Teknolojia ya kutengeneza matofali kwa taka za plastiki yaingia sokoni

July 30, 2019 7:23 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Wanafunzi wakiwa kwenye darasa lililotengenezwa kwa matofali ya plastiki nchini Ivory Coast. Picha|Mtandao.


  • UNICEF na kampuni ya Colombia Conceptos Plasticos wamezindua kiwanda ambacho kitabadilisha taka za plastiki  kuwa matofali ya kawaida ya plastiki. 
  • Matofali hayo yanatumika kujenga madarasa nchini Ivory Coast.
  • Yanapunguza gharama za ujenzi kwa sababu hayaungui moto, hayapitishi maji na yanadumu kwa muda mrefu. 
  • Ni njia nyingine kuondoa umaskini na kuokoa mazingira ya nchi za Afrika. 

Dar es Salaam. Wakazi wa bara la Afrika ikiwemo Tanzania ambao wanakabiliwa na changamoto ya makazi duni na gharama kubwa za ujenzi, sasa watapata ahueni baada ya wabunifu kuingiza sokoni teknolojia mpya ya kutengeneza matofali kwa kutumia taka za plastiki. 

Teknolojia hiyo ambayo imeanza kutumika nchini Ivory Coast inasaidia kuboresha elimu ya watoto wa nchi hiyo kwa kuwawezesha kusoma katika madarasa yaliyotengenezwa vizuri kwa tofali za plastiki. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) kwa kushirikiana na kampuni ya biashara ya kijamii ya Colombia Conceptos Plasticos, jana (Julai 29, 2019) wamezindua kiwanda cha kwanza cha aina yake ambacho kitabadilisha taka za plastiki  kuwa matofali ya kawaida ya plastiki. 

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa (UN) inaeleza kuwa taka hizo zilizokusanywa nchini Ivory Coast zinabadilishwa kuwa matofali ya kawaida ya plastiki ya gharama nafuu na yanayodumu kwa muda mrefu, ambayo yatatumika kujenga vyumba vya madarasa vinavyohitajika sana katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

“Kiwanda hiki kitakuwa cha aina yake na cha kisasa kinachojali mazingira na kuwa suluhisho nzuri la  hatari na changamoto kubwa za kielimu ambazo zinawakabili watoto wa Afrika na jamii zao. 

“Umuhimu wake mkubwa  ni kujenga maradasa zaidi kwa watoto nchini Ivory Coast, kupunguza taka za plastiki kwenye mazingira, na kuongeza kipato kwa familia nyingi masikini,” amesema Mkurugenzi mkuu wa UNICEF, Henrietta Fore katika taarifa hiyo. 


Zinahusiana:


Kwa mujibu wa UNICEF, Ivory Coast inahitaji madarasa15,000 ili kukidhi mahitaji ya watoto wasio na mahali pa kusomea. 

Ili kuziba pengo hilo, UNICEF imeingia ubia na Conceptos Plasticos kutumia taka za plastiki zilizokusanywa katika maeneo mbalimbali katika jiji la Abidjan kwa ajili ya kujenga madarasa 500 yatakayotumiwa na watoto zaidi ya 25,000  walio na mahitaji ya haraka katika kipindi cha miaka miwili ijayo.  

Taarifa ya UN imebainisha kuwa kiwanda hicho kitakapoanza kufanya kazi kitakuwa na uwezo wa kubadili tani 9,600 za taka za plastiki na kuwa matofali kila mwaka, hatua ambayo itakuwa chachu kubwa ya kipato hasa kwa wanawake wanaoishi katika umaskini watakaoingia katika biashara hiyo.

Hadi sasa kampuni ya Conceptos Plasticos inasema madarasa tisa yameshajengwa katika maeneo ya Gonzagueville, Divo na Toumodi kwa kutumia matofali ya plastiki ili kuonyesha  jinsi ya kuyatengeneza na kuyatumia matofali hayo.

“Matofali hayo kwa asilimia 100 yanatengenezwa na plastiki na hayaungui moto, gharama zake ni asilimia 40 chini ya tofali za kawaida na uzito wake ni asilimia 20 mepesi zaidi ya tofali za kawaida na pia yatadumu mamia ya miaka zaidi ukilinganisha na tofali za kawaida. 

Kwa kuwa ni plastiki matofali haya hayapitishi maji, na yametengenezwa ili kuhimili upepo mkali,” inaeleza taarifa hiyo. 

Chumba cha darasa kilichojengwa na matofali ya plastiki. Picha|Colombia Conceptos Plasticos

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW