Tanzania yazindua mkakati wa ukusanyaji mapato wa miaka mitatu
- Unalenga kujenga bajeti endelevu itakayoiwezesha Serikali kugharamia huduma muhimu kwa wananchi bila utegemezi wa misaada kutoka nje.
Dar es Salaam. Serikali imezindua Mkakati wa Muda wa Kati wa Ukusanyaji Mapato wa miaka mitatu (2025/2026 – 2027/2028) unaolenga kuongeza mapato ya ndani, kupunguza nakisi ya bajeti na kujenga bajeti endelevu itakayoiwezesha Serikali kugharamia huduma muhimu kwa wananchi bila utegemezi wa misaada kutoka nje.
Iwapo mkakati huo ukitekelezwa kwa ufanisi huenda ukaimarisha upatikanaji wa huduma muhimu kama afya, elimu, maji na uwekezaji katika miradi ya maendeleo.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square jijini Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk Natu El-maamry Mwamba, amesema mkakati huo utaimarisha uhiari wa ulipaji kodi, kuziba mianya ya ukwepaji, na kuongeza imani ya wananchi na wawekezaji kwa mfumo wa mapato.
“Utekelezaji wa kazi hii utaboresha usimamizi wa mapato ya Serikali na kuhakikisha tunakuwa na bajeti endelevu itakayowezesha Serikali kuongeza kasi ya utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi kwa kutumia mapato ya ndani,” amesema Dkt. Mwamba.
Dk Natu ameongeza kuwa mkakati huo umeainisha maboresho katika maeneo matatu makuu ikiwemo sera za kodi, usimamizi wa ukusanyaji mapato na marekebisho ya sheria pamoja na kuandaliwa kwa sera ya kodi ya kitaifa itakayotoa mwongozo wa kisera na kuhakikisha uthabiti wa marekebisho ya kodi kwa muda mrefu.
Maboresho mengine yanayopendekezwa ni kuimarisha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji mapato, kuongeza ufanisi wa usajili wa walipakodi, kuboresha usimamizi wa misamaha na marejesho ya kodi, pamoja na kuongeza udhibiti wa mapato yatokanayo na uchumi wa kidijitali na forodha.

Iwapo mkakati huo ukitekelezwa kwa ufanisi huenda ukaimarisha upatikanaji wa huduma muhimu kama afya, elimu, maji na uwekezaji katika miradi ya maendeleo. Picha l Wizara ya Fedha
Kwa upande wake, Kamishna wa Usimamizi wa Sera Wizara ya Fedha, Dk Jonson Nyella, amesema maandalizi ya mkakati huo yalifanywa kwa mashauriano na wataalamu wa ndani na msaada wa kiufundi kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Nyela amesema utekelezaji wake utasaidia kupunguza nakisi ya bajeti na kuiwezesha Tanzania kugharamia miradi ya maendeleo kwa fedha za ndani, hasa ikizingatiwa nchi imeingia kwenye uchumi wa kati unaohitaji kujitegemea zaidi.
Tanzania inaungana na nchi kama Kenya, Uganda, Malawi, Sierra Leone, Ghana, Morocco na Rwanda ambazo tayari zimekuwa zikitekeleza utaratibu wa mikakati ya muda wa kati ya ukusanyaji mapato ili kuimarisha uthabiti wa uchumi.
Kwa mwaka wa fedha wa 2025/26 Tanzania inatarajia kukusanya mapato ya jumla ya Sh56.49 trilioni kutoka katika vyanzo mbalimbali ambapo Sh34.1 ni mapato ya kodi.
Latest



