TRC kuajiri wafanyakazi 2460 ujenzi wa SGR Dar- Makutupora
- Ajira hizo zitatolewa kwa awamu mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26.
Arusha. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema linatarajia kuajiri wafanyakazi 2,460 katika mradi wa reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) kwa vipande viwili vya Kutoka Dar es Salaam mpaka Makutopora.
Kwa mujibu wa chapisho la TRC lililotolewa leo Agosti 20, 2025 ajira hizo zitatolewa kwa awamu mwaka wa fedha 2024/25 iliyokwisha muda wake na 2025/26.
“Katika ajira hizo 2,460 utekekezaji wake ni awamu ambapo katika mwaka wa fedha 2024/25 zaidi ya watumishi 500 wameshaajiriwa na mwaka huu wa fedha 2025/26 matarajio ni kuajiri watumishi 272 na TRC itaendelea kuajiri kufikia watumishi 2,460,” imesema taarifa hiyo ya TRC iliyochapishwa katika mtandao wa Instagram.
Aidha, TRC imebainisha kuwa wakati utekekezaji wa utoaji ajira rasmi ukiendelea, tayari ajira 115,000 kutoka kwa mkandarasi zimenufaisha makundi mbalimbali ikiwemo vijana wa elimu ya darasa la saba na viwango vingine vya elimu katika fani mbalimbali.
Kati ya hizo ajira 35,000 ni za moja kwa moja na zaidi ya ajira 80,000 ni zisizo za moja kwa moja zikijumuisha makundi mbalimbali kama baba na mama lishe, bodaboda, bajaji na watoa huduma za makampuni mbalimbali ya mawasiliano kama vocha na laini za simu.
Utoaji wa ajira hizo ni utekelezaji wa maagizo na maelekezo ya Serikali yaliyotaka miradi yote inayoendelea nchini inufaishe wazawa hususani wakazi wa maeneo yanayozunguka miradi.