Tume ya uchunguzi yatoa onyo wanaokwamisha ushahidi

December 27, 2025 2:56 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
  • Imesema ukwamishaji huo utazuia kupatikana kwa ukweli.
  • Yawataka wananchi kutoa maoni, ushauri na taarifa zitakazosaidia kutimiza majukumu yake kwa ufanisi.

Dar es Salaam. Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 imewataka wananchi kupuuza vishawishi vyovyote vinavyolenga kuwazuia kutoa ushirikiano kwa tume hiyo, ikieleza kuwa jitihada hizo zinahujumu juhudi za kitaifa za kutafuta ukweli na haki.

Taarifa ya tume hiyo iliyotolewa Desemba 26, 2025 imeeleza kuwa imebaini kuwepo kwa watu au makundi yanayowashawishi wananchi kutojihusisha na mchakato wa utoaji wa maoni, ushahidi au taarifa muhimu.

Tume imesisitiza kuwa ushawishi wa aina hiyo hausaidii mchakato wa kitaifa wa kuchambua matukio yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu, kujifunza kutokana na makosa ya nyuma na kuweka msingi wa suluhu ya kudumu kwa Taifa.

“Tume ya uchunguzi ipo kwa ajili ya Watanzania wote, na mafanikio ya kazi yake yanategemea ushiriki mpana, wa hiari na wenye uwazi wa wananchi. Amani, mshikamano na mustakabali salama wa Taifa letu ni jukumu la kila mmoja wetu,” imeeleza taarifa hiyo.

Tume hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mkuu Mstaafu Mohammed Chande Othman, imewataka wananchi kutoa ushirikiano wao kwa hiari, uwazi na bila woga, kwa kutoa maoni, ushauri na taarifa zitakazosaidia kutimiza majukumu yake kwa ufanisi.

Tume hiyo inaendelea na majukumu yake ya kukusanya maoni, ushahidi na taarifa kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kujenga demokrasia, haki na mshikamano wa kitaifa.

Rais Samia Suluhu aliunda tume hiyo yenye wajumbe nane Novemba 8, 2025 ili kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Tume hiyo itafanya kazi kwa kipindi cha miezi mitatu na ikichunguza mambo sita ikiwemo madhara yaliyojitokeza ikiwemo vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

Pia inachunguza madhara ya kiuchumi na kijamii, mazingira na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali na vyombo vyake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks