Tanzania mdogo mdogo kuunda satelaiti yake

May 18, 2023 11:52 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Rais Samia Suluhu Hassan akibonyeza Kitufe kuashiria ufunguzi wa Mradi wa Minara ya kurusha matangazo ya Televisheni Ardhini (DTT) ya Kampuni ya Azam Media kwenye hafla iliyofanyika katika Makao Makuu ya Ofisi hizo zilizopo Barabara ya Mandela Jijini Dar es Salaam. Picha | Ikulu.


  • Serikali iko katika mazungumzo na wadau kufanikisha mchakato wake.
  • Rais Samia asisitiza kuwa Tanzania itakuwa na satelaiti yake. 

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali iko katika mazungumzo na wadau kujenga satelaiti yake ili kuboresha sekta ya mawasiliano na kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi.

Rais Samia amesema Serikali imejipanga kufanikisha suala hilo ambalo ni sehemu maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani.

“Mnajua kama Serikali tunajipanga kuja na shughuli ya satelaiti ambayo niwahakikishie kuwa itakuwepo Tanzania. 

“Tunajipanga vizuri tumeanza mazungumzo tutajenga satelaiti Tanzania,” amesema Rais wakati wa Uzinduzi wa mradi wa minara ya kurusha matangazo ya televisheni Ardhini (DTT) ya kampuni ya Azam Media Limited, Tabata Dar es Salaam leo Mei 18,2023.

Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema dunia imepiga hatua kubwa ya maendeleo, hivyo kama nchi hatuna budi kujiendeleza katika teknolojia za kisasa zitakasaidia kuboresha maisha.

Novemba 10, 2022 Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Mathew Kundo alisema Serikali inatambua umuhimu wa nchi kuwa na satelaiti na kwamba katika mwaka huu wa fedha  imeanza kuandaa utaratibu wa awali utakaowezesha kuunda na kurusha satelaiti yake angani.

Alisema ili kuwezesha kufikia azma hiyo tayari imeunda andiko dhana na kuunda timu ya watalaamu watakaoshauri aina ya satelaiti itakayorushwa angani itakayoendana na mahitaji halisi ya nchi.

Kundo alisema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Bahi, Kenneth Nollo aliyetaka kujua ni lini Serikali itaanza programu ya kuunda na kurusha setelaiti angani.

“Ni matarajio kuwa timu hiyo itakamilisha kazi ya uchambuzi na kuwasilisha mapendekezo yake Serikalini kwa hatua za kimaamuzi ndani ya mwaka huu wa fedha,” alisema Kundo.

Kwa mujibu wa Kondo, hadi sasa Afrika ina takriban satelaiti 50, na kuanzia mwaka 2016 ni satelaiti 20 tu ambazo zimekuwa angani, na kati ya hizo, ni tisa tu ambazo zimetengenezwa na zina taswira ya Kiafarika.

Misri ilikuwa nchi ya kwanza katika bara la Afrika kutuma satelaiti angani mwaka 1998 huku Kenya ikiwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki. 

Aidha, Rais Samia ameitaka Wizara ya Habari,  Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutafuta teknolojia mbadala ya minara ya simu na mawasiliano ambayo kwa sasa inaongezeka kwa kasi. 

“Tatizo nililonalo kichwani mwangu ni moja nikamwambia waziri (Nape Nnauye) minara 700 na mipya, kuna minara ambayo ipo ndani ya nchi, kuna minara ya Azam Media inakwenda kujengwa, kuna wengine watakuja kujenga nikamuuliza waziri hakuna teknolojia ya kuchanganya yote haya kwa sababu nchi hii itajaa minara,” amesema Rais Samia. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW