Toyota, Suzuki kuunda gari la pamoja

June 24, 2022 2:27 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Uzalishaji wa gari hilo litakalouzwa kama modeli za Suzuki na Toyota unatarajiwa kuanza Agosti mwaka huu.
  • Lengo la ushirikiano huo ni kubadilishana teknolojia na kupunguza gharama.
  • Wadau wa magari watabiri itakuwa gari nzuri.

Dar es Salaam Ikiwa wewe ni mpenzi wa magari kutoka kampuni za Toyota na Suzuki huenda ukapata suluhisho ya kudumu kufuatia uamuzi wa kampuni hizo kutangaza kushirikiana kuunda gari jipya. 

Uzalishaji wa gari hilo unatarajiwa kuanza mapema Agosti mwaka huu katika kiwanda cha Toyota kilichopo Kusini mwa India modeli ya gari hilo litauzwa kama kwa majina ya Suzuki na Toyota mtawalia.

Suzuki na Toyota ni kampuni kubwa za utengenezaji wa magari zai Japan ambazo zimejizolea umaarufu ulimwenguni kwa ubora wa vifaa hivyo vya moto. Toyota inafahamika zaidi kwa magari yake kudumu kwa muda mrefu na gharama nafuu huku Suzuki ikifahamika kwa kuuza magari imara na yasiyo tumia mafuta mengi.

“Toyota na Suzuki wataliuza gari hili  katika soko la India kama bidhaa yao mpya lakini pia itasafirishwa katika soko la nje ya India ikiwemo Afrika,” imeeleza taarifa iliyotolewa hii leo Juni 24, 2022  na kampuni ya Toyota. 

Uzalishaji huo wa pamoja unatarajiwa kuja na matoleo mawili  ya magari  modeli ya SUV (Sport Utilized Vehicle) ambayo ni magari madogo ya abiria lakini hupewa uwezo wa kupita katika maeneo korofi na injini yenye uwezo wa kusukuma magurudumu manne kwa pamoja yaani  (Four wheel drive). 

Mojawapo ya modeli ya magari yatakayozalishwa katika ushirikiano huo itakuwa ya umeme ambayo itazalishwa na Toyota na isiyo ya Umeme itazalishwa na Suzuki. Mradi huo ni muendelezo wa ushirikiano kati ya kampuni hizo ulioasisiwa mwaka 2017. 

Kampuni ya Toyota kwa muda sasa imekuwa ikikosolewa kwa kuwa nyuma katika uzalishaji wa magari yanayotumia umeme tofauti na Tesla . Toyota imekuwa ikijitetea kuwa inaendelea kuzalisha magari ya mafuta na gesi kwa ajili ya maeneo ambayo teknolojia ya umeme haijafika hivyo itaendelea kutengeneza magari yasiyotumia umeme. 

Itakumbukwa mapema mwezi Julai mwaka huu Umoja wa Ulaya(EU) ulipitisha azimio la kupitisha sheria itakayoyataka kampuni ya uzalishaji wa magari barani Ulaya kuzalisha magari ya umeme pekee ifikapo mwaka 2024.

India ni miongoni mwa mataifa yanayohamasisha uzalishaji wa magari ya umeme jambo linalotekelezwa taratibu mno kwa kuwa ni kampuni ya Tata pekee iliyoanza kuzalisha magari hayo.

Kampuni ya Suzuki ilisema mwezi Machi itawekeza Dola za Marekani Bilioni 1.4 sawa na Sh3.2 trilioni kwa ajili ya uzalishaji wa magari ya umeme nchini India lakini magari hayo yataingizwa sokoni rasmi mwaka 2025.

 Hata hivyo, Toyota yenyewe imesema itatenga Dola za Marekani milioni 600 sawa na Sh1.3 trilioni katika taifa hilo kwa ajili ya uzalishaji wa magari ya umeme.

Magari yanayotumia teknolojia ya umeme yanauzwa bei ghali nchini India na maeneo mengine duniani kutokana na malighafi zinazotumika wakati wa uzalishaji na hiyo ndio sababu kubwa iliyosababisha kampuni hizo kuungana na kukubaliana kubadilishana teknolojia na kupunguza gharama za uzalishaji. 

Daudi Mbapani mkazi wa jijini Dar es Salaam, aliyewahi kutumia magari ya kampuni zote mbili, amesema anatarajia kuwa gari hilo litakuwa zuri kwani kampuni zotei huzalisha magari bora na vifaa vyake hupatikana kirahisi.

“Mi nadhani itakuwa gari nzuri kwa sababu kampuni zote  zinatengeneza magari mazuri na upatikanaji wa vifaa vyake ikitokea imeharibika ni rahisi kwa hiyo tusubiri tuone,” amesema Mbapani. 

Enable Notifications OK No thanks