Ukuaji wa demokrasia Tanzania wamkuna Kamala Harris
- Asema yeye na Rais Biden wanajisikia fahari na hatua zinazochukuliwa na Rais Samia katika kuimarisha demokrasia.
- Kutokana na hilo uwekezaji wenye thamani ya Sh1.17 trilioni kufanyika hivi karibuni.
- Rais Samia aahidi kuendeleza ushirikiano, aiomba Marekani kupitia upya mchakato wa viza na kurefusha mkataba wa Agoa.
Dar es Salaam. Huenda hatua ya kuboresha mifumo ya demokrasia nchini Tanzania iikaendelea kutoa matokeo chanya kutoka jumuiya za kimataifa mara baada ya Serikali ya Marekani kusema inafurahishwa na hatua hiyo na kuvutiwa kufanya uwekezaji.
Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris aliyekuwa akizungumza na wanahabari Ikulu jijini Dar es Salaam amesema yeye pamoja na Rais Joe Biden wanafurahishwa na jinsi Rais Samia Suluhu Hassan anavyoimarisha demokrasia na utawala bora nchini.
“Chini ya uongozi wako Tanzania imepiga hatua kubwa katika demokrasia, mimi na Rais Joe Biden tunajisikia fahari kwa hilo, umekubali kufanya kazi na vyama pinzani, umeondoa zuio la mikutano ya hadhara pamoja na kuimarisha uhuru wa kujieleza…, “ amesema Kamala.
Kamala ameongeza kuwa utawala bora huchochea uchumi stahimilivu na unaotabirika jambo ambalo huvutia uwekezaji hivyo Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania na kuwekeza katika nyanja mbalimbali za kiuchumi.
“Nina furaha kutangaza mipango mipya ya Serikali ya Marekani kwanza kupitia Benki ya Exim tutasaini mkataba wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 500 (Sh1.17 trilioni) za Tanzania ambapo zitasaidia uwekezaji katika masuala ya miundombinu, usafiri, teknolojia na na nishati safi, “ amesema Kamala.
Maeneo mengine ambayo Serikali ya Marekani inapanga kufanya uwekezaji ni pamoja na teknolojia ya intaneti yenye kasi ya 5G, usalama mtandaoni, pamoja na uwekezaji katika kiwanda cha kuchakata betri za magari ya umeme ambacho kinatarajiwa kukamilika mwaka 2026.
“Ubia huu utafanya kazi ya kutafuta fursa za ziada katika kanda kwa ajili ya kupata madini mengine muhimu ya kuchenjua katika kiwanda hicho kipya. LifeZone Metals itaanzisha kiwanda hicho mahali ambapo palikuwa na mgodi wa zamani wa dhahabu wa Barrick,” amesema Kamala.
Soma zaidi:
Rais Samia aishukuru Marekani
Rais Samia pamoja na kuishukuru Marekani kwa misaada mbalimbali katika sekta za afya ambayo imekuwa na matokeo chanya amesema Tanzania itaendelea kuwa washirika wa Marekani na kuzingatia makubaliano yaliyopo.
Aidha Rais Samia ameiomba Marekani kuliangalia upya suala la viza pamoja na kurefusha mkataba wa African Growth and Opportunity Act (Agoa) kwa miaka 10 zaidi kwani umekuwa unawarahisishia wafanyabiashara wa Tanzania kufanya shughuli zao Marekani ambapo katika makubaliano ya awali unapaswa kutamatika mwaka 2025.
“Tanzania inaiomba Serikali ya Marekani kutazama upya mkataba wa viza ili kuwawezesha wananchi wa nchi zetu mbili kunufaika na viza ya muda mrefu, tunaamini baada ya maboresho nchi zetu zitapata mafanikio katika sekta za biashara, utalii na uwekezaji,” amesema Rais Samia.
Makamu wa Rais wa Marekani yupo katika ziara ya kikazi ya siku tatu hapa nchini Tanzania ambayo inatarajiwa kukamilika kesho March 31, 2023 ambapo ataelekea nchini Zambia.
Kamala ni kiongozi wa nne wa ngazi ya juu nchini Marekani kufanya ziara ya kikazi hapa nchini Tanzania akitanguliwa na marais wastaafu Barack Obama aliyekuja mwaka 2013, George Bush (2008), na Hillary Clinton aliyekuja Tanzania mwaka 2000.
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akimpokea Mhe. Kamala Harris, Makamu wa Rais wa Marekani Ikulu, jijini Dar es Salaam pic.twitter.com/tpuu5neF09
— ikulu_Tanzania (@ikulumawasliano) March 30, 2023