Tanzania yajifua kudhibiti ajali za barabarani
- Maafisa usalama kutoka nchi 20 wakutana kutafuta mzizi.
- Juhudi mbalimbali zaendelea kufanyika kumaliza ajali hizo.
Mwanza. Huenda siku za hivi karibuni Tanzania ikashuhudia kupungua kwa ajali za barabarani mara baada ya kufanyika kwa semina ya nchi zaidi ya 20 kutoka barani Afrika na Ulaya iliyolenga kubadilishana uzoefu wa jinsi ya kupunguza ajali hizo.
Kwa mujibu wa kitabu cha hali ya uchumi kwa mwaka 2022 kinachotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (Nbs) ajali za barabarani nchini Tanzania zimeongezeka kutoka 1,052 zilizorekodiwa mwaka 2021 hadi ajali 1,405 mwaka 2022.
Mkuu wa usalama barabarani nchini, Ramadhan Ng’anzi aliyekuwa akizungumza kwenye semina hiyo (jana) Novemba 27, 2023 jijini Mwanza amesema juhudi mbalimbali zinaendelea kufanyika ili kupungunguza ajali hizo nchini.
“Tunaendelea vizuri na tangu safari za mabasi kwenda mikoani usiku zianze hatujapokea taarifa yoyote ya ajali, hivyo maboresho ni makubwa na tunajiathidi kuhakikisha ajali hizi zinapungua,” amesema Ng’anzi.
Baadhi ya wahudhuriaji wa semina ya usalama barabarani iliyofanyika jijini Mwanza Novemba 27, 2023.Picha|Mariam John.
Semina hiyo iliyoandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali linalotoa elimu ya usalama barabarani (TARS) itafanyika kwa siku tano, ikiwakutanisha maafisa usalama barabarani kutoka mataifa mbalimbali ya barani Afrika na Ulaya ikiwemo Rwanda, Burundi, Botswana na Uingereza.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini aliyekuwa akizungumza katika semina hiyo amesema anatumaini ujio wa semina hiyo utaendelea kuboresha matumizi bora ya barabara na kuongeza uelewa kwa madereva.
“Ajali za barabarani zinatokana na sababu za kibinadamu ambazo aidha ni za dereva mwenyewe pia kuna matatizo ya vyombo vya moto vyenyewe, uchakavu pamoja na miundombinu kuwa mibovu…
…Matarajio yetu kwa semina hii itaendelea kuboresha huduma na taratibu za matumizi ya barabara zetu na watumiaji wa vyombo vya moto,” amesema Sagini.
Soma zaidi:Hatari inayowakabili wauzaji, watumiaji mafuta ya vibaba Mwanza
Naye Mkuu wa idara ya mipango kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoani Mwanza Mhandisi Magesa Mwita, ameeleza kuwa barabara wanazojenga zinazingatia salama na alama ili kulinda watumiaji wake.
“Tunajitahidi kuweka alama za barabarani maeneo yote yanayo hitajika lakini changamoto ni kuibiwa, mkakati uliopo kwa sasa ni kutengeneza alama hizo nchi nzima na kuzipaka rangi,” amesema Mwita.
Latest