Tanzania yaporomoka kwa ubora wa vivutio vya utalii vya asili duniani

May 21, 2019 1:55 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Waziri huyo, ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Mjini, amesema sababu kubwa iliyosababisha Tanzania kushuka kwa nafasi sita ni kuwepo kwa uharibifu wa mazingira na uvamizi wa mifugo na makazi katika maeneo ya vivutio vya utalii vya asili. Picha|Mtandao.


  • Waziri wa Maliasili na Utalii amesema matokeo ya awali ya utafiti wa vivutio hivyo yanaonyesha Tanzania imeshuka kutoka nafasi ya pili iliyokuwa inashikilia mwaka 2014 hadi nafasi ya nane.
  • Sababu kubwa ni uharibifu wa mazingira na uvamizi wa maeneo ya utalii.
  • Serikali imeanza kuchukua hatua ya kuwaondoa wavamizi katika maeneo hayo.

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amesema matokeo ya awali ya utafiti wa ubora wa vivutio vya utalii vya asili duniani yanaonyesha Tanzania imeshuka toka nafasi ya pili iliyokua inashikilia mwaka 2014 mpaka nafasi ya nane kutokana na uharibifu wa mazingira katika maeneo ya utalii. 

Dk Kigwangalla ametoa ufanunuzi huo bungeni leo (Mei 21, 2019) wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Vunjo, James Mbatia aliyetaka kujua mwaka huu Tanzania inashika nafasi ya ngapi duniani kwa ubora wa vivutio vya utalii duniani na ubora wa miundombinu ya kuchochea vivutio hivyo. 

Katika swali lake, Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha NSSR-Mageuzi amesema mwaka 2014 Tanzania ilikuwa inashika nafasi ya pili kwa vivutio kati ya nchi 133 zenye kushindana kwenye ubora wa vivutio vya utalii duniani ambapo GDP (mchango wa sekta ya utalii katika pato la Taifa) wakati huo ilikuwa asilimia 17 na katika ubora wa miundombinu ya utalii ilikuwa inashika nafasi ya 110 kati 133. 

“Utafiti uliofanyika mwaka 2012 hadi 2014 ulitoa taarifa kwamba Tanzania inashika nafasi ya pili kwa vivutio vya nature (asili) duniani na kutokea kipindi hicho mpaka sasa haujafanyika utafiti mwingine wa kuweza kutupa position (nafasi) nyingine yoyote tofauti na ile ya awali,” amesema Dk Kigwangalla.

“Lakini matokeo ya katikati ya utafiti huo ambao unafanyika kila baada ya miaka mitano  yalitoka (na) Tanzania inaonekana imeshuka toka nafasi ya pili mpaka ya nane kwa vivutio vya nature duniani,” amesema Kigwangalla akielezea matokeo ya awali ya utafiti huo mwingine unaofanyika kati ya 2015 na 2019.

Waziri huyo, ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Mjini, amesema sababu kubwa iliyosababisha Tanzania kushuka kwa nafasi sita ni kuwepo kwa uharibifu wa mazingira na uvamizi wa mifugo na makazi katika maeneo ya vivutio vya utalii vya asili. 


Zinazohusiana: 


Hata hivyo, amebainisha kuwa kazi kubwa imefanyika katika Serikali ya awamu ya tano ya kuwaondoa wananchi ambao wamevamia maeneo hayo lakini pia kupandisha hadhi baadhi ya maeneo ya asili ili yahifadhiwe na kulindwa. 

Utafiti huo unatarajiwa kukamilika mwaka huu ambapo utatoa matokeo kamili yatakayobainisha kama Tanzania imebaki katika nafasi yake au imeshuka.

“Ninaa uhakika watakapofikia conclusion (hitimisho) ya utafiti huo baada ya miaka mitano ambao ni mwaka huu, nafasi ya Tanzania inayoshika katika vivutio vya nature (asili) inaweza kuwa imeongezeka zaidi,” amesema Dk Kigwangalla.

Enable Notifications OK No thanks