Tanzania yaahidi kudumisha ushirikiano wa kihistoria na Angola
- Ni pamoja na kushirikiana kwa karibu zaidi katika sekta za nishati mbadala, uchumi wa buluu, biashara ya kikanda.
- Rais Samia amekuwa kiongozi wa kwanza wa Tanzania kuhutubia Bunge la Angola.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wake wa kihistoria na Angola kwa kuwekeza zaidi katika sekta za kimkakati zikiwemo biashara, nishati mbadala, usafirishaji, kilimo, madini na maendeleo ya vijana.

Akihutubia Bunge la Angola katika ziara yake ya kiserikali iliyoanza Aprili 7 na kuhitimishwa Aprili 9, Rais Samia amesisitiza kuwa uhusiano baina ya mataifa haya mawili umejengwa juu ya msingi imara uliowekwa na waasisi Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Agostinho Neto wa Angola.
“Angola kwetu ni kama mojawapo ya nyumba nyingi ambazo mtu anaweza kuwa nazo. Haijalishi ni muda gani haujatembelea nyumba hiyo, lakini kila unaporudi joto na kumbukumbu nzuri huongezeka,” amesema Rais Samia akisisitiza ukaribu uliopo baina ya Angola na Tanzania.

Katika hotuba yake ya kihistoria akiwa kiongozi wa kwanza wa Tanzania kuhutubia Bunge la Angola Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kushirikiana zaidi katika sekta za nishati mbadala, uchumi wa buluu, biashara ya kikanda kupitia eneo huru la biashara Afrika (AfCFTA), pamoja na kuunganisha maeneo ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini kupitia usafirishaji wa bidhaa.
Aidha, amegusia wajibu wa mataifa haya kuwekeza kwa vijana kwa kuwajengea uwezo kupitia elimu, teknolojia, mafunzo ya stadi na ujasiriamali.
“Vijana wetu wana ndoto kubwa, vipaji na ubunifu. Tukiwawezesha, tunaweza kulifikisha bara la Afrika katika viwango vya juu vya maendeleo,” alieleza Rais Samia.
Aidha, Rais Samia alitumia nafasi hiyo kuyarai mataifa barani Afrika kuungana katika kukabiliana na changamoto mpya kama umasikini, ukosefu wa usawa na maendeleo duni.

Pamoja na kutambua mchango wa Angola katika kukuza amani Kusini mwa Afrika na Rais Samia alitambua ameahidi ushirikiano wa Tanzania kupitia Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili kutafuta suluhu kwa njia za Kiafrika.
Katika siku zake tatu nchini Angola, Rais Samia alifanya mazungumzo ya ana kwa ana na mwenyeji wake Rais João Lourenço, kutembelea miradi ya kimkakati ikiwemo ya nishati na miundombinu, na kushuhudia kusainiwa kwa mikataba ya ushirikiano.
Ziara hii imeelezwa na wachambuzi kuwa ni hatua muhimu katika kufungua ukurasa mpya wa mahusiano kati ya Tanzania na Angola, ikizingatiwa mchango wao katika historia ya ukombozi wa Afrika na dhamira yao ya sasa ya kuendeleza ushirikiano wa maendeleo.
Latest



