Televisheni zitaendelea “kudunda” muda mrefu ujao-ITU

November 22, 2019 7:14 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) za hadi Juni mwaka 2019, zinaeleza kuwa Tanzania ina vituo vya radio 158 na televisheni 51 na idadi hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka. Picha|Mtandao.


  • Shirika la Mawasiliano la Umoja wa Mataifa (ITU) limesema chombo hicho cha mawasiliano kitaendelea kuongeza uelewa wa masuala ya mambo mbalimbali duniani. 
  • Kauli hiyo imetolewa jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Televisheni duniani.
  • Idadi ya Watanzania wanaomiliki televisheni yazidi kuongezeka.

Dar es Salaam. Ikiwa imepita siku moja baada ya Watanzania kuungana na wenzao duniani kuadhimisha Siku ya Televisheni, Shirika la Mawasiliano la Umoja wa Mataifa (ITU) limesema chombo hicho cha mawasiliano kitaendelea kuwa na umuhimu mkubwa katika kuongeza uelewa wa masuala ya mambo mbalimbali duniani. 

Siku ya Televisheni duniani huadhimishwa Novemba 21 ya kila mwaka ili kutathmini mchango wa chombo hicho katika kuwaletea binadamu maendeleo. 

Katibu Mkuu wa ITU, Houlin Zhao katika kauli yake ya siku hiyo amesema kuwa televisheni inaendelea kuwa na dhima muhimu katika kuunganisha ulimwengu wa kubadilishana taarifa ilihali ikiwapatia watumiaji chaneli nyingi zaidi za burudani.

Katika taarifa iliyotolewa na ITU, Zhao amesema siku ya televisheni duniani inatoa fursa ya kuonyesha kazi ya kipekee na ya mfano ya ITU ya kuzalisha kazi zinazozingatia viwango ambavyo vinachochea mwelekeo ujao wa utangazaji na huduma za intaneti ambazo zinasaidia kuwapatia watumiaji kote ulimwenguni uzoefu wa kipekee.

Umoja wa Mataifa umekumbusha kuwa televisheni inaendelea kuwa chanzo muhimu cha matumizi ya video na kwamba, “ingawa ukubwa na  umbo la skrini umebadilika na watu wanatumia na kuweka video kupitia majukwaa tofauti, bado idadi ya kaya zinazomiliki televisheni duniani inazidi kuongezeka.”

Aidha, muingiliano kati ya teknolojia za kisasa za utangazaji na zile za zamani unajenga fursa ya kuongeza uelewa juu ya masuala muhimu yanayokabili jamii na dunia kwa sasa.


Zinazohusiana:


Kwa mujibu wa ripoti ya mapato na matumizi ya kaya mwaka 2017/18 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kuwa idadi ya Watanzania waishio Tanzania bara wanaomiliki televisheni imeongezeka kutoka asilimia 16 mwaka 2011/2012 hadi asilimia 24 mwaka jana. 

Mario Maniewicz, ambaye ni Mkurugenzi wa ofisi ya mawasiliano ya radio ya ITU amesema kuwa, hivi sasa kuliko wakati wowote ule, televisheni inatoa taarifa, habari na burudani kwa watu popote pale walipo.

Amesema kazi iliyopo ni kuendeleza mifumo ya viwango vipya vya utangazaji, na kuhakikisha vinaendana na teknolojia za kisasa zaidi zilizobuniwa ili matangazo ya televisheni yawe ya ubora zaidi na yapatikane kwa watu wote hata wale walio maeneo ya vijijini. 

Pia takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) za hadi Juni mwaka 2019, zinaeleza kuwa Tanzania ina vituo vya radio 158 na televisheni 51 na idadi hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW