Toolboksi ya Tanzania yapenya tuzo za ‘Startups’ bora kusini mwa Afrika

Ushindi wa Toolboksi siyo wa goli la mkono kwani kabla ya ushindi wake, imeshindanishwa na kampuni nyingine ya Kitanzania zikiwemo Smart Lab, Robotech na Jiajiri bila kusahau zile za kimataifa. Picha| SASAwards.
- Tuzo hizo zilihusisha kampuni takriban 3,000 katika ukanda huo
- Toolboksi ni kampuni pekee ya Kitanzania iliyo shinda kwa ngazi ya kikanda
- Nchi ya Afrika Kusini imeshikilia zaidi ya asilimia 60 ya tuzo hizo
Dar es Salaam. Kampuni ya huduma za ufundi wa kidijitali, Toolboksi imetangazwa kunyakua tuzo ya kampuni bora inayochipukia yenye tija kwa jamii “Best Social Impact Startup” nchini Afrika Kusini ikizipiga vikumbo kampuni 9 zikiwemo za Afrika Kusini, Mauritius na Malawi.
Toolboksi ambayo inashikilia taji hilo kutoka kwa “Southern Africa Startup Awards” ya Afrika Kusini, imejinyakulia ushindi huo ikiwa ni kampuni pekee kutokea Tanzania ambayo imeziona tuzo hizo zilizohusisha makampuni takribani 3,000.
Mbali na Tanzania, nchi nyingine zilizopenya kwenye tuzo hizo za wadau wa teknolojia ni pamoja na Mauritius, Afrika Kusini, Angola, Msumbiji, Namibia na Zimbabwe.
Orodha hiyo, inaonyesha ni nchi saba tu kati ya nchi 12 za kusini mwa Afrika ndizo zilizonyakua tuzo hizo huku Afrika Kusini ikishikilia tuzo 11 sawa na asilimia 61 ya tuzo zote na kuacha tuzo saba zikigombewa na mataifa mengine ikiwemo Tanzania.
Hata hivyo, ushindi wa Toolboksi siyo wa goli la mkono kwani kabla ya ushindi wake, imeshindanishwa na kampuni nyingine ya Kitanzania zikiwemo Smart Lab, Robotech na Jiajiri bila kusahau zile za kimataifa.
Akiziongelea tuzo hizo, Mkurugenzi wa Toolboksi Julius Mbungo amesema mbali na cheti na tuzo waliopata, kushinda mashindano hayo ni hatua kubwa kwa kampuni hiyo kwa kuwa imefungua milango ya kimataifa ya kampuni hiyo.
Zinazohusiana
- Mhariri Nukta Africa apata tuzo ya habari za takwimu 2019
- Mfahamu Given Edward, mtanzania aliyeshinda tuzo mbili za kimataifa katika sekta ya elimu
- Mtanzania atwaa tuzo ya ubunifu nchini Misri
Kwa kuanza tu, ushindi huo umeipatia Toolboksi mdau wa teknolojia ambaye atafanya nao kazi kuboresha hali ya kiteknolojia kwenye oparesheni zake.
“Tumepata partner (mdau) wa teknolojia ambaye amejitolea kutusaidia kutatua changamoto zetu za kiteknolojia. Mashindano haya yana maana kubwa sana kwangu na kwa timu nzima ya Toolboksi,” amesema Mbungo.
Tuzo za Startup za nchi za Kusini mwa Africa ni njia kuelekea Tuzo za startup za dunia zitakazofanyika Desemba 11-14 nchini China ambapo Mbungo na timu ya Toolboksi watashindanishwa na washindani wengine kutoka kanda nyingine duniani.
“Tayari hii ni hatua kubwa maishani. Imeipatia Toolboksi hamasa kwani sasa tunatambulika kimataifa. Tofauti na awali, sasa itahitaji maelezo madogo kumwelezea mdau yeyote wa teknolojia juu ya kampuni yetu,” amesema Mbungo ambaye anaamini tuzo hii imempa umaarufu mkubwa kwenye ulimwengu wa kiteknolojia na masoko.