TMA yatabiri mvua kubwa za masika, ikiwatahadharisha wavuvi, wakulima
- TMA yawataka kutumia vizuri ujio wa mvua hizo kuzalisha mazao mengi.
- Watumiaji wa bahari watahadharishwa kutokea vipindi vifupi vya upepo mkali vitakavyoathiri shughuli zao.
- Wananchi watakiwa kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa ili kufanya maamuzi sahihi katika maeneo yao.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wananchi kujiandaa na kutumia vema mvua za msimu za masika zinazotarajia kuanza hivi karibuni huku ikitahadharisha kutokea kwa vipindi vifupi vya upepo mkali katika pwani ya bahari ya Hindi na kuathiri shughuli za uvuvi na utalii.
Msimu wa mvua za masika ni mahususi kwa meneo yanayopata vipindi viwili vya mvua kwa mwaka kwa kipindi cha Machi hadi Mei, 2020 (MAM).
Maeneo hayo ni nyanda za juu kaskazini mashariki yenye mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro; pwani ya kaskazini (Dar es Salaam, Pwani ikijumuisha kisiwa cha Mafia, Tanga na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba).
Maeneo mengine ni ukanda wa Ziwa Victoria katika mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi amewaambia wanahabari leo (Februari 13, 2020) jijini Dar es Salaam kuwa mvua zitakuwa za kutosha maeneo hayo yanayopata vipindi viwili vya mvua kwa mwaka hivyo kuwafaidisha wakulima na wafugaji katika shughuli zao za uwekezaji na uzalishaji mazao.
“Kutokana na mifumo ya hali ya hewa ilivyo kwa sasa na jinsi inavyotarajiwa kuwa kwa kipindi chote cha msimu, kwa ujumla mvua za wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka,” amesema Dk Kijazi.
Amesema mvua hizo za masika zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya mkoa iliyotajwa, isipokuwa kwa maeneo ya mkoa wa Kagera, magharibi mwa mkoa wa Geita, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Pwani (ikijumuisha kisiwa cha Mafia) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
“Kwa maeneo yanayotarajiwa mvua za wastani hadi juu ya wastani, mvua hizo zinaweza kufaa kwa uzalishaji wa mazao ikiwa ni pamoja na yale yanayoweza kustawi kwenye unyevunyevu wa udongo uliopitiliza kama vile mpunga,” amesisitiza Dk Kjazi ambaye pia ni Makamu Rais wa tatu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

Mifugo, mazao hatarini kuathirika
Katika kipindi hicho wadudu waharibibu wa mazao, magonjwa ya mifugo kama vile homa ya bonde la ufa, ugonjwa na kwato na midomo yanaweza kujitokeza kutokana na hali ya maji maji na maji yaliyotuama.
Aidha, katika maeneo ambayo mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa, wakulima wanashauriwa kupanda mazao yanayokomaa mapema na yasiyohitaji maji mengi katika ukuaji wake na kuhifadhi malisho na kuvuna maji ya mvua kwa matumizi ya baadaye.
Hata hivyo, mvua za nje ya msimu zinazoendelea kunyesha katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, hususan yaliyopo katika pwani ya kaskazini zinatarajiwa kuendelea na kuungana na msimu wa mvua wa masika mwaka 2020.
Soma zaidi:
- TMA yatahadharisha ujio mvua kubwa
- Watanzania washauriwa kutumia taarifa za hali ya hewa kwenye mipango ya maendeleo
- Ujio mfumo wa taifa wa hali ya hewa kuchochea ujenzi wa viwanda nchini.
Watumiaji wa bahari na maziwa watahadharishwa
Watumiaji wa bahari ya Hindi na Ziwa Victoria wametakiwa kuchukua tahadhari kwa sababu kuna uwezekano wa kutokea vipindi vifupi vya upepo mkali vitakavyoathiri shughuli za kawaida za uvuvi na utalii wakati msimu wa mvua za masika ukikaribia kuanza.
“Uwezekano wa vipindi vifupi vya upepo mkali unaweza kutokea na hivyo kuathiri shughuli za uvuvi baharini,” amesema Dk Kijazi na kubainisha kuwa katika utabiri wao hawatarajii vimbunga katika kipindi chote msimu wa masika.
Kutokana na hali hiyo, watumiaji wa bahari na maziwa wametakiwa kufuatilia kwa karibu taarifa za kila siku za TMA ili kujua hali ya hewa katika maeneo yao na kujiweka katika nafasi ya kupunguza athari zinazoweza kutokea.
TMA imewataka watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, mamlaka za wanyamapori, wasafirishaji, mamlaka za maji na afya kuendelea kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika.
Latest