Tanzania kuboresha huduma za afya kuhudumia watoto njiti
- Yasema inaimarisha miundombinu ya wodi maalumu na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya.
- Yatoa wito kwa wajawazito kuhudhuria kliniki na kujifungulia hospitali.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema inaendelea kuimarisha huduma za kuwatunza watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) ili kuboresha matunzo ya kitabibu, lishe na malezi kwa watoto hao wanapokuwa hospitalini na majumbani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Novemba 17, 2025 na Wizara ya Afya imeeleza kuwa huduma zinazoimarishwa ni pamoja na miundombinu ya wodi maalum za watoto wachanga, kununua na kusambaza vifaa tiba, pamoja na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya.
Hayo yamebainishwa wakati ulimwengu unaadhimisha siku ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (World Prematurity Day) ikiwa lengo ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu changamoto zinazowakabili watoto njiti ambao huzaliwa kabla ujauzito haujakamilisha wiki 37 za umri wa mimba.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, tuwapatie mwanzo bora watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya wakati kwa afya bora ikiwa inalenga kuhakikisha kila mtoto njiti anapewa fursa ya kuishi, kukua na kustawi kwa kupata huduma stahiki za kitabibu, lishe bora, na uangalizi wa karibu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) takribani watoto milioni 15 huzaliwa kabla ya wiki 37 za ujauzito kila mwaka duniani, na zaidi ya watoto milioni moja hupoteza maisha kutokana na matatizo yanayohusiana na kuzaliwa kabla ya wakati.
WHO inasisitiza kuwa watoto njiti wako katika hatari kubwa ya kupata matatizo ya kiafya yanayohatarisha maisha kama shida ya kupumua, maambukizi na kushuka kwa joto la mwili.
Nchini Tanzania takwimu zinaonesha kuwa takribani mtoto mmoja kati ya 10 sawa na zaidi ya watoto 250,000 huzaliwa kabla ya wakati kwa mwaka, hali inayohitaji juhudi za pamoja katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto.
Hata hivyo, Wizara ya Afya imetoa wito kwa jamii kuhakikisha wajawazito wanahudhuria kliniki mapema na mara kwa mara, na kuhakikisha kila mama anajifungulia katika kituo cha kutolea huduma za afya ili kupunguza sababu za watoto kuzaliwa kabla ya wakati
Latest