Biashara ya mifugo inavyowainua vijana kiuchumi Arusha
- Imewasaidia kujiingizia kipato na kuendesha maisha.
- Masoko, magonjwa bado changamoto.
Arusha. Ufugaji ni miongoni mwa shughuli ya kiuchumi inayofanywa na watu wengi jijini Arusha ikiwawezesha maelfu ya wakazi wa jiji hilo kujiingizia kipato na kuendesha maisha.
Mkoa huo una jumla ya mifugo milioni 5.7 wakiwemo ng’ombe wa asili 1.6 milioni, ng’ombe wa maziwa 198,330,mbuzi milioni 2 na kondoo milioni 1.8 kwa mujibu wa takwimu zilioainishwa katika tovuti rasmi ya jiji hilo.
Mifugo hiyo huchungwa katika eneo lenye ukubwa wa hekta 1,065,392 sawa na asilimia 31 ya eneo lote la Mkoa huo ikiwawezesha wafugaji wakubwa na wadogo kupata malisho kwa ajili ya mifugo yao.
Kati ya hao wapo wanaofanya ufugaji huo kwa njia ya kisasa inayohusisha kuwanenepesha kisha kuwauza huku wengine wakifuga kiasili na kuwauza pale tu wanapohitaji fedha
Miongoni mwa wanufaika hao yupo Simon Lukumay kijana msomi wa Shahada ya Kwanza ya Biashara katika Fedha aliyegeukia biashara ya ununuaji na unenepeshaji wa mifugo ikiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Lukumay aliyeanza biashara hiyo miaka minne iliyopita anasema kilichomsukuma kufanya biashara hiyo ni kiu ya kuleta mabadiliko katika jamii yake ambayo imejikita kufuga kwa ajili ya ufahari na kuuza pale wanapohitaji fedha.
“Mimi ni mmasai na kama unavyojua wamasai ni wafugaji…nilivutiwa tu na bishara hii ili niondoe ule mtazamo wa kumiliki ng’ombe wengi au mbuzi wengi alafu hela hamna, wengi wameukalia utajiri lakini hawajui,”Amesema Lukumay.
Mbali na malisho bora, mifugo inahitaji kupata maji safi na salama ili iweze kukua na kunenepa kabla ya kupelekwa sokoni kwa ajili ya mauzo.Picha|Esau Ng’umbi.
Mbali na sababu hiyo Lukumay anasema alijiingiza katika biashara hiyo baada ya kuona mshahara anaoupata kutoka kwenye kazi aliyoisomea hautoshelezi mahitaji yake.
“Nimeona ninachopata ofisini na ninachopata kwenye ufugaji havilingani huku kwenye ufugaji napata zaidi na hakuna kazi nyingine inayoweza kunilipa kiasi kama hicho,” ameongeza Lukumay.
Wakati ‘mtonyo’ukimsukuma Lukumay kufanya biashara ya mifugo kwa Nailenya Morrel (23) muuzaji mwingine wa mifugo sababu ni tofauti yeye alijiingiza kwenye biashara hiyo kwasababu anaipenda.
“Mimi hii ‘mishe’ naipenda ndio maana unaona niko hapa (sokoni) nauza mifugo yangu kisha narudi kijijini kusaka wengine, wiki ijayo au ile nyingine utaniona tena hapa,” anasema Nailenya.
Safari yao ilianzaje?
Lukumay alianza rasmi biashara ya kuuza mifugo mwaka 2021 ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kumaliza Shahada ya Kwanza ya Biashara katika Fedha (Bachelor of Commerce in Finance) kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kurudi jijini Arusha.
Alianza na mbuzi 40 aliowanunua kwa Sh2 milioni ambapo kwa wastani kila mbuzi alimnunua kwa bei ya Sh 50,000.
Kama ilivyo kwa wafugaji wengine, Lukumay alitafuta eneo maalum na kujenga boma ya kufugia mifugo hao pamoja kumlipa mchungaji aliyeipeleka machungani, kuwapa maji na kuwasafisha ilipohitajika.
Miezi nane baadae mbuzi hao walinenepa na aliwauza kwa Sh6 milioni katika miongoni mwa masoko yaliyopo jijini hapa.
“Baada ya kuwalisha vizuri mbuzi wangu walinepa na kuongezeka thamani kila mbuzi niliuza kwa wastani wa Sh80,000 hapo namaanisha kuna ambaye aliuzwa75, 000 wengine 90,000 ndo nikapata kiasi hicho cha fedha (Sh 6 milioni),” amesema Lukumay.
Miaka miwili iliyofata Lukumay aligeukia biashara ya ng’ombe ambapo aliwanunua wakiwa wadogo (ndama) pekee na kuwanenepesha akilenga kuwauza kwa faida mara dufu mwishoni mwa mwaka 2024 watakapokomaa kuwa wakubwa.
Alinunua ndama 45 kwa Sh13 milioni ambapo kila ndama akinunua kwa Sh 200,000 hadi 300,000 na baada ya miaka miwili ya malisho, chanjo na dawa ngombe hao aliwauza kwa Sh45 milioni ambapo kila ngombe aliuzwa kwa wastani wa Sh1 milioni.
“Nilinunua ndama kwa sababu bado wanakua na wana nguvu hata kiangazi kikija wanaoathirika ni majike wanaozaa na wanaonyonyesha, ndama na madume huwa hawaathiriki,” anasema Lukumay.
Kwa mujibu wa Abdallah Ulega, Waziri Wizara ya Mifugo na uvuvi, sekta ya mifugo kwa mwaka 2022 ilikua kwa asilimia 5 na kuchangia asilimia 6.7 kwenye pato la Taifa ikichangiwa na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa za mifugo ya nje ya nchi.
Mbali na kukua kwa sekta hiyo, Waziri Ulega aliyekuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2024/25 alisema Serikali itaendelea kutekeleza programu ya Jenga Kesho kuwawezesha wanawake na vijana kufanya ufugaji kibiashara.
“Wizara itaendelea na utekelezaji wa programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) kwa kuimarisha vituo nane vilivyopo na kuanzisha vituo vipya vitano ambapo vijana na wanawake 390 watanufaika katika sekta ya mifugo,” amesema Ulega.
Hatua kwa hatua unenepeshaji wa mifugo
Wakati Nailenya yeye huuza mifugo bila kunenepesha hatua inayomfanya kuingiza faida kiduchu, Lukumay ameitaja mbinu hiyo kama namma pekee ya kujipatia fedha za ziada.
Baada ya kununua mifugo Lukumay hutafuta daktari ambaye huipima na kuwatibu magonjwa ambao wanakuwanayo ikiwemo minyoo.
Baada ya matibabu ya awali mifugo hiyo huwekwa chini ya uangalizi kwa muda wa wiki moja ili kubaini magonjwa mengine ambayo hujificha, kama hawana magonjwa daktari huwapatia chanjo kuwalinda na magonjwa mengine kama ‘bone marrow’
Hatua za matibabu zikikamilila mifugo hiyo husafishwa na kupewa malisho kama ilivyo mifugo mingine kwa kipindi cha miezi saba mpaka nane tangu ununuliwe.
Licha ya aina hii ya ufugaji kuonekana Ina gharama, Lukumay anasema gharama za uendeshaji hazizidi asilimia tano ya faida ambayo hutarajia kupata katika kila msimu wa mauzo.
“Ukipiga mahesabu ya kumlipa daktari wa mifugo, madawa, malisho pamoja na mchungaji unakuta dharama za uendeshaji haizidi asilimia tano ya bei nitakayoenda kuwauza…
…Mfano mauzo ya juzi ya Sh 45 milioni niliyoyafanya gharama za uendeshaji hazikuzidi Sh2 milioni kwa harakaraka hapo utaona ni biashara yenye tija,” amesema.
Ng’ombe mwenye afya bora hununuliwa kwa fedha nyingi zaidi kuliko walioodhoofu kwa njaa au magonjwa,Picha Esau Ng’umbi.
Masoko, magonjwa changamoto
Nailenya ameiambia Nukta Habari kuwa licha ya faida ya kipato cha Sh500,000 anayoipata katika kila mnada baada ya kuuza mbuzi 20 masoko bado ni changamoto kwake.
“Kwa sisi wafanyabiashara ambao bado mtaji wetu ni ndogo tunapata shida kuuza katika masoko haya ya kawaida ambapo wanunuaji wakubwa ni wananchi wa kawaida ambapo tinawauzoa kwa bei ya rejareja’” amesema Nailenya.
Kwa Lukumay masoko si changamoto kubwa sana kama ilivyo kwa wafanyabiashara wengine, kutokana na kujitengenezea jina linalomuwezeha kuuza mifugo yake katika masoko makubwa ikiwemo la duka bovu yanayokutanisha watu kutoka mikoa mbalimbali au hata nje ya nchi.
Changamoto kubwa kwa mfanyabiashara huyo ni magonjwa ambayo hushambulia sana mifugo wakati wa kiangazi ambayo wakati mwingine humfanya atumie gharama kubwa kwa ajili ya dawa
Hata hivyo, mfugaji huyo amesema changamoto anazopitia ni za kawaida kulinganisha na faida ambayo huipata katika kila msimu wa mauzo.
Ujenzi wa vibanda husaidia wafugaji kutunza mifugo midogo ikiwemo mbuzi na ndama baada ya kuinunua.Picha|Lucy Samson
Ni mgodi uliojificha
Kwa vijana wanaotamani kuingia katika biashara ya mifugo Lukumay amewashauri kujikuta katika upande wa unenepeshaji na uuzaji kwani hauhitaji muda mwingi wa uangalizi na kupata faida ni uhakika.
“Hii biashara ni kama mgodi haiihitaji uwepo wako kwa masaa mengi, unaweza kuendelea na mishe zako nyingine na bado upigaji wa hela ni wa uhakika” amesema Lukumay.
Licha ya uhakika wa faida Sunday Gimre mfugaji mwingine jiji hapa amewashauri vijana kuandaa mtaji wa kutosha kabla ya kuingia katika biashara hiyo ili waweze kujipatia faida maradufu.
“Ili utoboe kwenye uneneoeshaji na uuzaji wa mifugo kama mbuzi ni vyema kuanza na mtaji wa Sh2 milioni ndiyo utaniona faida vizuri chini ya hapo utafanya lakini faida hiatakuwa kubwa.
Mbali na mtaji ameyataja masuala kama umakini wa kuchagua mifugo bora, kuandaa eneo la malisho na kutafuta mchungaji mwaminifu kama masuala ya misingi ya kuzingatia katika biashara hiyo.