Mhariri Nukta Africa apata tuzo ya habari za takwimu 2019

Rodgers George 0326Hrs   Novemba 30, 2019 Habari
  • Ni Daniel Samson aliyeibuka mshindi wa kwanza.
  • Ni tuzo ya Mwandishi bora wa habari za kitakwimu inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
  • Nafasi ya kwanza na ya pili imeenda kwa Veronica Mrema wa gazeti la Jamvi la Habari na Halili Letea wa gazeti la Mwananchi.

Dar es Salaam. Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeanzisha tuzo ya Mwandishi bora wa habari za kitakwimu na kwa mwaka huu wa 2019, tuzo hiyo ametunukiwa Mhariri wa kampuni ya teknolojia na habari ya Nukta Africa, Daniel Samson.

Katika kuhamasisha uandishi bora wa kitakwimu, NBS imeamua kuanzisha tuzo hiyo kwa vyombo vya habari vinavyoandika habari za kitakwimu na mwandishi bora wa habari za kitakwimu kuanzia mwaka huu.

Wakati akitoa tuzo hiyo Novemba 28, 2019 katika Siku ya Takwimu Afrika jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, amesema tuzo hiyo imeenda kwa wanahabari watatu ambapo nafasi ya kwanza imeshikiliwa na mwanahabari Samson. 

Wengine waliopata tuzo hiyo ni Veronica Mrema kutoka gazeti la Jamvi la Habari aliyeshika nafasi ya pili huku mwanahabari kutoka gazeti la Mwananchi, Halili Letea akishika nafasi ya tatu.

Dk Mpango amesema uanzishwaji wa tuzo hizo ni hatua nzuri katika kuongeza uelewa wa masuala ya takwimu kwa sababu vyombo vya habari viko karibu na wananchi na vina uwezo wa kuwafikia kwa urahisi na haraka zaidi.

Amesema kama takwimu zitakusanywa na kutolewa kwa usahihi zitawasaidia wananchi na Serikali katika utekelezaji wa sera, mipango na maumuzi ya matumizi ya rasilimali za umma..

Wanahabari hao wote watatu wamekabidhiwa vyeti na fedha taslimu, ikiwa ni hatua ya mwanzo ya kutambua mchango walioutoa kupitia habari za kitakwimu walizoandika hasa katika kuiwezesha jamii kufanya maamuzi sahihi ya maendeleo.


Soma zaidi: 


Akizungumza mara baada ya kupata tuzo hiyo, mwanahabari Samson amesema tuzo hiyo ni heshima kubwa aliyopewa na NBS na imemuongezea nguvu ya kufanya kazi kwa bidii na kubobea zaidi katika uandishi wa habari za kitakwimu zitakazosaidia kuboresha maisha ya Watanzania.

"Nafarijika kupata tuzo hii kwa sababu ni ya kwanza tangu nianze kufanya kazi za uandishi wa habari miaka mitano iliyopita. 

“Tuzo hii ina maana kubwa kwangu hasa katika uandishi wa habari za takwimu ambazo ni muhimu katika kupambana na habari za uzushi na kusaidia jamii kufanya maamuzi katika maeneo mbalimbali ya maendeleo," amesema Samson.

Amesema anaamini tuzo hiyo itafungua fursa kwa wanahabari wengi zaidi kuongeza kasi ya kuandika habari za takwimu ili na wao wapate mwaka ujao.

Tuzo za mwandishi bora zitakuwa zikitolewa siku ya kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika ambayo hufanyika mwezi Novemba kila mwaka. Mwaka huu, kwa Tanzania, Maadhimisho hayo yalifikia kilele Novemba 28, 2019.

Aidha, tuzo hiyo itawahamasisha na kuwashajiisha waandishi wa habari kutumia takwimu kuchambua, kuhoji na kuchunguza masuala yanayoisibu jamii ili kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa takwimu na matumizi yake ambayo yanatawala maisha ya kila siku. 

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akimkabidhi zawadi Mharire wa Nukta Africa, Daniel Samson baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa kwanza katika tuzo ya Mwandishi bora wa habari za kitakwimu 2019. Picha|NBS.

Mkuu wa Mafunzo wa Nukta Africa, Daniel Mwingira ameishukuru NBS kwa kutoa tuzo hiyo kwa mwanahabari Samson kuwa mshindi wa kwanza kama mwandishi bora wa habari za takwimu.

“Hii kwetu kama kampuni ni heshima kubwa na kuzingatia kuwa tumejikita katika mafunzo na kuandika habari za takwimu ni hatua kubwa kwetu katika kutoa mchango katika tasnia ya habari Tanzania,” amesema Mwingira.

Mwingira amesema tuzo hiyo imeonyesha kuwa hata vyombo vya habari vya mtandaoni (online media) kama vikifuata misingi ya kihabari katika kuendesha vyombo hivyo na kuandika habari kwa kuzingatia weledi vinaweza kuwa sehemu ya kutoa mchango muhimu kwenye jamii.

Nukta Africa inamiliki tovuti ya habari ya www.nukta.co.tz na hufanya mafunzo kwa wanahabari na wadau wengine katika uandishi wa habari za takwimu na matumizi ya dijitali katika kuzalisha habari. 

Related Post