Msichana wa miaka 19 aibuka na suluhisho la FundiPopote
- Changamoto za kuwepo kwa vifaa vibovu bila kutengenezwa kumemsukuma kuanzisha sehemu itakayowakutanisha mafundi na wateja.
- Wadau washauri aboreshe zaidi mfumo wa ukutanishaji wa mteja na fundi ili usijeleta usumbufu.
Dar es Salaam. Kila kukicha vijana wanazidi kutatua matatizo yaliyopo kwenye jamii kwa kutumia njia ya ubunifu wa kiteknolojia katika nyanja mbalimbali za elimu, biashara, fedha, afya na nyinginezo.
Lakini ushawahi kufikiria kuwa kuna huduma nyingine kama upatikanaji wa mafundi pale unapohitaji kutengenezewa kifaa kilichoharibika au ukitaka kushona nguo jinsi inavyosumbua hasa ukiwa huna kwa kuanzia katika kuwapata mafundi.
Hii pia imemtokea mbunifu anayechipukia Queen Mtega (19) ambaye aliona tatizo la upatikanaji wa mafundi mwaka 2018, alipotoka katika mafunzo yake ya jeshi la kujenga taifa na kuamua kutafuta suluhisho litakalowasaidia watu wengi kupata mafundi kwa njia ya Tehama.
Queen ameiambia Nukta chanzo cha yeye kuanzisha tovuti yake ya FundiPopote ni baada ya kwenda kutembelea nyumbani kwa rafiki yake na kuomba maji ya kunywa, lakini alipewa ya moto na wakamwambia jokofu limeharibika.
“Mama wa rafiki yangu akasema anataka kununua jokofu lingine, lakini niliona lina uwezo wa kutengenezeka, hapo ndio wazo la FundiPopote likaja,” amesema Mtega.
Licha ya umri wake mdogo akaona kuna haja ya kuunganisha mafundi na wateja sehemu moja ili wanaokumbana na matatizo ya kuharibika kwa vifaa vyao au wanaotaka kupata huduma za kushonewa nguo, waweze kupata nafasi ya kukutana.
Hata hivyo Mtega ameiambia Nukta kuwa haikuwa rahisi kupata mafundi na kuwaunganisha na wateja moja kwa moja, kwa sababu ya umri wake mdogo mafundi wengi hawakumwamini lakini haikumkatisha tamaa na kufanikiwa kuwapata mafundi.
Jinsi Fundi Popote inavyoonekana katika tovuti ambayo inamrahisishia mteja kuona moja kwa moja walipo mafundi katika eneo lake. Picha| Zahara Tunda
Pamoja na hayo Mtega anatarajia kuzunguka mikoa mbalimbali Tanzania ili kukusanya taarifa za mafundi hapo mbeleni ili kusaidia huduma hiyo kupatikana sehemu yoyote mteja anapopatikana.
Hata hivyo, changamoto huwa haziwezi kuepukika katika kufanikisha jambo lolote lile, kutokana na kila mtu kuchukulia jambo kwa njia tofauti.
Hilo pia limemtokea Mtega alipokuwa anaanza kukusanya taarifa za mafundi huku akiweka wazi haikuwa rahisi kuwapata mafundi cherehani.
“Mafundi wa gereji na wa vifaa vya elektroniki haikuwa shida kuwapata ila mafundi cherehani wengi walikataa na kusema tayari wanawateja wao binafsi, hawataki kujitangaza zaidi,” amesema Mtega.
Teknolojia haijaachwa nyuma
Pamoja kuunganisha mafundi Mtega hajaacha kutumia mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter na Instagram ili kujitangaza na kumfanya aweze kujulikana na kuwafikia watu ambao FundiPopote itaweza kuwasaidia.
“Vilevile kwenye tovuti ya FundiPopote tumetumia ramani za Google hivyo inakuwa rahisi kwa mteja kumpata fundi wa eneo lake na mawasiliano ya fundi huyo,” amesema Mtega
Zinazohisiana: Uhaba wa wanawake sekta ya teknolojia wakwamisha utekelezaji wa ajenda za maendeleo
‘Maisha Package’ kifurushi kinachowakinga wasichana dhidi ya mimba zisizotarajiwa
Hata hivyo, ili huduma hiyo iweze kufanikiwa fundi atakuwa na ulazima wa kulipa asilimia 10 ya atakachokipata ili mtandao huo uweze kuendelea kujiendesha wenyewe.
Huku wadau wamepongeza juhudi hizo ambazo zitawarahisishia kazi wale wasiokuwa na muda wa kuzunguka kutafuta mafundi na kumtaka aboreshe zaidi mfumo wa ukutanishaji wa mteja na fundi ili usijeleta usumbufu.
“Ni jambo zuri ila wateja wengi wanatumia mafundi wa mwendokasi ambao wanataka pesa ya haraka bila ubora,” amesema William John, fundi kutoka Mbagala.
John ameshauri kuwepo na njia nzuri ya kumfanya mteja atambue thamani ya fundi na kumlipa vizuri hata kama watakuwa wamekutana kwenye mtandao ili kila mmoja wao aweze kunufaika.