababu ya bilionea huyo kusitisha dili hilo na kuitaka mahakama ya Delaware kushughulikia kesi hiyo kwa haraka ili kulinda kuporomoka kwa hisa za mtandao huo maarufu.
Katika kesi hiyo Twitter pia imemshutumu Musk kwa kukiuka sehemu ya makubaliano ya muungano ambayo yanamzuia kuchapisha maneno ya kashfa kwenye mtandao huo ikisema alimjibu Mkurugenzi Mtendaji wake Parag Agrawal kwa emoji ya kinyesi mwezi Mei.
Nini kitatokea?
Kwa mujibu wa Bloomberg, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Chancery Delaware Kathaleen McCormick amepanga kusikiliza ombi la Twitter la kuharakisha kesi hiyo Julai 19 mwaka huu.
Ikiwa Twitter watashinda kesi hiyo basi huenda mahakama ikamuamuru Bilionea Musk kununua mtandao huo kwa bei atakayopangiwa na mahakama na ikiwa Twitter watashindwa kesi basi huenda wakaamuliwa kulipa fidia ya kesi.
Latest
