Toolboksi: Teknolojia inayowaunganisha vijana na fursa za ufundi stadi Tanzania
- Ni jukwaa la mtandaoni linaliwawezesha vijana wenye ujuzi na stadi za ufundi kuwafikia watu wenye uhitaji wa kutengenezewa au kufanya marekebisho ya vifaa, ofisi na nyumba za kuishi.
- Inasaidia kuongeza fursa za ajira kwa vijana waliobobea katika fani mbalimbali za ufundi.
- Moja ya kibarua ilichonacho kampuni hiyo changa inakabiliana nacho ni kuhakikisha inakamilisha programu tumishi (app) ya huduma hiyo ili kuwafikia watu wengi.
Dar es Salaam. Wewe ni kijana mbunifu na una ujuzi wa kutengeneza kazi za mikono lakini umekosa sehemu sahihi ya kuonyesha uwezo wako ili kujipatia kipato cha kuendesha maisha?
Usihofu teknolojia ndiyo mpango mzima katika zama hizi za matumizi ya simu na kompyuta kwa sababu inakuletea suluhisho na kukufungulia fursa mbalimbali mkononi mwako.
Wabunifu wamebuni tovuti maalum ya toolboksi ambayo ni nyenzo muhimu kuwaunganisha vijana wa rika tofauti wenye ujuzi na stadi za maisha kama uselamala, ufundi ujenzi, magari, vifaa vya umeme, utunzaji wa bustani, nyumba na fursa mbalimbali za ufundi zilizopo katika jamii.
Tovuti hiyo, iliyobuniwa na kuendeshwa na kampuni ya teknolojia ya Toolboksi Limited ya Tanzania, ni jukwaa linalowasaidia vijana waliojiajiri kuwafikia watu na taasisi zenye uhitaji wa kutengenezewa au kukarabatiwa kifaa au kitu chochote cha ofisini au nyumbani kinachosaidia shughuli zingine zifanyike.
Kupitia toolboksi, wewe kijana unayeishi jijini Dar es Salaam hutahangaika tena kuweka matangazo au kuzunguka mitaani kutafuta wateja kwa sababu teknolojia hiyo inakuunganisha moja kwa moja na mteja wako popote alipo.
Mwanzilishi wa tovuti toolboksi, Julius Mbungo akitoa maelezo ya jinsi tovuti hiyo inavyowaunganisha vijana na fursa za ufundi stadi katika maeneo yao. Picha|Julius Mbungo.
Mwanzilishi wa tovuti hiyo, Julius Mbungo anasema tovuti hiyo pia inawasaidia watu na taasisi mbalimbali zinazohitaji mafundi wenye ujuzi tofauti kuwafanyia kazi za mikono katika maeneo yao ambapo inaondoa pengo la taarifa muhimu za ufundi katika jamii, kuharakisha shughuli za maendeleo na kuokoa muda ambao mteja na fundi wangekutana.
“Tumeamua kuja kutatua tatizo la ukosefu wa ajira na umasikini kwa sababu kuna maelfu ya watoa huduma hususan mafundi stadi, wanawake kwa wanaume ambao wana ujuzi na wako tayari kufanya kazi lakini hawapati nafasi,” amesema Mbungo.
Mbungo amebainisha kuwa maeneo ambayo yamekuwa na uhitaji mkubwa wa ufundi ni pamoja ufundi wa mabomba ya maji, umeme, uselemala, washi, ufungaji wa madishi ya visimbuzi. Maeneo mengine ni utengenezaji wa viyoyozi, kompyuta,fenicha na usafi wa nyumba.
Ukitazama kwa ukaribu utagundua kuwa maeneo hayo yanagusa moja kwa moja maisha ya mwanadamu katika nyanja za usalama wa afya na mazingira yanayomzunguka ambayo yana mchango mkubwa wa kuharibu au kuendeleza maisha ya binadamu.
Tayari toolboksi inafanya kazi na mashirika na taasisi zinazowajibika moja kwa moja katika kuendeleza ujuzi na ufundi stadi kama Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), taasisi ya Digital Opportunity Trust (DOT) na kampuni ya ujenzi ya JINGU.
Soma zaidi: Msichana wa miaka 19 aibuka na suluhisho la FundiPopote
Vijana wanaounganishwa katika jukwaa hilo wanapatiwa mafunzo zaidi ili kuimarisha stadi zao na jinsi ya kuwahudumia wateja ili kukidhi mahitaji wakati wakitoa huduma za ufundi.
Kwa mteja anayetaka huduma ataingia kwenye mtandao huo na kuchagua huduma inayoitaka na kuweka oda. Baada ya hapo utapokea barua pepe, ujumbe mfupi wa maneno (SMS) au kupigiwa simu kulingana na njia uliyotuma maombi.
Mafundi wa toolboksi watafika nyumbani au ofisini kwako kwa kutumia anuani ya makazi kufanya tathmini ya ukubwa wa kazi na kufanya makubaliano ya bei. Baada ya makubaliano kazi itafanyika kwa uangalifu mkubwa kulikangana na mahitaji ya mteja.
Kazi ikikamilika malipo yatafanyika hapo hapo baada ya kujaza fomu maalum ili kuthibitisha kama kazi imefanyika vizuri.
Watumiaji wa huduma za kifedha kupitia simu watasubiri kidogo wakati tovuti hiyo itakapokamilisha mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao.
Toolboski ni nyenzo muhimu kuwaunganisha vijana wa rika tofauti wenye ujuzi na stadi za maisha kama ufundi ujenzi na fursa mbalimbali za ufundi zilizopo katika jamii. Picha|Toolboksi.
Toolboksi inawafikia vijana wote hadi wale wasiotumia intaneti ambapo wanaweza kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi wa maneno ili kuunganishwa katika orodha ya mafundi ambao wameidhinishwa kufanya shughuli hizo katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Mpaka sasa jukwaa hilo la mtandaoni limeweza kusajili vijana rasmi 350 na 500 wasio rasmi wa Dar es Salaam wenye ujuzi na kuwaunganisha na wateja waliopo katika maeneo mbalimbali ili kujipatia kipato cha kuendesha maisha.
Hata hivyo, huduma haipatikani kwa mikoani kwa sasa jambo linalofanya mafundi wa maeneo hayo kukosa fursa ambazo wenzao wa Dar es Salaam wanazipata.
Siku zijazo, Mbungo amesema wamepanga kuwafikia vijana wa mikoa ya Mbeya, Arusha na Dodoma ikiwa ni hatua ya kuongeza wigo wa huduma na kushiriki katika mikakati ya wadau wa maendeleo kuwaondolea vijana umasikini na kuwaunganisha na fursa zilizopo katika jamii.
Moja ya kibarua kigumu kampuni hiyo changa inakabiliana nacho ni kuhakikisha inakamilisha programu tumishi (App) ya huduma hiyo kwa kuwa sehemu kubwa kwa sasa watumiaji wa huduma za intaneti wanatumia simu za mkononi kupata huduma.