Tanzania yamuita balozi wa Marekani kuelezea taarifa inazotoa mtandaoni
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Njena Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge akiwa katika mazungumzo na Kaimu Balozi wa Ubalozi wa Marekani hapa nchini Dk Imni Patterson. Kaimu Balozi huyo ameitwa Wizarani kwa lengo la kutoa ufafanuzi masuala mbalimbali ambayo Ubalozi huo umekuwa ukiyaandika katika mitandao yake ya kijamii bila ya uthibitisho. Mazungumzo halo yamefanyika Ofisi ndogo za Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Jijini Dar es Salaam. Picha| Wizara ya Mambo ya Njena Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
- Katibu Mkuu mambo ya nje asikitishwa na taarifa mbalimbali za ushauri wa kiusafiriki ikiwemo namna Tanzania inavyoshughulikia Corona.
- Serikali imesema taarifa hizo zisizo na uthibitisho zina uwezekano wa kuleta taharuki kwa Watanzania na wageni.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imemuita Kaimu Balozi wa Marekani Dk Imni Patterson kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ambayo ubalozi huo umekuwa ukiyaandika kwenye mitandao yake bila uthibitisho ukiwemo ushauri wa kiusafiri kwa raia wake kuhusu ugonjwa wa Corona.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliyotolewa Mei 26 inaeleza kuwa Patterson amekutana na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Balozi Kanali Wilbert Ibuge jijini Dar es Salaam kutoa ufafanuzi huo.
“Katika mazungumzo hayo katibu mkuu ameeleza masikitiko yake kutokana na namna ambavyo ubalozi huo umekuwa ukitoa taarifa mbalimbali za ushauri wa kiusafiri (travel advisory) zinazoandikwa na kusambazwa na ubalozi wa Marekani kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo suala la namna Tanzania inavyoshughulikia ugonjwa wa COVID-19.,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Msemaji wa wizara hiyo Emmanul Buhohela.
Soma zaidi:
- Ugonjwa wa Corona unavyopukutisha mifuko ya wanunuzi Kariakoo
- Serikali yamuhoji Nabii aliyedai kugundua dawa ya kutibu virusi vya Corona
Buhohela amesema Kanali Ibunge ametolea mfano wa taarifa zilizotolewa na ubalozi huo Mei 13 na Mei 25 kwenye mtandao wa Twitter ambazo zote zimeonekana kukusudiwa kutoa tahadhari kwa raia wa Marekani waliopo nchini na wanaotarajia kuja Tanzania kuwa jiji la Dar es Salaam si salama kutokana na kuwepo na idadi kubwa ya wagonjwa.
“Tahadhari hizo zimeendelea kudai kuwa hospitali nyingi za Dar es Salaam (bila kuzitaja hospitali hizo) zimefurika wagonjwa wa CoVID-19 jambo ambalo si kweli na lina uwezekano wa kusababisha taharuki kwa Watanzania na wageni kutoka nje ya nchi ili hali si ndivyo inavyodaiwa,” amesema Buhohela.
Katika mazungumzo hayo, Kanali Ibuge amemjulisha balozi huyo umuhimu wa kutoa taarifa zilizothibitishwa kwa kuwa Serikali haina “kizuizi cha aina yeyote kwa mabalozi kutafuta na kupata taarifa sahihi na zenye ukweli.”
Latest
