Marekani yaiwekea Tanzania masharti dhamana ya viza 

October 9, 2025 4:52 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Uamuzi huo umetolewa wakati mazungumzo kuhusu masuala ya uhamiaji na uhamaji yakiendelea kati yao.
  • Hatua hiyo itaongeza maumivu kwa Watanzania wanaotaka kutembelea taifa hilo. 
  • Masharti hayo mapya yanalenga kuongeza ugumu kwa wafanyabiashara.

Dar es Salaam. Serikali ya Marekani imeiweka Tanzania katika mataifa ambayo raia wake watahitajika kuweka dhamana ya viza (visa bond) isiyopungua Sh12 milioni kabla ya kuzuru taifa hilo, hatua itakayopeleka maumivu kwa Watanzania wanaopanga kutembelea nchi hiyo kibiashara na utalii. 

Huu ni mwendelezo wa sera kali za Rais wa Marekani Donald Trump kudhibiti wahamiaji tangu aingie madarakani kwa awamu nyingine Januari 2025.

Katika utaratibu mpya unaoanza Oktoba 23, Watanzania wanaotaka kutembelea Marekani kwa viza za biashara B-1 au utalii B-2 watatakiwa kuweka Dola za Marekani 5,000 (Sh12.03 milioni), 10,000 (Sh25.05 milioni) au 15,000 (Sh36.07) inategemeana na tathmini itakayofanyika wakati wa mahojiano ya kuomba viza. 

Viza za biashara B-1 na utalii B-2 ni aina ya viza za muda mfupi (non-immigrant visas) zinazotolewa na Marekani kwa watu wanaoenda nchini humo kwa shughuli maalum zisizo za ajira au makazi ya kudumu. Madaraja mengine ya viza yakiwemo ya wanafunzi hayajahusishwa katika mpango huo wa dhamana za viza.

Fedha kurejeshwa ukitii masharti

Dhamana ya viza ni kiasi cha fedha kinachowekwa kama hakikisho kwamba mwombaji wa viza atazingatia masharti ya viza yake, yaani hatakaidi muda wa kukaa nchini humo au kufanya shughuli zisizoruhusiwa na aina ya viza aliyopewa.

“Kiwango chote cha dhamana kitarejeshwa kwa muombaji iwapo atafuata masharti yote ya viza za muda mfupi (Nonimmigrant visa) na dhamana ya viza,” imeeleza taarifa ya Idara ya Huduma za Kibalozi ya Marekani.

Miongoni mwa masharti hayo ni wamiliki wa viza kuondoka Marekani wakati au kabla ya muda wa kukaa nchini humo kuisha, mwenye viza kuahirisha kwenda Marekani kabla ya muda wa viza kuisha na muombaji wa viza kuzuiwa kuingia nchini humo. 

Uamuzi huo mpya utakuwa ni maumivu kwa Watanzania ambao walikuwa wamepanga kufanya safari zao Marekani kwa kuwa watahitajika kutafuta fedha zaidi ya zile walizopanga kutumia kwa ajili ya safari ili kuweka dhamana hiyo. 

Serikali ya Tanzania imesema imepokea taarifa hiyo na kwamba kwa sasa mazungumzo kuhusu masuala ya uhamiaji na uhamaji bado yanaendelea na Marekani.

Tanzania yaanza mazungumzo

“Serikali inapenda kuuhakikishia umma kwamba itaendelea na majadiliano hayo na Serikali ya Marekani kwa njia za kidiplomasia ili kutafuta suluhisho lenye kuzingatia usawa, heshima, na maslahi ya pande zote mbili kwa kuzingatia uhusiano wetu mzuri uliodumu kwa zaidi ya miongo minne,” alisema Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa Oktoba 08,2025.

Aidha, Serikali imesisitiza kuwa hatua hiyo ya Marekani haitabadilisha uhusiano wa kirafiki uliopo kati ya nchi hizo mbili, kwani uhusiano huo umejengwa juu ya misingi ya urafiki, ushirikiano na kuheshimiana.

Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanaeleza kuwa hatua hiyo ya Marekani itaongeza ugumu wa kwa wafanyabiashara na watalii kutoka Tanzania wanaosafiri kwenda Marekani.

Mchambuzi wa masuala ya kidiplomasia, Ocheck Msuva, amesema licha ya kuwa Tanzania inaweza isiwe na watalii wengi wanaoenda Marekani, lakini wapo baadhi ya watu wanaotumia aina hiyo ya viza zilizowekewa vikwazo. 

‘Tanzania haiwezi kulipiza kisasi’

“Nadhani Serikali ya Marekani imeangalia zaidi maslahi yake, kwa kuwa sera yao ya mambo ya nje inatanguliza Marekani kwanza,” amesema Msuva.

Alipoulizwa iwapo Tanzania inaweza kujibu mapigo kwa kuweka vikwazo vya kiviza, Msuva amesema Serikali haiwezi kuchukua hatua kama hiyo kwa kwa sababu ya malengo ya kukuza sekta ya utalii na kuvutia uwekezaji. 

“Serikali imelichukulia hili kama fursa ya mazungumzo ya kidiplomasia, si kama changamoto ya kisiasa…pengine kuna mambo fulani fulani ambayo wao watakuwa wameyaona ambayo hawajaweka wazi,” amesema Msuva. 

Mbali na Tanzania nchi nyingine ambazo raia wake watatakiwa kuweka dhamana ya viza (visa bond) ni Mali, Mauritania ,Sao Tome na Principe, Gambia, Malawi na Zambia.

Hata hivyo, Serikali imewataka wananchi kuendelea kufuata taratibu za kawaida za maombi ya viza kupitia Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania au katika maeneo mengine wanakoishi waombaji wa Kitanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks