TBC yaweka wazi mikakati kuboresha chaneli mpya ya safari Tanzania

December 21, 2018 11:09 am · Zahara
Share
Tweet
Copy Link

Chaneli hiyo itaonyesha maisha halisi ya wanyama katika hifadhi za Taifa. Picha| Fullshangwe.


  • Imeanza mazungumzo na wadau wa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha chaneli mpya ya utalii inawafikia watu wengi na kuchangia kukuza sekta ya utalii nchini.
  • Itakuwa inatumia lugha ya Kiswahili na kutafsiriwa kwa lugha nyingine za kimataifa ili kuwafikia wateja wengi zaidi.
  • Ni sehemu nyingine ya kutangaza na kukuza utalii ndani na nje ya nchi ili kukuza pato la taifa na kuongeza ajira nchini.
  • Pia itatengenezwa programu maalum ya simu (App) itakayobeba maudhui ya chaneli hiyo ili kuwavutia vijana na watu wengine ambao hawana muda wa kuangalia runinga. 

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk Ayoub Rioba amesema wameanza mazungumzo na wadau wa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha chaneli mpya ya utalii inawafikia watu wengi na kuchangia kukuza sekta ya utalii nchini.

Hatua hiyo imekuja ikiwa zimepita siku nne tangu Waziri Mkuu Kassim Mjaliwa alipozindua chaneli hiyo iliyopewa jina la “Tanzania Safari Channel” inayosimamiwa na TBC na shirika la hifadhi za Taifa (Tanapa) na kupatikana katika king’amuzi cha Startimes.

Dk Rioba ameiambia Nukta kuwa mikakati iliyopo sasa ni kutanua wigo wa upatikanaji wa chaneli hiyo katika maeneo mbalimbali ambapo juhudi za kuwasiliana na wadau wa maendeleo zimeanza wakiwemo wamiliki wa ving’amuzi nchini.

“Tunataka kuhakikisha inapatikana kila mahali, tupo na mazungumzo na wadau kama DSTV na wengine ili tuweze kufika maeneo mengi duniani,” amesema Dk Rioba.

Pia itatengenezwa programu maalum ya simu (App) itakayobeba maudhui ya chaneli hiyo ili kuwavutia vijana na watu wengine ambao hawana muda wa kuangalia runinga. 


Zinazohusiana:


Sambamba na hilo, amesema kwa kuanzia chaneli hiyo inatumia lugha ya Kiswahili lakini wakikamilisha mazungumzo na wadau wataanza kutumia lugha zingine za kimataifa ikiwemo Kiingereza, Kichina na Kirusi ambazo zinazungumzwa na watu wengi duniani.

“Kwa kuanza tutatumia Kiswahili na baadae tutatafsiri kwa lugha  kama Kingereza, Kichina, Kirusi, Kihindi na nyinginezo,” amesema Dk Rioba.

Chaneli hiyo itakuwa kiungo muhimu katika kutangaza utalii wa Tanzania ambao haupewi hadhi inayohitajika, jambo linalotoa mwanya kwa baadhi ya watu kufaidika na vivutio vilivyomo nchini isivyo halali.

Ameeleza kuwa wana mpango wa kuajiri watu wengi wa kufanya nao kazi, hii ni kwasababu uendeshaji wa chaneli hiyo unahitaji watu wengi wenye weledi katika sekta ya utangazaji na utalii. 

“Tumeomba kwanza turuhusiwe kuajiri wafanyakazi 31 kwa kuanzia, na tutaongeza wengine zaidi,” amesema na kuongeza kuwa wafanyakazi watakaoajiriwa ni wale wenye ubunifu na uzoefu wa maisha ya viumbe na sekta ya utalii.

Tanzania sio nchi ya kwanza kuanzisha chaneli hiyo, zipo nchi mbalimbali ikiwemo Kenya zilizoanza kutumia fursa hiyo muda mrefu kuutangaza utalii katika nchi zao ambapo itakuwa ni muda muafaka kwa Tanzania kufaidika kiuchumi na chaneli hiyo.

“Kabla hatujaanzisha tulifanya utafiti na tukagundua sisi sio wa kwanza zipo nchi nyingi zinafanya hivyo, hata majirani zetu Kenya wanayo ila ni ya mtu binafsi,” amesema Dk Rioba.

Chaneli hiyo ni sehemu ya kupata burudani na taarifa muhimu za utalii ikizingatiwa kuwa itakuwa inaonyesha maisha halisi ya viumbe katika maeneo mbalimbali ya uhifadhi nchini. 

Enable Notifications OK No thanks