Tanzania, Angola kuimarisha biashara na usafirishaji
- Ni fursa kwa wananchi kutumia ushirikiano huo unaotarajiwa kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa pamoja na kukuza biashara kukuza kipato binafsi na kuchechemua uchumi wa nchi.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania na Angola zimesaini mikataba minne ya makubaliano kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kupitia sekta za biashara na usafirishaji hatua inayolenga kuongeza uwekezaji na utalii kwa mataifa hayo mawili.
Hatua hiyo imefikiwa leo, Oktoba 29, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, baada ya mazungumzo kati ya Rais Samia Suluhu Hassan na Rais João Lourenço wa Angola, kufuatia ziara yake ya siku tatu ya kikazi nchini.
Akizungumza mara baada ya makubaliano Rais Samia amesema ushirikiano huo unahusisha ukarabati wa reli ya Tazara upande wa Tanzania na reli ya Benguela inayopitia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Zambia kwa upande wa Angola.

Amesema miradi hiyo inalenga kuunganisha ukanda wa Lobito na ukanda wa kati unaounganisha na Bandari ya Dar es Salaam ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kukuza biashara.
“Moja wapo wapo ya kikwazo kikubwa cha biashara barani Afrika ni changamoto ya miundombinu ya usafiri na usafirishaji, hivyo tumekubaliana kutatua changamoto hii kwa kuunganisha korido za Lobito na Dar es Salaam,” amesema Rais samia.
Fursa kwa Watanzania
Hii ni kwa mara ya kwanza Rais Lourenço kutembelea Tanzania tangu Rais wa kwanza wa Taifa hilo, Agostino Neto alipofanya hivyo mwaka mwaka 1979 wakati wa harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.
Ujio wake na makubaliano haya mapya ni fursa kwa wananchi kutumia ushirikiano unaotarajiwa kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa pamoja na kukuza biashara, uwekezaji na utalii kati ya Tanzania na Angola kuongeza kipato binafsi na kuchechemua uchumi baina ya mataifa hayo.
Kwa upande wake Rais Lourenço ametoa wito kwa kwa mataifa mengine ya Afrika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi ndani ya bara ili kutumia fursa zilizopo na kupunguza utegemezi mkubwa wa biashara na uwekezaji kutoka Ulaya, Amerika na Asia.
“Tumekua tukiacha uhusiano na nchi zetu ambazo ni ndugu, nchi za Kiafrika ambazo zina kitu cha kuweza kusaidia katika kuleta maslahi ya pamoja, ambapo wote tunaweza kunufaika,” amesema Rais Lourenço
Mbali na mambo mengine, marais hao wawili wamekubaliana kufungua tena ubalozi wa Tanzania nchini Angola ili kuendelea kudumisha uhusiano wa kihistoria na kidugu uliopo kati ya Angola na Tanzania, pamoja na kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi ili kuchochea maendeleo ya mataifa yote kwa maslahi ya wananchi.