Rais Samia: Tozo za miamala ya simu ni kwa ajili ya maendeleo

July 27, 2021 4:28 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema tozo hiyo ipo pale pale ila wataangalia njia bora isiyoumiza. 
  • Ni pamoja na barabara za vijijini na miradi ya maji.
  • Amesema amesikia vilio vya Watanzania na Serikali itavifanyia kazi.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amejibu malalamiko ya Watanzania juu ya ongezeko la tozo kwenye miamala ya simu akieleza kuwa zitaendelea kuwepo kwa ajili ya kuleta maendeleo ila kwa sasa wataangalia njia bora isiyoumiza. 

Rais Samia ameeleza leo (Julai 27, 2021)  Ikulu jijini Dar es Salaam kuwa fedha zinazokatwa kwenye miamala hiyo zimepangwa kutumika katika shughuli za maendeleo ikiwemo kujenga barabara za vijijini na kuendeleza miradi ya maji kwa ajili ya wananchi.

Kiongozi huyo amesema “tozo hizo zipo” na kueleza kuwa Serikali imepokea maoni ya wananchi baada ya kuyakusanya kwa wiki nzima na kisha kuwataka mawaziri walifanyie kazi jambo hilo.

“Nachotaka kusema makato haya tuliyaweka kwa nia njema tu. Nchi yetu sasa hivi wakulima wameamka na kilimo kikubwa lakini wakivuna wanashindwa kutoa mazao yaliko kuleta kwenye masoko. Tatizo ni njia za vijijini hakuna. Sehemu ya fedha hii au sehemu kubwa itakwenda kwenye kujenga njia za vjijini,” amesema. 

Rais Samia amesema fedha nyingine zitaboresha huduma za maji kwa kuwa hadi sasa Serikali imetoa huduma ya maji kwa karibu robo tatu au asilimia 74.

“Niwaambie Watanzania tumesikia vilio, tunakwenda kuangalia njia nzuri za kwenda na hili  lakini hizi tozo nataka niseme zipo ila tutaangalia njia nzuri ambayo haitoumiza watu,” amesema Rais Samia.

Tangu Julai 15, kumekuwepo na malalamiko lukuki kwa watumiaji wa huduma za simu Tanzania baada ya Serikali kuanza kutoza tozo mpya kwenye miamala ya simu ambazo wengi wamesema zinawaumiza kwa kuongeza gharama za maisha. 

Baada ya kukithiri kwa malalamiko hayo Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk Faustine Ndugulile waliwaeleza wanahabari kuwa Rais Samia ameagiza wafanyie kazi malalamiko hayo.

Hata hivyo, kauli ya Rais Samia leo kuwa tozo hizo zitaendelea kuwepo huenda bado ikaendelea kupeleka manung’uniko kwa watumiaji wengi wa huduma hizo ambazo zimesaidia sana kuongeza ujumuishi wa kifedha nchini. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW