Mambo 6 yatakayochunguzwa vurugu za uchaguzi Oktoba 29

December 1, 2025 6:04 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na vifo na majeruhi yaliyotokea 
  • Chande aomba wananchi kushirikiana na Tume kwa kutoa taarifa za kweli na sahihi ili kuwezesha uchunguzi wa kina.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchunguzi, wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, Jaji Mkuu mstaafu Othman Chande, ameainisha maeneo sita yatakayopewa kipaumbele katika uchunguzi wa tume hiyo ikiwemo vifo. 

Akizungumza na wanahabari leo Disemba 1, 2025 jijini Dar es Salaam Chande amesema tume hiyo itachunguza maeneo hayo sita na mengineyo ambayo itaona ni muhimu. 

“Kuchunguza na kubainisha madhara yaliyojitokeza ikiwemo vifo majeruhi uharibifu wa mali na madhara ya kiuchumi na kijamii, kuchunguza mazingira na hatua mbalimbali zilizochukuiliwa na Serikali na vyombo vyake na Mtu yeyote mwingine…

…Kupendekeza maeneo yanayohitaji kuimarishwa zaidi ili kuongeza uwajibikaji wa viongozi na raia kwenye kulinda amani ya Tanzania, utawala bora, haki za binadamu, utawala wa sheria hadi kufikia maridhiano ya kitaifa,” amesema Chande akifafanua maeneo hayo sita yatakayochunguzwa.

Novemba 18 mwaka huu Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliunda tume hiyo yenye wajumbe nane kwa lengo la kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Tume hiyo iliundwa ikiwa ni siku tatu tangu Rais Samia atoe ahadi hiyo alipokuwa akihutubia Bunge kwa mara kwa kwanza katika awamu ya pili ya uongozi wake Novemba 14 mwaka huu.

 Ili kutimiza majukumu waliyotwishwa Chande ameomba ushirikiano wa wananchi na wadau wengine wanaoweza kuwa muhimu.

“Tunatoa wito kwa Watanzania, Wadau wote, tushirikiane ili Tume iweze kupata taarifa sahihi na nasisitiza ya ukweli ambayo itatuwezesha kufanikisha uchunguzi na hadidu za rejea” ameongeza Chande.

Tume hiyo unatarajiwa kufanya kazi katika mikoa na wilaya 14 zilizokumbwa na matukio ya vurugu nchini, ikiangalia pia wilaya ambazo hazikupata madhara kama sehemu ya kujifunza na kupata uzoefu tofauti. 

Aidha, Chande amebinisha kuwa tume hiyo itatumia mbinu mbalimbali za ukusanyaji taarifa ikiwemo mapitio ya uchambuzi, mahojiano, dodoso la mtandaoni na ujumbe mfupi kukamilisha uchunguzi wa matukio hayo yalioacha alama katika maisha ya Watanzania.

Mpaka sasa hakuna taarifa rasmi za idadi ya watu waliopoteza maisha katika vurugu hizo mbali na takwimu za awali za uharibifu wa miundombinu zilizotolewa na Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba hivi karibuni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks