TMA yatahadharisha ujio mvua kubwa Aprili

March 30, 2019 8:13 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Athari za mvua kubwa ni pamoja na uharibifu wa miundombinu ya barabara na kutatiza shughuli za usafiri. Picha|Mtandao.


  • Mvua hiyo inatarajia kunyesha katika baadhi ya maeneo yanayopata mvua za masika katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Morogoro, Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es Salaam.
  • Mvua hiyo inaweza kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwemo usafiri katika baadhi ya maeneo nchini.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya kunyesha mvua kubwa katika kipindi cha wiki mbili zijazo inayoweza kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii katika baadhi ya maeneo nchini.

Shughuli nyingine zinazoweza kuathirika ni pamoja na sekta ya usafiri hasa barabara zinazotumika kupitisha magari ya abiria na mizigo.

Kwa mujibu wa taarifa ya TMA iliyotolewa jana (Machi 29, 2019) inaeleza kuwa mvua zinatarajiwa kunyesha katika maeneo mengi yanayopata mvua za masika baada ya athari ya upungufu wa mvua uliotokana na vimbunga vilivyojitokeza mfululizo katika bahari ya Hindi ikiwemo kimbunga Idai, Savannah na Joaninha katika mifumo ya hali ya hewa kuanza kupungua. 

“Vipindi vya mvua vinatarajiwa kuongezeka katika baadhi ya maeneo katika wiki mbili zijazo za mwezi Aprili, 2019,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Vipindi vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya,
Songwe, Rukwa, Morogoro (Mahenge) na mikoa ya Lindi na Mtwara katika kipindi cha mwisho wa wiki kuanzia Machi 30 hadi Aprili 3, 2019.

Pia mwanzoni mwa Aprili, 2019 vipindi vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa kujitokeza katika mkoa wa Morogoro na kusambaa katika maeneo machache ya mikoa ya Pwani na Dar es Salaam. Hata hivyo, mvua hiyo imeanza kunyesha katika baadhi ya mkoa wa Dar es Salaam.


Soma zaidi: 


Katika hatua nyingine, TMA imesema wimbi la joto lililojitokeza katika kipindi cha upungufu wa mvua katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini na Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki hasa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani linatarajiwa kupungua kiasi katika kipindi cha uwepo wa mvua.

“Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kuzingatia tahadhari zilizotolewa na marejeo yake pamoja na kupata na kuzingatia ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza,” imeeleza taarifa hiyo.

Enable Notifications OK No thanks