TTCL kuachana na minara ya simu ya kukodi

May 22, 2019 12:25 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Itasaidia TTCL kuongeza wigo wa huduma na kumudu ushindani wa soko la mawasiliano nchini. Picha|Mtandao.


  • Hatua hiyo inakuja baada ya Rais Magufuli kuagiza  Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kuwekeza miundombinu ya minara ya simu kwa TTCL.
  • Itasaidia TTCL kuongeza wigo wa huduma na kumudu ushindani wa soko la mawasiliano nchini.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameutaka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kutoa kipaumbele katika uwekezaji wa miundombinu ya minara ya simu kwa kampuni ya simu Tanzania (TTCL) ili kuiimarisha na kuiwezesha kumudu ushindani katika soko la mawasiliano nchini.

Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza katika hafla ya upokeaji wa Gawio la Serikali la Sh2.1 bilioni kutoka TTCL jana (Mei 21, 2019) amesema  njia pekee ya kuiendeleza TTCL ni kwa viongozi wa Serikali kuwa na moyo wa uzalendo wa kusimamia rasilimali za umma ikiwemo kampuni hiyo.

Amebainisha kuwa TTCL imekuwa ikitumia kati ya Sh700 milioni hadi Sh800 milioni  kila mwezi kwa ajili ya kukodisha minara ya mawasiliano, jambo ambalo halikubaliki kwa sababu mfuko wa UCSAF upo kwa ajili ya kutoa ruzuku kwa kampuni za mawasiliano nchini. 

“Hili la TTCL kukopa minara katika makampuni mengine halikubaliki,  Serikali ina mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF) ambao wanatoa ruzuku kwa makampuni mengine ya simu lazima tulitazame upya.

“Nataka sasa TTCL tuwape mitaji ya kutosha ili kuhakikisha kuwa inaendelea kupanua huduma zake kwa Watanzania wengi zaidi,” amesema Rais Magufuli.


Zinazohusiana:


Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Fedha na Mipango kuipatia TTCL Sh30 bilioni iliyobaki kati ya Sh66 zilizotengwa katika mwaka wa fedha 2018/19 kwa ajili ya kupanua mtandao wa huduma zake nchini.

Kwa sasa kampuni hiyo inamilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali tangu mwaka 2016 baada ya kampuni ya Bharti Airtel ya nchini India kuikabidhi Serikali hisa zake  ilizokuwa inamiliki katika kampuni hiyo. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba amesema kampuni hiyo inaendelea kusimamia majukumu yake ya msingi ya kuimarisha mfumo wa viwango vya huduma kwa mteja, kujenga uwezo wa teknolojia na miundombinu pamoja na kusimamia mkakati wa mawasiliano kupitia Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa.

Amesema wataendelea kujiimarisha zaidi ili kutanua wigo wa upatikanaji wa huduma nchi nzima ili kuhimili soko la ushindani katika sekta ya mawasiliano.

Enable Notifications OK No thanks